Aliyasema hayo juzi katika salamu zake katika sherehe za kuukaribisha mwaka mpya alizowaandalia mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa nchini.
Alisema kuwa safari hii tahadhari imechukuliwa ili kuhakikisha kuwa kinachoafikiwa kinakuwa suluhisho la kudumu la matatizo ya kisiasa, ambayo yamekuwa yakivikumba visiwa hivyo tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
“Mazungumzo ya muafaka kati ya Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusiana na hali ya kisiasa Zanzibar, yanakaribia kufikia mwisho. Tunatarajia kuwa safari hii tutafanikiwa kujenga msingi imara wa kufanya mpasuko wa kisiasa Zanzibar kuwa historia,” alisema.
Rais Kikwete aliwashukuru mabalozi na wawakilishi hao kwa kuunga mkono juhudi na mchakato wa kusaka suluhu ya kisiasa visiwani Zanzibar na kuelewa ugumu wa jitihada hizo.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete inaibua matumaini kutoka kwa Wazanzibari kuhusu mustakabali za nchi uliozingirwa na migawanyiko ya kisiasa, ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa kikwazo kwa maendeleo ya visiwa hivyo.
Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, siasa za Zanzibar zimekuwa ni za ushindani wa hali ya juu kutokana na nguvu zinazokaribiana za vyama vikubwa visiwani humo; CUF na CCM, jambo ambalo limefanya matokeo ya uchaguzi kupishana kwa asilimia ndogo.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha migongano na kutoelewana huku CUF ikidai kila mara kupokonywa ushindi na CCM ikisisitiza kuwa inashinda kihalali.
Mabishano hayo ya kisiasa yameshawahi kusababisha maandamano ya wafuasi wa CUF mwaka 2001 yaliyoandamana na kupotea kwa maisha ya watu kadhaa baada ya wafuasi hao kupambana na polisi.
Mtafaruku uliotokea baada ya mauaji hayo, ulisababisha baadhi ya watu kisiwani Pemba kukimbilia Kenya kutokana na hofu ya kulipiziwa kisasi kwa visa vya kisiasa.
Alipoingia maradakani mwaka 2005, Rais Kikwete aliahidi kutafuta suluhu ya kudumu kwa matatizo ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kuanzisha mazungumzo hayo ambayo yamedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Wakati fulani, mazungumzo hayo yaliingia majaribuni baada ya CUF kutishia kujitoa kutokana na kauli zilizowahi kutolewa na kiongozi mmoja wa CCM zikiashiria kuwa, chama hicho hakiwezi kukubaliana na kuundwa kwa serikali ya mseto, ambalo ndilo dai la msingi CUF na hoja inayoungwa mkono na wachambuzi kadhaa wa masuala ya kisiasa.
Kuhusu suala la amani kwa ujumla, Rais Kikwete aliwaambia mabalozi kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Tanzania imeendelea kuwa na amani na utulivu wa kujivunia.
“Na hii ni kwa sababu Watanzania wanajiona wanaongozwa vizuri,” alisema na kuongeza kuwa, serikali imekuwa ikithamini uhuru wa watu, hasa uhuru wa kutoa mawazo yao, kujumuika, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kuabudu dini mtu aipendayo,” alisema.
Aliwaahidi kuwa kuendeleza utawala bora itakuwa moja ya ajenda muhimu za serikali kwa mwaka huu.
Alisema kuwa serikali itaendelea kutoa fursa kwa watu kushiriki katika siasa, na kwa kuheshimu na kuthamini umuhimu wa mazungumzo, serikali ya chama chake itapanua zaidi wigo wa mazungumzo na kujumuisha vyama vingine vya siasa.
Akizungumzia hali ya Kenya, Rais Kikwete alisema Tanzania inasikitishwa na kilichotokea huko na kuwaomba wanasiasa nchini humo kujizuia kutoa kauli zinazochochea uhasama zaidi na badala yake wajikite katika mazungumzo kama njia muafaka ya kumaliza matatizo yao.
Alisema Tanzania inaguswa na hali ya Kenya kwa sababu kinachotokea nchini humo kinaiathiri pia Tanzania ambayo ni jirani wa Kenya.