MADAKTARI sita na wauguzi sita wa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), wamepatikana na makosa ya uzembe yaliyosababisha kufanyika kwa upasuaji tata wa wagonjwa wawili katika taasisi hiyo, hivi karibuni.
Hayo yalitangazwa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa, wakati akitangaza hadharani, ripoti ya uchunguzi wa upasuaji huo, uliozusha gumzo nchini.
Waziri Mwakyusa alisema kuwa kamati aliyoiunda kuchunguza upasuaji huo, imebaini kuwa, matatizo hayo ya uzembe yaliwahusu madaktari bingwa wawili, madaktari wasaidizi watatu na daktari wa usingizi.
Wengine ni wauguzi wa dawa ya usingizi wawili, wauguzi wa upasuaji wawili na wauguzi wa wodini wawili, ambao wote kwa pamoja hawakufanya kazi yao kwa umakini.
Waziri Mwakyusa alisema, hali hiyo imechangiwa na mahusiano duni kati ya mgonjwa, muuguzi na daktari kwa kuwachanganya wagonjwa Emmanuel Didas (20) na Emmanuel Mgaya (19) ambaye sasa ni marehemu, kwa kuwa ugonjwa haukuhusishwa na mgonjwa mwenye ugonjwa, bali waliridhika kwa kuangalia majibu ya vipimo pekee.
Hivyo, ameiagiza Bodi ya Wadhamini ya MOI, ichukue hatua kali za kinidhamu kwa wale wote waliozembea katika kuwahudumia wagonjwa hao, na iendelee kuchukua hatua kwa wengine wote watakaofanya hivyo baada ya tukio hilo, pamoja na kusimamia kwa karibu utawala wa MOI na kuimarisha utendaji wake.
Pia ameitaka bodi hiyo kuisimamia menejimenti, ili iwafikishe mara moja kwenye Baraza la Madaktari, madaktari wanne waliosimamishwa kazi kutokana na taarifa ya tume ya kwanza, pamoja na wengine wanne ambao tume yake imewakuta kuwa wana masuala ya kujibu, ambao ni wasaidizi wa madaktari bingwa na dawa za usingizi.
“Aidha, menejimenti iwafikishe wauguzi wanne ambao hawakuwa makini katika kutekeleza majukumu yao ya kitaalamu kwenye Baraza la Wauguzi na Wakunga kwa hatua hizo hizo,” aliagiza Waziri Mwakyusa.
Katika sakata hilo, Didas alifanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu wa kushoto na marehemu Mgaya alifanyiwa upasuaji wa mguu wa kushoto badala ya kichwa, kabla ya kuja kupasuliwa kichwa kilichokuwa na matatizo na siku chache baadaye akapoteza maisha.
Mwakyusa alisema uchunguzi umebaini kuwepo kwa udhaifu katika kusimamia taratibu zilizopo zinazohusiana na upasuaji na huduma za wagonjwa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mwakyusa, upasuaji tata huo ulichangiwa na kutokufuata maelekezo ya madaktari waandamizi, hali iliyosababisha orodha ya wagonjwa wa kupasuliwa kuwa tofauti na maelekezo ya jopo la madaktari bingwa.
Pia hali hiyo ilisababishwa na kutokufuata utaratibu wa idhini ya mgonjwa, pamoja na maandalizi hafifu ya wagonjwa kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Waziri Mwakyusa alisema ripoti hiyo haikusita kuweka bayana eneo la utawala kuwa na udhaifu wa usimamizi wa kazi katika baadhi ya vitengo vya idara, hususan vile vinavyoshughulika na matibabu ya wagonjwa, mawodini na katika vyumba vya upasuaji.
“Kamati ilibaini kuwa kuna udhaifu katika kusimamia taratibu za kuwaandaa wagonjwa wa upasuaji na wakati wa hatua za awali kabla ya upasuaji,” alisema Profesa Mwakyusa.
Ripoti inabainisha kuwepo kwa usimamizi dhaifu katika baadhi ya vitengo vya MOI, ambao umedhihirika zaidi katika idara za upasuaji mifupa, upasuaji mishipa ya fahamu na ubongo, utoaji dawa za usingizi, vyumba vya upasuaji na uuguzi.
Profesa Mwakyusa alisema kuwa pia katika mfumo wa utendaji, kuna kasoro kubwa katika maeneo ya wodini kabla ya upasuaji, ukaguzi kabla ya kupata dawa za usingizi, utayarishaji orodha ya upasuaji, uuguzi katika wodi na chumba cha upasuaji.
Aliyataja maeneo mengine ambako udhaifu umebainika kuwa ni sehemu ya dawa za usingizi katika chumba cha upasuaji, sehemu ya wagonjwa kusubiri kabla na baada ya upasuaji, chumba cha upasuaji chenyewe na sehemu ya dawa za usingizi pamoja na wodini baada ya upasuaji.
Mwakyusa alisema kuwa pamoja na maagizo mengine, pia ameiagiza Bodi ya Wadhamini ya MOI kuisimamia menejimenti katika kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Profesa William Mahalu, ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji kutoka Hospitali ya Bugando, na kumpatia taarifa ya utekelezaji ndani ya wiki mbili kuanzia jana.
Profesa Mahalu ndiye aliongoza tume iliyoundwa na Bodi ya MOI awali.
Pia aliiagiza bodi hiyo imwagize Mkurugenzi Mkuu wa MOI, Profesa Lawrence Museru, wakurugenzi wakuu wa vitengo kusimamia utendaji kazi ipasavyo na kuwasilisha taratibu mpya zitakazoimarisha usimamizi wa idara zote.
Pia aliitaka bodi hiyo kuhakikisha kuwa inapitia upya mgawanyo wa kazi wa idara na vitengo na kuongeza wigo wa madaktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na ubongo.
“Kwa jinsi hiyo, ni vyema kila ‘firm’ (kitengo) iwe na madaktari bingwa wawili, badala ya wanne kama ilivyo sasa, ili kuongeza uwajibikaji,” alisema Mwakyusa.
Aliitaka bodi hiyo iiagize menejimenti kuimarisha uongozi wa vitengo ambavyo vimeonekana kuwa na udhaifu wa uongozi na usimamizi, hususan kitengo cha uuguzi, dawa za usingizi, chumba cha upasuaji na huduma nyingine za wagonjwa.
“Kwa mfano uongozi wa firm A umeonyesha udhaifu mkubwa katika utendaji, hivyo ubadilishwe,” alisema Mwakyusa.
Alisema tukio hilo ni fundisho katika utoaji wa huduma za afya nchini, hivyo amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wilson Mukama, atoe mwongozo utakaoimarisha utoaji wa huduma za afya nchini kwa kuzingatia vigezo vinavyokubalika katika upasuaji na huduma nyingine za afya na waraka huo usambazwe katika hospitali zote nchini.
“Naagiza mabaraza ya kitaaluma, kupitia na kusimamia kwa makini na kwa karibu zaidi miongozo ya kitaaluma, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kwa wale wote watakaokiuka maadili ya taaluma zao,” alisema.