Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mafuta yashuka bei
Mafuta yashuka bei
By Habari Tanzania | Published  07/2/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Charles Mullinda

HATIMAYE wafanyabiashara wa mafuta ya petroli na dizeli wameufyata na kupunguza bei ya bidhaa hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya awali kutunisha msuli wakidai kuwa wasingeweza kushusha bei ya bidhaa hiyo kutokana na gharama kubwa za kuiagiza nje ya nchi.

Uchunguzi uliofanywa jana na gazeti hili katika vituo mbalimbali vya mafuta jijini Dar es Salaam, umeonyesha kuwa bei hiyo imeshuka kwa sh 45 kwa mafuta ya petroli kwa lita na sh 35 kwa mafuta ya dizeli kwa lita.

Vituo vilivyoshusha bei ni Fire Kariakoo, Oryx kilichopo Posta, Magomeni Filling Station na kile kilichopo katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Mandela, Ubungo.

Bei ya mafuta ya petroli katika vituo hivyo jana ilikuwa sh 1,350 kwa lita ya petroli badala ya sh 1,395 ya awali, na dizeli ilikuwa sh 1,295 kwa lita badala ya sh 1,330 kwa lita.

Wafanyakazi wa vituo hivyo walieleza kuwa, bei hiyo imeanza kutumika jana kutokana na serikali kupunguza ushuru wa mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa. Hasa kubwa likiwa ni kufuta VAT.

Walisema bei hizo mpya zimepangwa na wamiliki wa vituo ambao walikwishatangaza kupunguza bei ya mafuta baada ya kutangazwa kupunguzwa ushuru na kuondoa kabisa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa mafuta ya petroli.

Kituo kimojawapo ambacho hakijashusha bei ya mafuta ni cha BP kinachopakana na Mahakama ya Wilaya ya Ilala. Mmoja wa wafanyakazi wa kituo hicho aliyezungumza na gazeti hili, alisema wanatarajia kushusha bei kuanzia kesho.

Mfanyakazi huyo alisema uongozi wa kituo hicho umeamua kushusha bei kuanzia Jumatatu kwa sababu ndio siku ambayo watu wengi wanakuwa kazini na kununua mafuta.

Alisema kushuka na kupanda kwa bei kwa bidhaa muhimu kama mafuta ambayo ina watumiaji wengi, kunapaswa kufanywa siku za kazi ili mabadiliko yawafikie wengi badala ya siku za sikukuu ambapo wananchi wengine huwa wanakataa kupokea ongezeko lolote wakidhani kuwa wanafanyiwa uhuni kwa vile ni siku za mapumziko.

Bei ya petroli katika kituo hicho ni sh 1,440 kwa lita wakati dizeli inauzwa sh 1,390 kwa lita.

Wakati bei ya petroli na dizeli ikiteremka, nauli ya daladala bado iko pale pale kwa magari yote yanayomalizia safari zake Posta na Feri.

Baadhi ya makondakta waliozungumza na Tanzania Daima jana, walisema kuwa gharama za kuendesha magari yao ni kubwa, hazisababishwi na bei kubwa ya mafuta peke yake.

Walisema ingawa baadhi ya vituo vimepunguza bei ya mafuta, bei itaendelea kuwa ile ile kwa sababu hawajapewa maelekezo ya kupunguza bei na mabosi wao.

Kondakta wa gari namba T 665 ADL linalofanya safari zake kati ya Masaki na Posta, alisema kushuka kwa bei ya mafuta ni danganya toto, kwa sababu bei ya vipuri inazidi kupaa, hivyo haoni haja ya kupunguza nauli.

Baadhi ya magari mengine ambayo makondakta wake walisema hawatateremsha bei kutokana na gharama kubwa za uendeshaji magari ya abiria, ni wenye magari namba T 569 AYY lilinalofanya safari zake kati ya Buruguni na Posta kwa nauli ya sh 200.

Magari mengine ni yenye namba T 336 AGH linalosafirisha abiria Vingunguti - Posta kwa sh 250 na gari namba T 932 AFP linalosafirisha abiria kati ya Tabata na Posta kwa nauli ya sh 300.

Katika bajeti ya serikali iliyotangazwa Juni 15, Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji alitangaza kwamba serikali imepunguza kiwango cha ushuru kwenye mafuta ya taa kutoka sh 122 kwa lita hadi sh 52.

Waziri Meghji alitangaza kwamba nafuu nyingine ya kodi iliyotolewa na serikali ni kufuta VAT kwenye bei ya mafuta ya petroli ili kupungza ongezeko la bei za mafuta, lakini bila kuathiri mapato ya serikali.

Alisema bajeti ya serikali ya mwaka huu imerekebisha viwango vya ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya petroli na sasa itakuwa petroli ya MSP na MSR sh 315 kwa lita, Dizeli (GO) sh 292 kwa lita, mafuta ya taa (IK) sh 52 kwa lita.

Kwa mafuta mazito ya mitambo (HFO) sh 109 kwa lita wakati dizeli ya kuendesha mitambo viwandani (IDO) ni sh 366 kwa lita. Awali bidhaa hizo zilikuwa zikitozwa kodi kupitia utaratibu wa VAT.

Hata hivyo, wananchi waliozungumza na Tanzania Daima wameomba serikali iingilie kati kwa maelezo kuwa walichofanyiwa si uungwana.

Walitoa hoja kwamba gharama ya VAT kwa kodi ya mafuta yote ni asilimia 20 kwa maana kuwa mteja akinunua lita moja sh 1,400, gharama ya VAT inakuwa sh 240, hivyo wakahoji kwa nini ipunguzwe sh 45 pekee.

Wakati wakiomba serikali iingilie kati, wenye kuuza mafuta wanasema ushuru wa barabara umeongezeka na serikali haitaki kusema ukweli kwa kiasi gani inawakaanga wananchi.

Wanasema kuna mchezo katikati wasioujua wananchi, hivyo ni bora serikali itoe kauli rasmi kueleza ni kiasi gani imepunguza na kuongeza kupitia mlango mwingine.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.