Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Mwinyi akemea rushwa vyombo vya habari
http://www.habaritanzania.com/articles/4269/1/-Mwinyi-akemea-rushwa-vyombo-vya-habari
By Habari Tanzania
Published on 12/22/2007
 
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, amekemea rushwa kwenye vyombo vya habari, na kuwataka wanahabari wote kuungana na kupinga rushwa kwa nguvu zote.

RAIS mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, amekemea rushwa kwenye vyombo vya habari, na kuwataka wanahabari wote kuungana na kupinga rushwa kwa nguvu zote.

Rais Mwinyi aliyasema hayo jana katika sherehe za maadhimisho ya kutimiza mwaka mmoja kwa gazeti la kiswahili la serikali la Habari Leo.

Mwinyi alisema anatoa kauli hiyo kwa masikitiko makubwa, kwani ana taarifa kwamba rushwa imekithiri ndani ya vyombo vya habari, hali inayosabababisha mmomonyoko wa maadili ndani na nje ya fani hiyo.

“Nasikia siku hizi ukitaka kumchafua mbaya wako au ukitaka ufisadi wako usiandikwe unatoa bahasha kwenye vyombo vya habari na kisha mabaya yako yanazimwa na pia unafanikiwa kumchafua mbaya wako,” alisema Mwinyi huku akionyesha kukerwa na tabia hiyo.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo zinaongoza kuwa na magazeti mengi na majarida, lakini hivi sasa inaongoza kwa kutofuata maadili.

“Siyo waandishi wa gazeti la Habari Leo peke yao, ni waandishi wengi wana tabia hiyo inayosababisha mmomonyoko wa maadili hivyo siyo sifa nzuri ni hila,” alisema Mwinyi.

Alilalamikia pia viwango vidogo vya elimu miongoni mwa waandishi wa habari na kusema kuwa vinasababisha kuwepo kwa waandishi wababaishaji ambao wamepewa jina la ‘makanjanja’.

“Nashauri wamiliki wa vyombo vya habari wawe wanaandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa ajili ya kuwanoa waandishi wao ili kuweza kutokomeza mmomonyoko wa maadili ambao umekuwa ukifanywa na baadhi ya waandishi wa habari,” alishauri.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Seif Khatib, alisema serikali haina mpango wa kulitumia gazeti hilo kwa maslahi yake binafsi na badala yake gazeti hilo litaendelea kutumika kwa maslahi ya umma.