CHAMA cha Maalbino nchini (TAS) kimeazimia kumuona Rais Jakaya Kikwete ili ashughulikie haraka suala la mauaji ya maalbino yanayoshamiri hivi sasa nchini.
Hilo ni miongoni mwa maazimio ya kikao cha maalbino kilichomalizika jana mjini hapa, kujadili namna ya kukabiliana na mauaji hayo.
Mwenyekiti wa TAS, Ernest Kimaya, alisema kuwa awali, yatafanyika maandamano ya nchi nzima kuonyesha kupinga kwao na kulaani mauaji hayo, hasa baada ya serikali kukaa kimya baada ya mauaji hayo.
Aidha, alisema kabla ya maandamano hayo, wataandaa mkutano wa waandishi wa habari na kuwakaribisha maofisa wa Jeshi la Polisi nchini, ili waeleze jeshi hilo limefanya nini kukabiliana na mauaji hayo.
Kimaya alisema kuwa ni jambo lililo dhahiri kuwa, mauaji hayo ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao umekuwa ukifumbiwa macho na mamlaka husika.
Hadi hivi sasa takriban watu wanne ambao ni maalbino, wameripotiwa kuuawa na mauaji hayo yanahusishwa na imani za kishirikina, na mwenyekiti huyo alisema hakuna ushahidi wa wazi kuonyesha kuwa kuna hatua zilizochukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Naye Katibu wa TAS, Samwel Mluge, ameitaka jamii kuungana kwa pamoja kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu na mauaji ya maalbino.
Alisema inashangaza pia kuwa Tume ya Haki za Binadamu, Kituo cha Haki za Binadamu na Utawara Bora na taasisi nyingine kadhaa zinazojihusisha na utetezi wa haki za binadamu, zimekaa kimya kuhusu suala hilo.
“Uhuru wa nchi si bendera pekee, bali inatakiwa na watu wake kuwa huru tofauti na hali ilivyo kwa maalbino ambao sasa hawako huru,” alisema Mluge.
Mkutano huo wa siku mbili uliwahusisha viongozi wa chama cha maalbino wa mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, mwakilishi toka shirikisho la watu wenye ulemavu Barani Afrika tawi la Tanzania, Chama cha Wasioona na watendaji wakuu wa TAS.