Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Kufaulu kwa shuka - matokeo darasa la saba
http://www.habaritanzania.com/articles/4261/1/-Kufaulu-kwa-shuka---matokeo-darasa-la-saba
By Habari Tanzania
Published on 12/19/2007
 

KIWANGO cha kufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kimeshuka kwa asilimia 16.3 mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana, ambapo waliofaulu walikuwa asilimia 70.48 ya wanafunzi wote waliofanya mitihani.

KIWANGO cha kufaulu kwa wanafunzi wa darasa la saba kimeshuka kwa asilimia 16.3 mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana, ambapo waliofaulu walikuwa asilimia 70.48 ya wanafunzi wote waliofanya mitihani.

Akitangaza matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kuhitimu elimu ya msingi, Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi, Margaret Sitta, alisema jumla ya wanafunzi 419,198 wamefaulu mwaka huu ambao ni sawa na asilimia 54.18.

Akifafanua mbele ya waandishi wa habari jana, Waziri Sitta alisema idadi hiyo ni ndogo ukilinganisha na idadi ya waliofaulu mwaka jana ambapo waliofaulu walikuwa 468,187.

Alisema mwaka huu kulikuwa na jumla ya watahiniwa 773,550 ambao ni asilimia 97.41 ya wote waliotarajiwa kufanya mitihani hiyo, kati yao wavulana wakiwa 248,354 ambao ni asilimia 62.52 na wasichana 170,844 sawa na silimia 45.39.

Mwaka 2006, idadi ya wanafunzi wa darasa la saba waliofanya mtihani walikuwa 667,294, ambao ni asilimia 97.2 ya wote waliotarajiwa kufanya mitihani hiyo.

“Jumla ya wasichana 170, 844 wamefaulu, ambao ni asilimia 45.39 ya wasichana waliofanya mitihani na wavulana 248,354, sawa na asilimia 62.52 ya wavulana wote ambao walifanya mtihani huo,” alisema.

Waziri Sitta alisema jumla ya watahiniwa 354,405 hawakufaulu na kati yao wasichana ni 205, 618, sawa na asilimia 54.61 na wavulana 148,787, sawa na asilimia 37.48 ya watahiniwa waliopewa matokeo.

Sitta alisema jumla ya wanafunzi 794, 102 wa shule za msingi Tanzania Bara waliandikishwa kufanya mitihani hiyo, wasichana wakiwa 385,614, sawa na asilimia 48.6 ya watahiniwa wote na wavulana 408,488, sawa na asilimia 51.4.

Alisema ikilinganishwa na walioandikishwa kufanya mitihani hiyo mwaka 2006, idadi ya walioandkishwa mwaka huu inaonyesha ongezeko la watahiniwa 107,910, ambao ni sawa na asilimia 15.7.

Aliongeza kuwa watahiniwa 209 wa mwaka huu wamesitishiwa matokeo kutokana tuhuma za udanganyifu na wengine 878 wamefutiwa matokeo yao kwa sababu mbali mbali za udanganyifu katika mitihani.

Aidha, alisema matokeo hayo yanaonyesha kiwango cha ufaulu kwa masomo ya Hisabati na Kiingereza si mzuri ukilinganisha na masomo mengine, ambapo asilimia ya waliofaulu kimasomo ni Kiswahili (asilimia 80.23, Sayansi (asilimia 66.66), Maarifa (asilimia 56.39), Kiingereza (asilimia 31.31) na Hisabati (asilimia 17.42).

Waziri alisema kati ya wanafunzi 419,198 waliofaulu mtihani, wanafunzi 378,506, ambao ni asilimia 90.29, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2008. Kati yao wasichana ni 159,543, sawa na asilimia 93.39, na wavulana ni 218,963, sawa na asilimia 88.17.

Pia Sitta alisema jumla ya wanafunzi wenye ulemavu 301 walifanya mitihani hiyo na 212 kati yao wamefaulu, ambao ni sawa na asilimia 70.43 ya wanafunzi waliofanya mitihani hiyo.

Alisema kufuatia kushuka huko kwa kiwango cha ufaulu, wizara itafanya utafiti ili kubaini sababu za kushuka, ili iweze kuchukua hatua stahili za kuongeza ufaulu, na kuwaagiza walimu wakuu, walimu na watendaji wa elimu nchini, kuongeza juhudi na maarifa katika utendaji wao, ili mwakani kiwango cha kufaulu kiongezeke.

Hata hivyo, Sitta aliwahakikishia wananchi kuwa wizara yake itaendelea kuwachukulia hatua kali za kinidhamu na kisheria wale wote ambao watabainika kushiriki katika vitendo vya udanganyifu katika mitihani.

Aliongeza kuwa idadi ya watahiniwa waliofutiwa matokeo mwaka 2007, imepungua kwa watahiniwa 236 ukilinganisha na mwaka jana, ambapo jumla ya watahiniwa 2,677 walisitishiwa matokeo yao kutokana na tuhuma za udanganyifu.

Waziri alitoa wito kwa wadau wa elimu kukamilisha majengo ya shule za sekondari za kata na kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwakani na kuwahimiza wazazi, walezi na jamii kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa wanajiunga na shule na kusoma sambamba na kuendelea kuchangia ujenzi wa shule kwa ajili ya wanafunzi waliobaki.

Hali kadhalika, alisema kuwa serikali ina mpango wa kujenga chuo cha ufundi katika kila wilaya, ili kuwawezesha wahitimu wengi zaidi wa elimu ya msingi kujiunga na kupata stadi za maisha.