Wakati sakata la tuhuma za ufisadi katika Benki Kuu nchini, BOT, likiendelea kuzizima, zimepatikana habari kuwa Gavana wa benki hiyo ameandika barua kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Jakaya Kikwete, akiomba kujiuzulu.
Taarifa hizo, ambazo zimeelezwa na chanzo chetu ndani ya Serikali, zinasema kwamba Gavana Balali, ambaye kwa miezi zaidi ya mitatu sasa amekuwa akiendelea na matibabu nchini Marekani, ameandika barua ya kuomba kuachia ngazi kutokana na sababu za kiafya.
``Amemuandikia barua Rais akiomba kujiuzulu kutokana na hali ya afya yake... sifahamu zaidi ya hilo,`` chanzo chetu hicho kimesema.
Aidha, imedaiwa kuwa Gavana Ballali ameandika barua hiyo ya kuomba kujiuzulu siku ya Jumatano.
Hata hivyo, juzi wakati wa mazungumzo yake na waandishi wa habari, Rais Kikwete aliulizwa swali kuhusu madai kwamba Gavana Ballali amekimbia nchi.
Katika majibu yake, Rais Kikwete alisema anachojua yeye ni kwamba Bw. Ballali ni mgonjwa na yuko nchini Marekani kwa matibabu.
Jana, mwandishi wa Alasiri alipomuuliza Waziri wa Fedha Bi. Zakia Meghji kuhusiana na habari hizo za Gavana kuomba kujiuzulu, alikataa kuzithibitisha, akikwepa kukiri wala kuzikanusha.
``Siwezi kukuambia kuwa Balali kajiuzulu ama hajajiuzulu, niliondoka ofisini saa nane Jumatano, lakini hapakuwa na taarifa yoyote,`` akasema.
Kwa miezi kadhaa sasa, wapinzani wamekuwa wakimshutumu Gavana Ballali kuhusika na kile wanachodai kuwa ni ufisadi ndani ya taasisi hiyo nyeti katika uchumi wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuidhinisha malipo yenye utata kwa makampuni kadhaa na pia gharama kubwa za ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo Jijini na Zanzibar.