Licha ya kutuma salamu za kuwataka wanasiasa nchini humo kutafuta njia za kumaliza vurugu hizo haraka, Rais George Bush, pia amemtuma waziri mdogo wa mambo ya nje, anayeshughulikia Afrika, Jendayi Frazer.
Frazer alikuwa anatarajiwa kuwasili Nairobi jana na alipanga kukutana na Rais Mwai Kibaki, ambaye ushindi wake unalalamikiwa na aliyekuwa mgombea urais kupitia ODM, Raila Odinga.
“(Kibaki na Odinga ) Wana fursa ya kukaa pamoja na kukubaliana njia za kumaliza matatizo yaliyojitokeza,” Rais Bush aliiambia Reuters, katika mlolongo wa juhudi za kimataifa kumaliza mgogoro ulioikumba Kenya.
Ufaransa nayo ilijiunga katika jitihada hizo kwa waziri wake wa Mambo ya Nje, Bernard Kouchner, kutoa kauli kali dhidi ya kulichotokea nchini humo.
“Kura ziliibwa au la? Nafikiri ziliibwa, wengi wanafikiri hivyo, Wamarekani wanafikiri hivyo, Waingereza pia, na wanaifahamu nchi hiyo vizuri,” alisema.
Wakati huo huo, Benki ya Dunia imeonya kuwa vurugu zinazoendelea, zitauumiza uchumi si wa Kenya tu, bali pia na majirani zake.
Tayari nchi za Uganda, Rwanda na Burundi zimeanza kuwa na upungufu wa bidhaa, hasa mafuta, baada ya bandari ya Mombasa wanayoitegemea kupitishia bidhaa zake, kufungwa.
Jana, Jiji la Nairobi lilionekana kuanza kurejea katika hali ya kawaida, kukiwa na magari mengi kidogo, lakini polisi waliendelea kupambana na wafuasi wa ODM, waliokuwa wamepanga kukusanyika katika viwanja vya Uhuru.
Hata hivyo, kwa muda mrefu, viongozi wa ODM walikuwa katika ofisi zao katika jengo la Pentagon, wakiwapokea wageni wa kimataifa ambao wamefika kusaidia kutafuta suluhu ya matatizo yaliyojitokeza.
Wakati huo huo, Rais Kibaki alikutana na Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini, na kubainisha kuwa yupo tayari kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Rais Kibaki alimhakikishia Askofu Tutu kuwa, amedhamiria kushiriki katika mazungumzo ya kisiasa na vyama vingine katika kutafuta suluhu ya matatizo hayo.
Katika hatua nyingine, akizungumza kupitia kipindi cha ‘Tuambie’ kilichorushwa na Televisheni ya Taifa (TvT), juzi usiku, Odinga alitaka kuundwa kwa serikali ya mpito ya miezi mitatu kama masharti mapya ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa uchaguzi ambao Rais Kibaki ametangazwa mshindi na kusababisha mauaji na vurugu kubwa nchini humo.
Akizungumza moja kwa moja kwa njia ya simu kutoka Kenya, Odinga alisisitiza ni lazima Rais Kibaki aachie madaraka na kisha iundwe serikali ya mpito itakayokaa madarakani kwa kipindi cha miezi mitatu kutayarisha uchaguzi mpya wa urais.
Alisema uchaguzi utakaorudiwa ni wa urais tu na wabunge waliochaguliwa wataendelea na kazi zao kwa sababu matokeo yao hayana dosari tofauti na ya urais ambayo yamevurugwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK).
Odinga alisema hayo ni masharti yatakayowekwa mezani iwapo Kibaki atakubali kushiriki mazungumzo ya amani ya kutafuta suluhu ya mtafaruku wa kisiasa nchini humo ambao hadi sasa inakisiwa kwamba zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha na wengine 100,000 kukosa makazi kutokana na ama nyumba zao kuchomwa moto au kuyakimbia mapigano katika sehemu mbalimbali nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, Odinga alisema kwamba Kibaki anastahili kubeba lawama za mauaji na vurugu zinazoendelea kwa sababu amebariki wizi wa kura uliofanywa na ECK.
Alisema kwamba amewasiliana na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na wa Uganda, Yoweri Museveni juu ya hali ya vurugu za Kenya ambazo zimesababishwa na wizi wa kura na kuwataka marais hao wawasiliane na Kibaki juu ya wizi huo na akubali kwamba hakushinda kwa halali.
Odinga alisema kwamba wote waliahidi kuwasiliana na Kibaki na kwamba baadaye wangempa ujumbe wa Kibaki, hata hivyo Museveni alimpigia simu na kumweleza kwamba Kibaki amesema hana sababu yoyote ya kufanya mazungumzo hadi hapo nchi itakapotulia.
Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, amezungumza na Odinga na kupendekeza kwake majina ya watu watatu ambao wanaweza kutumika kama wasuluhishi wa kimataifa.
Mmoja wa viongozi wa ODM, William Ruto aliwataja watu waliopendekezwa na Brown kuwa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Ghana, John Kufour, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Koffi Annan na msimamizi mkuu wa Jumuiya ya Madola, Tejan Kabba.
Ruto alisema kati ya watu hao, ODM inapendelea Annan kuwa kiongozi wa timu ya usuluhishi.
Alisema Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, naye alizungumza na Odinga na kukubaliana kuwa Kufour afike Alhamisi kwa ajili ya kazi ya usuluhishi, lakini serikali ilikataa kiongozi huyo kuingia nchini Kenya.
Aliwataja viongozi wengine ambao walizungumza na Odinga kuwa ni Rais wa Djibouti, Ismail Omar Guelleh, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, Rais wa DRC, Laurent Kabila na Muammar Gaddafi wa Lybia.
Pia alisema kuwa Mwenyekiti wa ECK, Samuel Kivuitu, naye alizungumza na Odinga na kukubali kutoa ushahidi kuonyesha kuwa kura ziliibwa katika uchaguzi.