VURUGU huenda zikatokea leo jijini Dar es Salaam, iwapo wanasiasa wa vyama vya upinzani wataamua kupuuza amri ya polisi na kuandamana ili kupinga mauaji yanayoendelea nchini Kenya.
Iwapo busara haitatumika na hilo likatokea, kuna uwezekano mkubwa Jeshi la Polisi likatumia nguvu kukabiliana na waandamanaji hao katika kile kinachoweza kuwa na sura ya kinachotokea katika Jiji la Nairobi nchini Kenya, hivi sasa.
Kwa muda wa siku kadhaa zilizopita, polisi wa Nairobi wamekuwa wakipambana na waandamanaji, wafuasi wa chama cha Orange Democratic Movemant (ODM), wanaotaka kuandamana kupinga ushindi wa Rais Mwai Kibaki alioupata katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo, Desemba 27 mwaka jana.
Mabishano kuhusu uchaguzi huo, yaliyoibuka baada ya mgombea wa ODM, Raila Odinga kudai kuwa ameibiwa kura, yamesababisha vurugu na mauaji ya mamia ya watu.
Hali hiyo imewapa sababu wanasiasa wa upinzani nchini kuandaa maandamano, kulaani mauaji hayo, lakini Jeshi la Polisi jana ilitangaza kuyapiga marufuku.
Hata hivyo, licha ya Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kuyapiga marufuku maandamano hayo, vyama hivyo vimeapa kuandamana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, alisema jeshi lake limeamua kupiga marufuku maandamano hayo kwa sababu hali ya usalama wa nchi hivi sasa si shwari.
“Kwa sasa hali nchini Kenya ni ya vurugu na kutokana na vurugu hizo, Wakenya wengi wanakimbilia hapa nchini kupitia mipaka yote, ikiwemo viwanja vya ndege, vituo vya mabasi na baharini… kutokana na hali hii, hali ya usalama katika nchi yetu si salama,” alisema Tibaigana.
Alisema, juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, alipokea barua kutoka kwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akimtaarifu kufanya maandamano leo yatakayoshirikisha chama hicho, CUF, TLP na NCCR-Mageuzi.
Tibaigana alisema, baada ya kupokea barua hiyo jana asubuhi aliwaita wawakilishi wa vyama hivyo, ili kuzungumzia suala hilo na katika mkutano huo, walikubaliana kuwa Tanzania kama jirani, inapaswa kuchukua hatua za kusaidia kumaliza vurugu nchini Kenya kwa usalama.
Alisema kuwa aliwaeleza kuwa makundi ya Wakenya wanaokimbilia Tanzania si lazima wawe upande mmoja wa mgogoro na kwa maana hiyo, maandamano yanayounga mkono upande mmoja yana uwezekano mkubwa kukasirisha kikundi kimoja, hivyo kuvamia maandamano hayo na kuleta rabsha.
“Kama tumemwomba rais wetu asuluhuhishe mgogoro huku tunaandamana dhidi ya upande mmoja wa mgogoro, nadhani tutakuwa tunachochea mgogoro huo badala ya kuusuluhisha,” alisema.
Kuhusu suala la kuandamana kwenda ubalozi wa Kenya, alisema ubalozi huo ni wa Kenya na si wa Tanzania, hivyo polisi kuruhusu maandamano kwenda ubalozi wa nchi yoyote ile bila ridhaa na maelekezo ya ubalozi huo, ni kukiuka sheria za kimataifa.
Pamoja na mambo mengine yaliyojitokeza kwenye kikao hicho, alisema wawakilishi hao hawakuweza kufikia muafaka na hawakuona umuhimu wa suala la usalama wa nchi, na kwamba maandamano yao kwa sasa yangeweza kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.
“Baada ya kujadiliana nao takribani saa tatu na baada ya kuwashauri kuwa hali ya nchi si salama kwa sasa, na kwamba askari wote tuko katika tahadhari kutokana na wimbi la watu wanaoingia kutoka Kenya, wenzetu walishindwa kutuelewa, na walisisitiza lazima wafanye maandamano hayo na lazima waende Ubalozi wa Kenya.
“Wajumbe wa vyama niliofanya nao kikao wamesema wataandamana licha ya maandamano na mkutano kuzuiliwa… nadhani hiyo inaonyesha dhahiri kwamba nia yao si nzuri na wamedhamiria kuanzisha vurugu ili nao waonekane wanaonewa,” alisema Kamishna Tibaigana.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kususuia maandamano hayo, kwani si ya amani, kwamba hayana tija wala faida na kuongeza kuwa jeshi hilo litahakikisha hayafanyiki na ni vema wananchi wakaelewa hivyo, ili wasije kulalamika baadaye.
“Ili tusije kulaumiana, ni vema wakazi wa Dar es Salaam wasusie maandamano hayo ambayo tumeyakataza kwa sababu za kiusalama,” alisisitiza.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa ushirikiano huo wa vyama vya siasa, Chacha Wangwe (CHADEMA), alisema maandamano hayo yapo kama walivyoyapanga kwa kuwa sababu zilizotolewa na Kamishna Tibaigana ni za kisisa zaidi.
“Huyu Tibaigana anapenda sana mambo ya siasa, sasa kama anataka uwanja mpana zaidi aache kazi ya upolisi, ili aje kwenye ulingo wa siasa, lakini si kama anavyofanya sasa,” alisema Wangwe.
Alisema vitisho kama hivyo vimepitwa na wakati na kilichobaki hivi sasa ni kila mtu kuheshimu haki za mwingine bila kujali cheo, sura au kabila lake.
Wangwe alisema maandamano kama hayo leo yanatarajia kufanyika katika nchi za Australia, Marekani na Afrika Kusini, hivyo ni vema Tibaigana akawapa ulinzi badala ya kuwazuia.
Vyama vya upinzani juzi viliwasilisha barua kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam vikitaarifu nia ya kufanya maandamano ya kupinga matokeo ya kura za urais nchini Kenya. Wamepanga kukusanyika eneo la Urafiki, Ubungo na kutembea kupitia Manzese na kuishia kwenye ubalozi wa Kenya hapa nchini.
Katika hatua nyingine, serikali imekubali kuiuzia mafuta nchi ya Uganda kutokana na kukumbwa na uhaba wa bidhaa hiyo.
Uamuzi huo wa serikali umetokana na ombi la Uganda kwa Tanzania, ikiomba iruhusiwe kununua mafuta nchini baada ya kushindwa kupata huduma hiyo kupitia nchini Kenya kutokana na kufungwa kwa bandari ya Mombasa kutokana na vurugu nchini humo.
Taarifa ambazo Tanzania Daima imezipata jana toka Wizara ya Nishati na Madini na kufafanuliwa na Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Invocavit Swai, zilieleza kuwa serikali ilipokea ombi kutoka Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini ya Uganda mapema wiki hii, kutaka iuziwe mafuta kutoka Tanzania baada ya kule ambako imekuwa ikichukua siku zote kukumbwa na machafuko.
“Tumewaambia Uganda watueleze ni kiasi gani wanahitaji na kwa muda gani, ili tuone jinsi ya kuwasaidia. Kwa sasa tuko tayari kusaidia kwa kipindi cha muda mfupi,” alisema Swai.
Aidha, alisema kuwa hivi sasa tayari kuna mfanyabiashara anayepakia mafuta kiasi cha lita 450,000 kupeleka Uganda.
Kuhusu bei, alisema Tanzania iliweka soko huria la mafuta kuanzia mwaka 2000, hivyo suala la bei litapangwa na wafanyabiashara wenyewe.
Katika hilo, alisema serikali itahakikisha kwamba wanafuata sheria zote, ikiwemo kutumia magari yanayokubalika kisheria, mafuta yawe na ubora unaokubalika kisheria na walipie kodi zote zinazostahili.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo Tanzania yenyewe inajitosheleza kwa mafuta mpaka kufikia hatua ya kuuza nje, Kaimu Katibu Mkuu huyo alijibu suala hilo ni muhimu na serikali inalipa kipaumbele.
“Leo hii mchana kuna mkutano wa EWURA na wadau wa nishati ya mafuta kuangalia ni kiasi gani cha mafuta tulichonacho na kiasi gani kipo njiani,” alisema.
Swai alisema serikali itahakikisha kwamba ni ziada tu ndiyo inapelekwa, na kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha mtaji wa Tanzania hauathiriwi na pia kuhakikisha soko la ndani linatoshelezwa kwanza.
Katika hatua nyingine, muungano wa vyama vitano vya kizalendo (PFA), vimedai kuwa iwapo hakutaundwa Tume Huru ya Uchaguzi haraka, mwaka 2010 yatatokea kama yanayotokea Kenya sasa.
Mwenyekiti wa vyama hivyo, Emmanuel Makaidi, alisema wakiwa kama vyama vya kisiasa vya upinzani, wamejifunza jambo muhimu kutokana na uchaguzi mkuu wa Kenya uliofanyika hivi karibuni.
“Kuna kitu tumejifunza katika uchaguzi wa Kenya, ila sisi tunachotaka ni kuwe huru kabla ya uchaguzi, ili kuepuka kuibiwa kura zetu na huu ujanja ujanja wa Kiafrika,” alisema.
Aidha, wanachama wa mtandao wa mashirika ya haki za binadamu kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (SAHRINGON), wamewasilisha barua ya wito wa haraka wa kukomesha uvunjaji wa haki za binadamu unaoendelea nchini Kenya kwa Balozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Mwenyekiti wa mtandao huo, Hellen Kijo-Bisimba, alisema upelekwaji wa majeshi katika maeneo kadhaa ni wa kutisha na unatia shaka, na kudai kuwa kutokana na nguvu zinazozidi kutumika dhidi ya waandamanaji, watu wanaopinga matokeo hayo wameamua kuchukua sheria mikononi na wameingia katika vitendo viovu dhidi ya raia wenzao.
Taarifa hii imeandaliwa na Salehe Mohamed, Dauson Harold, Amana Nyembo, Ratifa Baranyikwa na Safina Tibanyindera.