BAADHI ya wakazi wa Dar es Salaam jana waliipasha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwa hawana imani nayo kutokana na kutoa ripoti zinazoleta shaka.
Wakizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Takukuru kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maadili jana, wananchi hao walihusisha ushiriki wa taasisi hiyo katika sakata la Kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development (RDC) kuwa ni moja ya matukio yaliyowafanya wapoteze imani na Takukuru.
Walisema kitendo cha Takukuru kufanya uchunguzi na kubaini kuwa hakukuwa na rushwa katika suala la kuipata kampuni hiyo, na baadaye Bunge kuunda kamati ya kupata maoni kuhusiana na suala hilo, baada ya kubaini kuwa kuna harufu ya rushwa, kinaishushia hadhi taasisi hiyo.
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa masuala ya Bunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema, alipokuwa akichangia mada kwenye mdahalo wa wazi kuhusu Rushwa na Maadili.
"Takukuru ni waongo, kwani hufanya kazi yao kwa kuwaogopa wanasiasa na hivyo kushindwa kutimiza maadili ya kazi yao," alisema Mrema.
Mrema aliwataka Takukuru kuacha kuwa wanasiasa, kwani wanatakiwa kufuatilia tuhuma wanazoletewa na kuacha kuhoji ushahidi, kwani wao ndio wanatakiwa kuchunguza na kutafuta ushahidi huo na si mtoa taarifa.
Aidha, Mrema alisema viongozi wanaotiwa hatiani kwa tuhuma za rushwa wasipewe adhabu ndogo ndogo bali wapewe adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kufilisiwa mali zao zote.
Pia alisema sekta binafsi nako kunafukuta rushwa kutokana na kukosekana kwa maadili, hasa ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya shughuli nchini hufanywa na kampuni na taasisi binafsi.
"…kwa mfano hapa tupo katika mjadala wa rushwa na tumepewa T-shirts za Takukuru huku pembeni zikiwa na nembo ya ENGEN, ambalo ni kampuni la mafuta. Unafikiri kampuni hii ikiwa na tuhuma za rushwa wataweza kuwakamata wakati ni wafadhili wao? Hapa maadili yatatoka wapi?" alihoji Mrema.
Alisema ili Takukuru na hata serikali iwe huru kufanya mambo yake bila kuathiriwa, ni lazima iachane na kutegemea wafadhili, hasa kampuni binafsi.
Wakati huo huo, Abubakar Kitogo ambaye ni Ofisa wa Chama cha Wananchi (CUF), akichangia katika mdahalo huo, alidai kuwa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi imeshindwa kufanya kazi yake ipasavyo, kwani haijaonekana kuchukua hatua dhidi ya wala rushwa.
"Nimesema hivyo kwa kuwa wanasiasa wameishasema na kutoa ushaidi kuhusiana na tuhuma za rushwa, ikiwa ni pamoja na nyumba zilizouzwa, mkataba wa Richmond, Buzwagi na mingine mingi lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa," alisema.
Kitogo alisema hii yote inasababishwa na katiba mbovu iliyopo na bila kuifanyia marekebisho itakuwa vigumu kupambana na rushwa na kushinda.
"Hata rais anawajua wala rushwa kwa majina… kusema eti anawapa muda wajirekebishe, hii inathibitisha hata hii taasisi ya Takukuru ni uzushi mtupu," alizidi kudai.
Naye Zawadi Sanga, mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Ualimu Chang'ombe (DUCE), alisema viongozi wa ngazi za juu ndio wanajenga mazingira ya rushwa na kuishia kuunda tume nyingi ambazo hutumia fedha nyingi bila kuleta majibu yoyote ya maana.
Sanga alisema serikali ikitaka kutokomeza rushwa ni lazima ihakikishe inaboresha masilahi ya watumishi wake, kwani inasikitisha kuona mfanyakazi analipwa sh 80,000 na ana familia inayomtegemea.
"Huyu akipokea rushwa kweli utamlaumu?" alihoji na kuongeza:
"Na hii ndiyo sababu inayofanya hata maprofesa wengi kuacha kazi ya kufundisha na kujiingiza katika mambo ya kisiasa ili waweze kupata masilahi yatakayo wawezesha kukimu mahitaji yao muhimu."
Pia Edwin Chitage, ambaye ni Rais wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo cha Sayansi za Tiba Muhimbili, alisema ili kuhakikisha rushwa inaondoka katika taasisi za umma, kinachotakiwa si kuboresha masilahi ya wafanyakazi tu, bali kuboresha huduma pia.
Chitage alisema katika hili, viongozi wakubwa wanapaswa kuacha tabia ya kwenda kufanya ziara mahospitalini kwa nia ya kujionyesha tu, bali wawe wanakwenda kupeleka vifaa mbalimbali.
Aidha, Chitage alisema ni vigumu kuzungumzia suala la maadili wakati haijulikani hasa nchi inafuata siasa gani, kati ya ujamaa inayoelezwa katika katiba au ubepari, ambayo ndiyo inayoonekana katika hali halisi.
Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Loyola, Godfes Msofe, alisema rushwa haitaisha nchini kutokana na viongozi, hasa wa ngazi za juu, kutokuwa waaminifu, waadilifu na kulindana katika utendaji wao wa kazi.
Msofe alisema kuna baadhi ya mifumo haipo wazi, na kutoa mfano wa suala la kusainiwa kwa mikataba mbalimbali, ambayo hufanywa kwa siri bila wananchi kujua.
Mjumbe mwingine ambaye jina lake halikupatikana mara moja, aliituhumu Takukuru na kusema kuwa si taasisi ya kuaminika kwa kuwa haionyeshi mafanikio katika vita dhidi ya rushwa.
Mjadala huo wa wazi uliokuwa unaendeshwa na mhadhiri wa Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (IJMC), Ayub Rioba, uliandaliwa na Takukuru, ikiwa ni moja ya maadhimisho ya Siku ya Maadili Kitaifa ambayo hufanyika Desemba 10 kila mwaka. Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa ni "Kukataa kwako rushwa kuna thamani."
Mjadala huu ulikuwa na utangulizi wa mada tatu ambazo ni umuhimu wa maadili ya umma kama njia ya kuzuia rushwa, umuhimu wa kuzingatia maadili katika utendaji wa sekta binafsi na wanafunzi na mapambano ya rushwa na ulishirikishaji wa wanafunzi kutoka sekondari na vyuo mbalimbali