Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Marekani yakumbusha Muafaka wa Zanzibar
Marekani yakumbusha Muafaka wa Zanzibar
By Habari Tanzania | Published  12/14/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
UBALOZI wa Marekani nchini, umetaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) kuhitimisha haraka na kwa haki mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

Wito huo ulitolewa jana na Balozi wa Marekani hapa nchini, Mark Green wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jumba la Patterson iliyofanyika visiwani hapa.

Balozi Green alisema Zanzibar ni muhimu kwa wananchi wa Marekani na wana shauku kubwa kuona mchakato huo wa usuluhishi visiwani Zanzibar ukimalizika haraka na kwa amani.

"Watu wanaweza kusema kuwa 2010 bado iko mbali, lakini tuko karibu kuingia 2008 na kufumba na kufumbua, uchaguzi ujao utakuwa umewadia.

"Ni lazima tujikumbushe kuwa mazungumzo ya muafaka kati ya Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi cha CUF yalianza Zanzibar takriban mwaka mmoja uliopita, yaani tarehe 17 Januari 2007," alikumbusha balozi huyo.

Alisema mazungumzo hayo yameendelea kwa muda wa mwaka mmoja sasa na yalipokwama Agosti mwaka huu, pande zote mbili zilikubaliana kuweka juhudi mpya.

"Pamoja na kuwa tumefurahi kuona kwamba mazungumzo yamekwenda mbele, wakati huohuo ningependa kuzitia moyo pande zote mbili kufanya juhudi za dhati kufikia makubaliano ya haki, makubaliano ambayo yataruhusu muda wa kutosha kuyatekeleza," alihimiza.

Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa juhudi zake za dhati kuhakikisha kuwa majadiliano hayo yanaendelea na kuelezea matumaini yake kwamba, makubaliano ya haki yatapatikana, ambayo yatahakikisha kuwa taasisi za kidemokrasia zinaendelea kukua visiwani hapa.

"Bila shaka, muafaka siyo suala pekee linaloongelewa na Marekani hapa. Tunajaribu pia kuunga mkono wito wa Rais Kikwete wa kuimarisha zaidi uwazi, pamoja na kupiga vita rushwa.

"Njia moja tunayotumia kufanikisha masuala haya ni kupitia sheria ya taasisi ya Millennium Challenge. Hii ina mpango wa awali unaoitwa Threshold Program, ambao lengo lake ni kuimarisha asasi za kiraia, pamoja na waandishi wa habari katika kazi yao kama 'walinzi' dhidi ya rushwa," alisema.

Alisema kupitia mpango wa kufuatilia matumizi (PETS), idadi ya habari za rushwa zinazoandikwa kila mwezi nchini imeongezeka mara saba.

"Nimepata fursa ya kutembelea sehemu nyingi zinazotekeleza mfumo wa PETS katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Morogoro. Lilikuwa ni jambo zuri sana kuona wananchi wa kawaida wakija pamoja kuhamasisha uwazi. Ilikuwa inasisimua kuwaona Watanzania hawa wema wakipata taarifa zaidi kuhusu fedha za umma, na jinsi zinavyotumika," alisema.

Alisema mpango wa Threshold, unatangulia mkataba wa msaada kutoka kwenye Mfuko wa Millennium Challenge Account na utakapotiwa saini mapema mwaka kesho, msaada huo utatoa dola milioni 698 kwa kipindi cha miaka mitano, kusaidia utekelezaji wa miradi ya miundombinu, nishati, pamoja na maji safi nchini kote.

Mbali ya hayo alisema nchi yake ina dhamiria kujikita zaidi visiwani Zanzibar katika shughuli zake kwa kuweka mwakilishi wa kudumu wa taifa hilo atakayekuwa akifuatilia shughuli mbalimbali za ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

"Maofisa kutoka Ubalozi wa Marekani huwa wanasafiri kuja hapa karibu kila siku, na ninaamini wengi wenu mnamfahamu Mussa Shehe, msaidizi wetu wa masuala ya kisiasa na ya umma, ambaye anafanya kazi nasi hapa Zanzibar," alisema.

Green alisema kuwa uamuzi wa Marekani kumweka mtu wake wa kudumu Zanzibar unatokana na ukweli kuwa kuna miradi mingi sana inayotekelezwa na Marekani.

"Kwa mfano, kupitia mfuko wa Balozi wa kuhifadhi utamaduni, Marekani imesaidia kukarabati misikiti miwili Pemba, imekarabati nyumba ya makumbusho ya Chake Chake, iliyo kwenye ngome ya karne ya 18 na kusaidia kuhifadhi muziki wa taarab," alibainisha.

Aidha, alisema kuwa mfuko wa Balozi wa kusomesha wasichana unasaidia kugharamia elimu ya wasichana takriban 300 kutoka visiwani hapa, kuanzia elimu ya msingi hadi masomo ya sekondari.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.