Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Siasa  »   CHADEMA yafufua hoja ya mafisadi
CHADEMA yafufua hoja ya mafisadi
By Habari Tanzania | Published  12/19/2007 | Siasa | Rating:
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimehoji ukimya wa serikali kuhusu kuwashughulikia watuhumiwa wa ufisadi walioanikwa hadharani na wapinzani miezi michache iliyopita.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alipofungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Land Mark, Dar es Salaam.

Mbowe alisema chama hicho hakiuelewi ukimya huo wa serikali, kwani kama tuhuma hizo zingekuwa si za kweli wapinzani hao wangekuwa wameshachukuliwa hatua za kisheria.

Mbowe alisema tangu kuibuliwa kwa hoja hiyo ya mafisadi, baadhi ya watuhumiwa walijitokeza hadharani kukanusha madai hayo sambamba na kuahidi kwenda mahakamani kwa kuchafuliwa majina, lakini katika hali ya kushangaza, mpaka sasa hakuna hata mtu mmoja aliyefungua kesi mahakamani.

“Baada ya kutajwa kwa mafisadi, baadhi yao walijitokeza hadharani na kusema tuhuma hizo si za kweli na kuahidi kwenda mahakamani… lakini mpaka sasa hakuna aliyekwenda mahakamani kwa madai ya kuchafuliwa jina wala wapinzani hawajafunguliwa mashitaka, na cha kushangaza zaidi ni ukimya wa serikali kuhusu suala hilo,” alisema Mbowe.

Septemba 15, mwaka huu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Willbrod Slaa, aliwataja viongozi 11, wakiweno mawaziri na maofisa waandamizi wa serikali, aliodai kuwa ni mafisadi waliokula fedha za umma.

Baada ya kutolewa kwa tuhuma hizo, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Patrick Rutabanzibwa, walijitokeza hadharani na kukanusha tuhuma hizo, huku wakiahidi kwenda mahakamani kwa madai ya kuchafuliwa majina.

Wengine waliojitokeza kujibu tuhuma hizo, lakini hawakuonyesha dhamira ya kwenda mahakamani, ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono na Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge.

Aidha, katika hatua nyingine, Mbowe alimtaka Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji kuweka hadharani ripoti ya uchunguzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), uliofanywa na Kampuni ya Ernest & Young.

Akizungumzia tathmini ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Kikwete, Mwenyekiti huyo wa CHADEMA, alisema wananchi wamechoshwa na takwimu za kuridhisha na kauli za matumaini zinazotolewa na kinachohitajika sasa ni vitendo.

Kuhusu kauli ya Waziri Ofisi ya Rais Ikulu, Siasa na Uhusiano wa Jamii, Kingunge Ngombale-Mwiru kuwa mjadala kuhusu katiba umefungwa kwa kuwa hauko katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema fikra hizo ni za ukiritimba.

“Katiba inapaswa kujadiliwa kwa sababu ni mali ya Watanzania wote… mjadala hauwezi kufungwa kwa ilani ya chama kimoja… Kingunge amefanya kazi kwa muda mrefu, anapaswa kupumzika sasa,” alisema Mbowe.

Kuhusu kauli ya Peter Kisumo kuwa CHADEMA ni wezi wa sera ya madini, alipinga kauli hiyo na kusema kuwa sera hiyo ilikuwapo katika ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2005 na kwamba chama hicho ni kisima cha sera.

Aidha, alisema tuzo ya Sulivan aliyotunikiwa Rais Kikwete hivi karibuni ni kiini macho na ina lengo la kumfunga mdomo, kwani watu hao wanajihusisha zaidi na masuala ya uchimbaji madini.

Akijibu tuhuma zilizotolewa jana na Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, kupitia vipeperushi kuwa chama hicho kimegeuzwa kuwa mali ya ukoo wa baadhi ya viongozi wa makao makuu, kwani karibu wabunge wote wa viti maalumu wameteuliwa kutoka mkoa mmoja, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Slaa, alisema wabunge hao wameteuliwa kutokana na uwezo wao katika kujenga hoja na kuzitetea.

“Watu wazungumze kuhusu hili na nipo tayari kulisimamia, kwani bungeni si mahali pa kwenda kupeleka sura, unaangalia uwezo wa mtu katika kujenga hoja, hasa ukizingatia tulikuwa na nafasi chache.

“Wabunge hawa wametupa sifa CHADEMA na ndio jeuri ya CHADEMA. Mtu aje na hoja si maneno light (mepesi),” alisema.

Kuhusu tuhuma kwamba kuna upendeleo katika mgawo wa ruzuku za chama hicho na kwamba ruzuku yote ya milioni 60 kwa mwezi inaishia makao makuu ya chama, alisema wakati wa uchaguzi kunakuwa na maneno mengi, lakini mara nyingi tuhuma zinakwenda na vielelezo.

“Katika kipindi cha miaka miwili, hukuna Mtanzania asiyejua CHADEMA imefanya nini. Tumepeleka bendera na kadi zilizogharimu sh milioni 200 karibu mikoa yote nchini isipokuwa Lindi na Mtwara.

“Mbali na hilo, chama kimekuwa kikifanya ziara katika mikoa mbalimbali nchini sambamba na kupeleka vipeperushi mbalimbali,” alisema Dk. Slaa.

Wangwe ni mmoja wa wagombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho iliyoachwa wazi na Amani Walid Kabourou aliyejiunga na CCM mwaka jana. Mgombea mwingine katika kinyang’anyiro hicho ni Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi.

Uchaguzi huo ulitarajiwa kufanyika jana, lakini kutokana na kuwekwa kuwa ajenda ya mwisho kuna uwezekano kuwa ulifanyika usiku.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.