Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »   Balali akamatwe - Slaa
Balali akamatwe - Slaa
By Habari Tanzania | Published  12/22/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Salehe MohamedKATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuamuru kukamatwa na kushtakiwa kwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daudi Balali.

Dk. Slaa ametoa kauli hiyo jana siku moja tu baada ya kuwepo kwa taarifa ambazo hazijathibitika kuwa gavana huyo, ambaye yupo Marekani kwa matibabu, ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo, akitaja maradhi yanayomsumbua kama sababu kubwa ya kufikia uamuzi huo.

Akizungumzia taarifa za kujiuzulu kwa Dk. Balali, Dk. Slaa kwanza alimpa pole kutokana na maradhi yanayomkabili, lakini akamtaka Rais Kikwete kuamuru kukamatwa kwa gavana huyo mara moja ili ajibu tuhuma zote zinazomkabili.

Akiandika ujumbe mrefu wa simu ya mkononi, Dk. Slaa aliorodhesha baadhi ya tuhuma ambazo Dk. Balali anatakiwa kuzijibu kuwa ni kughushi taarifa ya BoT ya 2005 aliyowasilisha kwa Waziri wa Fedha, Zakia Meghji Septemba 20, 2005 katika kitabu ambacho ndani yake taarifa ya fedha ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imesainiwa Juni 21, 2007.

“Isitoshe yeye mwenyewe amesaini kama Mwenyekiti wa BoT Juni 21, 2007. Balali pia amesaini balance sheet (mizania) ndani ya kitabu hicho hicho. Taarifa zinazohusika ni hizo hizo za 2005/2006 zenye migogoro. Ni dhahiri kuna kughushi.

“Meghji kakaa kimya. Kughushi au ku-back-date (kurudisha nyuma tarehe) ni kosa la jinai. Kuna kirusi gani nchini? Raia wa kawaida hata angeumwa saa hizi angekuwa analindwa na askari magereza hospitalini… hakuna mwenye kibali kuvunja sheria,” alisema.

Alizitaja tuhuma nyingine kuwa ni matumizi yenye kutia shaka katika malipo ya akaunti ya nje (EPA), fedha zilizolipwa KAGODA Co bila maelezo, fedha zilizopelekwa Deep Green na zile za Tangold Ltd.Aidha, alimtaka Rais Kikwete kumchukulia hatua za kisheria na ikiwezekana kumfikisha mahakamani Balali akimtuhumu kufuja fedha za wavuja jasho, ambao kila kukicha maisha yao yanazidi kudidimia kwa sababu ya watu wachache wanaotumia rasilimali za nchi kwa maslahi binafsi.

“Serikali inaogopa nini kumchukulia hatua mtu anayefuja mabilioni ili hali mjamzito anajifungulia bila huruma ofisi ya WEO kwa ajili ya kukosa sh 20,000?” alihoji Dk. Slaa. Hata hivyo, madai hayo ya Slaa yalipata kukanushwa wakati fulani na Balali wakati alipoitisha mkutano nadra na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya watu kadhaa kumhusisha na tuhuma za ubadhirifu wa BoT alizozielezea kuwa zisizo na msingi.

Wakati Slaa akitoa madai hayo, ripoti ya uchunguzi wa ubadhirifu wa fedha BoT uliofanywa na kampuni ya ukaguzi wa mahesanu ya Ernst & Young kwa maagizo ya ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), itawekwa hadharani wiki ijayo.Hayo yalithibitishwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri Meghji, aliyewaambia waandishi wa habari kuwa ripoti hiyo ndiyo kwa kiasi kikubwa itakayoisaidia serikali kushughulikia kile kitakachoonekana kina tatizo.

Akifafanua, Meghji alisema kuwa, ushughulikiaji huo wa matatizo yatakayoainishwa katika ripoti hiyo, kutahusisha pia kuwachukulia hatua stahili, wale wote watakaobainika kufanya makosa, kulingana na taratibu za kazi na sheria za nchi.Alisema hivi sasa ni vigumu kuanza kuzungumzia suala la ubadhirifu wa fedha au kumnyooshea mtu kidole, hadi hapo ripoti hiyo itakapokamilika, hivyo ni vema kwa wakati huu jamii ikaendelea kuvuta subira.

“Тuvute subira jamani kwani ripoti itatolewa ‘next week’ (wiki ijayo) na ndipo hapo tutaangalia cha kufanya kwa yale yatakayobainika na kuwachukulia hatua wale wote watakatajwa na ripoti hiyo,” alisema Meghji.Serikali iliiagiza CAG kuyafanyia uchunguzi madai ya viongozi wa upinzani kuwapo kwa matumizi mabaya (ufisadi) ya fedha za wavuja jasho katika BoT.Viongozi hao wa upinzani wakiongozwa na Dk. Slaa, ndio walioibua sakata hilo bungeni na kudai kufanyika kwa uchunguzi kuhusiana na matumizi ya fedha yenye kutia shaka ndani ya BoT.

Awali, madai hayo ya wapinzani yalipingwa vikali na serikali, lakini baadaye, ilibainika kuwepo kwa kasoro katika akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) na ndipo serikali ilipoiagiza ofisi ya CAG kufanya ukaguzi huo.

Meghji anatoa kauli hiyo siku chache tu baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe kuhoji sababu za serikali kuikalia ripoti hiyo kwa muda mrefu hata baada ya kazi kukamilika.Kwa upande wake, Dk. Slaa bado anaendelea kudai kuwa, ukaguzi huo umefanywa katika sehemu ndogo sana kwani ubadhirifu ndani ya BoT unahusisha vitengo vingi zaidi ya EPA.

Katika hatua nyingine, Meghji, alisema mpaka sasa ofisi yake haijapata taarifa ya kujiuzulu kwa Dk. Balali na kusema kuwa taarifa hizo alizisoma kwenye magazeti jana.

Alisema anachokijua ni kuumwa kwa Dk. Balali na yupo nchini Marekani akipatiwa matatibu ya maradhi yake na si kujiuzulu wadhifa wake kama ilivyoripotiwa kwenye magazeti kadhaa ya hapa nchini.“Mimi sijapata barua ya Balali kujiuzulu na kama amefanya hivyo, anapaswa kuandika barua na mara tutakapoipata tutaueleza umma kuhusiana na uamuzi huo,” alisema Meghji.Kujiuzulu kwa Dk. Balali bado ni kitendawili kikubwa kutokana na kauli ya Waziri Meghji pamoja na ile iliyotolewa na Rais Kikwete majuzi wakati alipozungumza na wahariri kuwa, anachofahamu ni kuwa gavana huyo yupo katika matibabu.

Hata Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alipoulizwa juzi, naye alishindwa kukubali au kukanusha iwapo Dk. Balali ameandika barua hiyo ya kujiuzulu.

Kwa muda wa miezi kadhaa sasa, Dk. Balali yupo nchini Marekani, inakoelezwa kuwa amelazwa katika hospitali moja baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa.

Huku nyuma, ameacha wingu zito la tuhuma dhidi yake na taasisi anayoiongoza, kutokana na matumizi yenye kutia shaka ya fedha, hasa zile zilizotumika katika malipo kwa kampuni kadhaa na ujenzi wa majengo mapya ya BoT.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.