Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »   Zanzibar wagomea mishahara
Zanzibar wagomea mishahara
By Habari Tanzania | Published  12/22/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
BAADHI ya wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) wamegoma kupokea mishahara yao katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Idd el Hajj kwa kile walichokiita kupunjwa mishahara yao na kuahidi kuwa wataendelea kuigomea hadi hapo marekebisho yatakapofanywa.

Watumishi wa taasisi mbalimbali wametoa malalamiko hayo, wakiwemo madaktari na wauguzi.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa sharti la kutotajwa majina yao, baadhi ya wafanyakazi wa taasisi za umma waliapa kutopokea mshahara wa mwezi Desemba hadi tatizo hilo litakaposhughulikiwa na Wizara ya Fedha na Uchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Zanzibar, Sultan Mohammed Mugheiry, alisema kuwa serikali inafahamu vyema tatizo la wafanyakazi wake na akaahidi kuwa suala hilo litashughulikiwa na kuwaomba wafanyakazi kuvuta subira.

Hata hivyo, Waziri Mugheiry hakupenda kulizungumzia suala hilo na kusisitiza kuwa serikali inalitafutia ufumbuzi ambao utapatikana katika kipindi kifupi kijacho.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi wa Huduma za Umma (ZAPSU), Talib Mbwana, aliitahadharisha SMZ kuhusu toleo la serikali la mishahara mipya, akisema halikuambatanishwa na muongozo wa utelekezaji wake.

“Sisi tunaitanabahisha serikali isiporekebisha viwango vya mishahara, kuna hatari kubwa ya kukimbiwa na wafanyakazi wake, hasa madaktari na walimu, hivyo basi ushauri wetu kwao ni kukaa pamoja na Bodi ya Ushauri ya Mishahara kuzungumzia suala hilo,” alisema.

Alisema katika toleo jipya la mishahara, hapakuwa na muongozo unaoonyesha wafanyakazi wa awali walikuwa wakipokea mshahara gani na ngazi yao na kwa hivyo katika utaratibu mpya watapata mshahara gani katika ngazi ipi.

Shirikisho hilo limesema kwamba kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wafanyakazi kuhusu suala la mishahara, ambako wengine wamepunjwa na wengine kuongezewa kiasi cha fedha, jambo ambalo limewavunja moyo wafanyakazi wengi.

“Tunaomba kuitanabahisha serikali kuwa sokomoko hili limeleta mtafaruku kwa wafanyakazi wa serikali waathirika wa zoezi hili kiasi kwamba kazi hazifanywi kwa ufanisi na tija, kazi kwa ujumla zimezorota katika sehemu zote za kazi tangu utekelezaji wa mishahara mipya ulipoanza,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Alisema kwamba mpango wa serikali wa kutokuwa na nyongeza za mishahara za moja kwa moja kama ilivyokuwa zamani, linaweza kuwa tatizo kwani sasa mfanyakazi atapandishwa daraja la mshahara kwa kupimwa utendaji wake wa kazi.

Kupitia bajeti yake ya mwaka huu wa fedha, SMZ iliongeza kiwango cha mishahara na kufanya kima cha chini kuongezeka kutoka sh 50,000 kwa mwezi hadi sh 60,000.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.