JUHUDI za serikali kuwasafirisha mahujaji waliokwama kwenda kuhiji Makka, zimeshindwa kuzaa matunda kwa wakati muafaka, baada ya ndege iliyokodiwa kutoka Kampuni ya AL-Wassam kushindwa kuhimili safari za kuwasafirisha mahujaji hao baada ya kuharibika.
Hiyo ilikuwa ni ndege pekee, kati ya tatu ambazo zilitafutwa, ambayo ilifanikiwa kupeleka kundi la kwanza la mahujaji 379, lakini iliporejea kuwafuata wengine jana ilipata hitilafu za kiufundi na jitihada za kuitengeneza zilikwama baada ya kuelezwa kuwa vinahitajika vipuri vingine kutoka Afrika Kusini.
Hata hivyo, katika safari hiyo ya kundi la kwanza, serikali ilijikuta ikilazimika kulipa faini ya dola za Marekani 6,000 kutokana na ndege hiyo kuchelewa kufika kulingana na ratiba iliyokuwa imepangiwa.
Baada ya Madina, ndege hiyo ililazimika kuchelewa angani kwa nusu saa, baada ya kuzuiliwa, kwa maelezo kuwa imechelewa kufika kulingana na kibali kilivyoonyesha kuwa ilitakiwa kufika saa nane mchana.
Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana, Mwenyekiti wa Bodi ya ATC, Mustaafa Nyang'anyi, alisema kuwa baada ya ndege hiyo kufika katika anga za Madina, pamoja na kuwa na kibali maalumu kilichoombwa baada ya viwanja vya ndege kufungwa, ilielezwa kuwa haiwezi kutua kutokana na kuchelewa na hivyo kutozwa faini hiyo.
Awali, ndege hiyo ambayo ilikuwa imekaa uwanjani hapo tangu Jumanne usiku kwa kukosa kibali cha kwenda Jeddah, ilitakiwa iondoke juzi saa nne asubuhi, baada ya kibali kupatikana.
Hata hivyo, kibali hicho hakikuwa na namba ya kupaki ndege, hali iliyozidi kuchelewesha safari hiyo na kumlazimu Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kukatisha ziara yake mkoani Kagera na kumuita Balozi wa Saudi Arabia, ambapo walifanya mazungumzo na kupata kibali kamili na kisha ikapangiwa iondoke saa 10 jioni.
Hata hivyo, katika mazingira ya kutatanisha ilishindwa kuondoka hadi saa moja jioni.
Iliporejea Dar es Salaam baada ya kulifikisha kundi la kwanza la mahujaji, ndege hiyo ilikumbwa na balaa jingine baada ya kuelezwa kuwa imeharibika na jitihada za kuitengeneza zimeshindikana, kwa kuwa karakana ya uwanjani hapo haikuwa na vipuri vilivyohitajika kwa matengenezo hayo.
Baadaye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, ambaye katika siku tatu zilizopita amekuwa akishinda uwanjani hapo, alisema kuwa kifaa kilichohitajika kimeagizwa Afrika Kusini, jambo ambalo liliwafanya mahujaji waliokuwa wameanza kurejewa na matumaini ya kusafiri kukata tamaa.
Baadhi yao walionekana wakilengwalengwa machozi huku wakiwa na nyuso za simanzi na kutoamini kile kilichotokea.
Kwa upande mwingine, mahujaji kutoka Comoro, Msumbiji na DRC, ambao waliletwa kwa ajili ya safari hiyo na mashirika mengine ya ndege, wapo kwenye hali mbaya zaidi baada ya ATC kudai kuwa jitihada zake zinaelekezwa katika kuwasafirisha Watanzania kwanza.
ATC ilisema kuwa, mahujaji hao kutoka nje watasafirishwa iwapo tu itapatikana nafasi katika ndege hiyo itakapopona. Ilitarajiwa kuwa ndege hiyo ingefanya safari yake ya pili jana jioni na kurejea kuwafuata mahujaji wengine.
Awali, iliripotiwa na mahujaji hao kuwa taasisi zinazopaswa kuwasafirisha zililipa pesa ATC kwa ajili ya kupelekwa hijja na ndiyo maana walifika hapa kwa ajili ya safari hiyo ambayo wameendelea kuisubiri.
Lakini juzi wakati Kandoro akitoa taarifa alisema kuwa wao wanashughulikia mahujaji 1,177 tu wa hapa nchini na kuongeza kuwa, ndege ya kwanza inatakiwa kupeleka mahujaji 379, kisha kurudia wengine wakati serikali ikifanya mpango wa kupata ndege nyingine ya kuwapeleka 300 waliosalia.
Alisema iwapo itapatikana nafasi, hao wengine watasafirishwa mwisho kama msaada tu.
Hata hivyo, jana, wakati ndege iliporipotiwa kuharibika, Mwenyekiti wa mahujaji hao kutoka nje, Seif Amir Ullah, alimweleza Nyang'anyi kuwa wanahitaji huduma muhimu.
Nyang'anyi katika jibu lake kwao, aliwataka kuwasiliana na kampuni za ndege zilizowaleta au wafuate taratibu za uhamiaji.
Wakati utata huo ukizidi kujitokeza, baadhi ya Waislamu wameendelea kumwaga misaada ya vyakula ili kuwasaidia mahujaji baada ya kulalamika kuwa wameishiwa pesa za kununulia maji na chakula.