NIMESUKUMWA na kauli ya Kingunge Ngombale-Mwiru kujadili kauli yake kwamba “Mjadala wa katiba umefungwa.”
Kingunge bingwa wa propaganda za Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu enzi, amesema hadharani kwamba chama hicho katika ilani yake ya uchaguzi hakina sera ya kutaka kuandikwa kwa katiba mpya na kwa maana hiyo mjadala huo kwao umefungwa.
Kingunge, Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Siasa na Uhusiano wa Jamii, alitoboa yaliyoko moyoni mwake alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wiki iliyopita, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa serikali kwa kila waziri kueleza utendaji wa wizara yake.
Kauli hii ni kama moshi waliowashiwa nyuki wakaukimbia mzinga wao, na pengine ni kama maji ya moto yaliyomchomoa nyoka pangoni. Nimechomoka mafichoni na sasa ninajibu au kujadili kauli ya Kingunge, ninaandika ili kuanzisha mjadala mpana.
Awali ya yote, ninaomba kurejea maandiko ya mwandishi mmoja akizungumzia kauli ya Kingunge aliyotoa Septemba mwaka huu juu ya madai ya wapinzani na ufisadi wa viongozi waandamizi serikalini.
Mwandishi huyo alimtaja Kingunge kama kiongozi aliyepitwa na wakati, amekosa mshiko na haelewi kwamba kila zama ina vitabu vyake. Mwandishi huyo aliandika akitathmini kauli ya Kingunge katika kujibu tuhuma za ufisadi dhidi ya viongozi waandimizi wa serikali na chama tawala.
Kingunge alisema kwamba serikali ina kazi za kufanya na kwamba haiwezi kujibishana na wapinzani juu ya tuhuma za ufisadi.
Muda haukupita, hoja ya ufisadi ikapamba moto na kuenea nchi nzima. Moto ulipokolea sana juu ya tuhuma za ufisadi na nguvu za kutaka kukomboa rasilimali za taifa hili zinazohujumiwa na wenye dhama za ofisi za umma, watawala wamefungua masikio wamechukua hatua.
Kwa hakika uundwaji wa kamati ya kupitia mikataba ya madini na hata kuchunguzwa kwa tuhuma za ufisadi za Benki Kuu bila kusahau uchunguzi wa mkataba wa Richmond Development Corporation, ni matokezo ya kupigwa kelele dhidi ya ufisadi huo.
Kwa maneno mengine, kilichotokea sasa ni kinyume kabisa cha alivyodhani na kutaka Kingunge. Kwamba serikali badala ya kupuuza tuhuma za ufisadi dhidi yake na baadhi ya vigogo, inafanya kinyume chake.
Kwa hiyo aliyepuuzwa hapa ni Kingunge na si wapinzani. Kwamba serikali imekwepa ile hulka na staili ya akina Kingunge ya kukataa kusema lolote, kukataa kuchukua hatua na kwa hakika imechoswa kuanikwa hadharani kwa madhambi mengine ya kujitakia yaliyofanywa na sasa inataka kujisafisha.
Kwa maana hiyo basi, hata kauli ya Kingunge kwamba eti hakuna mjadala wa katiba mpya kwa sababu hilo si suala la CCM, ni kauli nyingine inayotolewa na kiongozi ambaye amepitwa na wakati, kiongozi anayeshindwa au hataki ama hawezi kusoma alama za nyakati.
Kingunge kujigamba kwamba hakuna mjadala wa katiba mpya Tanzania, ni sawa na mtu aliyekaa uchi, lakini anasema hahitaji nguo. Kingunge ni lazima atambue mambo muhimu katika taifa hili kwa sasa, na awe tayari kukubali mabadiliko.
Kwamba Kingunge ni lazima afahamu kwamba zile zama za kung’ang’ania sera na itikadi ambazo zimekwisha kushindwa, zimepitwa na wakati na sasa watu wanataka kushirikishwa katika mchakato mzima wa utawala wa nchi yao.
Ili kubainisha ukweli huu, naomba kumkumbusha Kingunge mambo makuu mawili ya msingi. Moja, kwamba Katiba ya Tanzania ya sasa halingani wala kurandana na mazingira tunayoishi leo.
Hii ni katiba ambayo kwa kiwango kikubwa inajisimika mno kwenye mfumo wa chama kimoja. Ni katiba ambayo inaamini tu kwamba wenye haki ya kutawala kwa asilimia mia ni wale walioshinda uchaguzi, ni katiba ambayo haitambui kwamba kuna uwezekano wa siku moja kutokea kwa rais aliyechaguliwa na watu wachache (minotity) kwa sababu tu atakuwa ameongoza kwa wingi wa kura miongoni mwa wagombea wengi.
Katiba ya sasa ya nchi hii imejielekeza kujenga watawala wenye nguvu kama miungu watu, viongozi wasiopingwa. Watawala wenye uwezo wa kuumba kila kitu bila kuhojiwa hata na taasisi nyingine za madaraka ya dola.
Hii si katiba inayoakisi jamii inayoishi katika misingi ya demokrasia pana ya uwakilishi. Jamii inayoshiriki katika utawala wa nchi yao kwa maana pana zaidi haisubiri kupiga kura tu kila baada ya miaka mitano na kwenda kulala.
Lakini la pili na muhimu, inabidi mzee Kingunge ajikumbushe kwamba hadi leo Tanzania kama taifa, haina mwafaka wa kitaifa. Haina mwafaka huo kwa sababu nchi hii inaendeshwa kwa awamu.
Awamu ya kwanza na yake, ya pili vivyo, ya tatu sawia na ya nne na mambo yake. Kila awamu inajidai kuwa na itikadi yake, lakini kimsingi ukiacha awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere, awamu nyingine zote hazina itikadi! Hazina dira, hatujui tulipo, tunataka kwenda wapi na tutakwenda vipi.
Ni kwa sababu ya kukosekana kwa hali hiyo si ajabu kumwona mtu kama Kingunge akiwamo ndani ya awamu zote.
Wakati wa Mwalimu Nyerere na Azimio la Arusha alikuwako, akaja Ali Hassan Mwinyi na Azimio la Zanzibar Kingunge yumo, akaja Benjamin Mkapa na utandawazi Kingunge yupo, sasa tunaambiwa Jakaya Kikwete ni wa mrengo wa kushoto kati, Kingunge yumo.
Haiwezekani kuweza kutumikia awamu zote kwa hakika kama kweli kuna kitu kinachoitwa itikadi ya dhati na ambayo inatafsirika katika sera za kweli na mikakati sawia.
Ndiyo maana Kingunge anaposema kwamba katiba mpya hapana, sisi tunaoweza kusoma alama za nyakati tunamwona kama tulivyomwona hivi karibuni akibeza tuhuma za ufisadi.
Kabla ya kuhitimisha mjadala huu ningependa kumuuliza Kingunge kama anaweza kusema kwa yakini kabisa madaraka aliyokuwa nanyo rais leo ni haki na halali katika nchi inayojigamba kwamba inaendesha utawala wa demokrasia, rais asiyehojiwa kokote, akiwa madarakani na hata baada ya kuondoka?
Ni kwa kiwango gani basi Kingunge anaweza kueleza Watanzania wamuelewe kama kweli rais anawezaje kuwafahamu mawaziri wote, manaibu waziri wote, wakuu wote wa mikoa, wakuu wote wa wilaya, wakuu wote wa mashirika na taasisi za serikali zinazojitegemea, wakuu wa vyombo vya usalama, wakuu wa mahakama, wakuu wa kila kitu? Hivi ni kwa nini uteuzi wa hawa wote ufanywe na rais peke yake, tena bila kuthibitishwa kokote?
Katiba ya nchi hii si tu imejenga rais mfalme, bali pia wapo watu kama akina Kingunge ambao wao ni matokeo ya mfumo huo na asilani wasingependa kuona mfumo huo ukibadilishwa, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwaeleza kwamba wafungue milango ili mfumo wa utawala ushirikishe wengi zaidi na kwa manufaa ya umma kwa ujumla wake.
Kauli za kung’ang’ania ukale, ni matokeo ya kuwa na fikra za kihafidhina. Hakuna mabadiliko, na kwa maana hiyo hakuna maendeleo. Hili ndilo linamkabili mzee wetu Kingunge.
Kwa takribani miongo minne Kingunge amekuwako kwenye ngazi za utawala. Ametetea ukale na ‘status quo’ kwa muda mrefu, kwa maana hiyo kwa kauli kwamba hakuna mjadala wa katiba mpya si kauli ya bahati mbaya, bali ndiyo undani wa kiongozi huyu anayetaka Watanzania wote wakubali kuendelea kuishi katika maisha ya ukale, maisha ya kujenga watawala miungu watu, kukubali kutawaliwa na si watu kushiriki katika utawala wa nchi yao.
Maendeleo ya kweli katika taifa hayawezi kuja kama kila mdau hatakuwa na haki ya kushiriki kutoa maamuzi katika mambo yanayomhusu.
Chimbuko la madaraka ni watu na watu ni lazima washiriki katika kujitawala. Katiba ambayo ni mkataba wa wananchi jinsi wanavyotaka wajitawale ni lazima ipate ridhaa yao.
Kwa bahati mbaya Kingunge anafahamu Katiba ya Tanzania haijawahi kupata ridhaa ya wananchi kwa maana ya kuwashirikisha kuitunga na kuitolea maoni hasa kulingana na maisha ya sasa.
Je, anafikiri kutokuwa kwenye ilani ya CCM au kuwako kunabadili maana na umuhimu wa kuwa na katiba mpya kwa sasa?