Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali kunusuru mahujaji?
Serikali kunusuru mahujaji?
By Habari Tanzania | Published  12/11/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
na Mobin Sarya


SERIKALI imeingilia kati sakata la kukwama kwa mahujaji wanaokwenda Makka na kuamua kutafuta suluhu ya dharura ya kuwasafirisha kwa awamu mbili, wakati siku ya leo ikiwa ndiyo ya mwisho.

Taarifa za uhakika kutoka serikalini zinaeleza kuwa hatua hiyo ilikuja baada ya mahujaji waliokuwa wasafirishwe na ATC kushindwa kuondoka hadi kufikia jana usiku baada ya kukosekana ndege kwa zaidi ya wiki moja, hali iliyozusha malalamiko kutoka kwa mahujaji hao.

Inadaiwa kuwa hatua ya ATC kushindwa kuwasafirisha mahujaji hao, iliishitua serikali na hatua ya juzi usiku ya mke wa Rais, Salma Kikwete, kwenda kuwafariji mahujaji hao akitokea Dodoma alikokwenda kuhudhuria maadhimisho ya miaka 46 ya uhuru ilitokana na hali hiyo.

Mke wa Rais alifika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) na akawataka kuendelea kuwa na subira wakati serikali ikifanya kila linalowezekana ili waweze kusafiri.

Hata hivyo hadi tukienda mitamboni jana usiku, katika uwanja huo wa ndege, kikao kati ya Bodi ya Wakurugenzi wa ATC kikiongozwa na Mustafa Nyang'anyi na viongozi wa mahujaji hao kilikuwa kikiendelea ili kupata suluhu ya kudumu.

Ofisa mmoja wa juu wa serikali aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini, alisema dalili zilikuwa zikionyesha kuwa kundi la kwanza la mahujaji hao lingeondoka usiku wa kuamkia leo wakati wengine waliobaki wanatarajia kuondoka wakati wowote leo hii.

"Kimsingi tatizo limeshapata suluhisho. Kundi la kwanza la mahujaji linatarajia kuondoka usiku huu na wengine wa mwisho wataondoka kesho (leo)," alisema ofisa huyo.

Wakati mahujaji hao wakisubiri hatima yao, juzi usiku Nyang'anyi ambaye ni Mwenyeki wa Bodi ya ATC, aliwaambia mahujaji mbele ya Salma kuwa, ndege ya kuwachukua iliyokodiwa kutoka Saudia ilikuwa njiani ikielekea Dar es Salaam ambako ilitarajiwa kufika wakati wowote na kuwachukua mahujaji 379 wa kwanza, ahadi ambayo hadi jana saa 2:00 usiku ilikuwa haijatimia.

Kutokana na ahadi hiyo, mahujaji waliopangiwa kusafiri na ndege hiyo wakiwamo wale wanaotoka katika mataifa mbalimbali jirani, walianza kukamilisha taratibu za safari uwanjani hapo, ikiwamo kukaguliwa kwa ajili ya safari.

Hata hivyo, walipokuwa katika hatua za mwisho za ukaguzi, waliambiwa kuwa ndege hiyo ililazimika kurudi ilikotokea baada ya kunyimwa kibali cha kukatisha katika anga ya Ethiopia na Sudan.

Ilipotimu majira ya saa saba mchana jana, ndege kubwa ya Emirate iliwasili na kusababisha mahujaji kutaharuki wakidhani kuwa ndege hiyo imekuja kuwafuata wao, bila kujua kuwa ilikuwa imewabeba mahujaji 200 kutoka nchini Comoro waliokuja kuungana nao katika safari kuelekea Saudia kupitia ATC.

Baada ya muda mfupi waliwasili mahujaji wengine 22 kutoka DRC walioletwa na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Katika kile kilichoonekana kuwa kutafuta suluhu, jana mahujaji hao walifanya mkutano mrefu na maofisa wa ATC na inadaiwa kuwa kiongozi mmoja wa juu wa serikali alikuwa akifuatilia kwa karibu mkutano huo kwa njia ya simu na kuhoji ni kwa nini ATC ilitoa taarifa kuwa ndege imeisharuka na mpaka sasa haijafika.

Mmoja wa mahujaji wanaosafiri kupitia Hajj Trust, Juma Nchia, ambaye alihudhuria kikao cha kwanza, aliliambia gazeti hili uwanjani hapo kuwa viongozi wa ATC walijiteteta wakidai kuwa ofisa mmoja wa ubalozi wa Tanzania aliyeko Saudia ndiye aliwapa taarifi hizo.

Nchia alidai kuwa, katika kikao hicho, ilielezwa kuwa serikali ilikuwa imeomba ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 200 kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Saudia lakini hadi jana jioni ndege hiyo nayo ilikuwa haijawasili.

Hata hivyo, katika mwendelezo wa ahadi zao, viongozi wa ATC nao waliendelea kusisitiza kuwa wamekodi ndege tatu kutoka katika Shirika la Al-wasam ambazo zitawachukua abiria 379.

Nchia alisema kuwa pamoja na kuwa ATC wameanza kuwapatia chakula na kuwatafutia malazi katika mahoteli, bado shirika hilo linawajibika kwa kila namna kwa usumbufu walioupata.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.