BAADA ya vuta nikuvute ya takriban miaka miwili sasa, Rais Jakaya Kikwete amekata mzizi wa fitina na akabariki kufanyika kwa mabadiliko makubwa ya wakurugenzi katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Katika mabadiliko hayo mazito, ya kwanza ya aina yake katika wizara hiyo tangu yale yaliyopata kumgusa waziri na baadaye katibu mkuu, Emmanuel Severe aliyekuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori, ameondolewa katika nafasi yake hiyo.
Kuondolewa kwa Severe ambaye mara kadhaa jina na idara yake vimekuwa vikihusishwa na matatizo ndani ya wizara hiyo, kunaweza kuonekana kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika wizara hiyo ambayo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Mabadiliko hayo ambayo yamekuja yakiwa yamechelewa, yalitangazwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, ambaye aliwahakikishia waandishi wa habari kuwa yalikuwa yamepata baraka zote za Rais Kikwete.
Maghembe katika taarifa yake hiyo, alisema nafasi ya Severe ambaye atapangiwa kazi nyingine, imechukuliwa na aliyekuwa Ofisa Wanyamapori Mkuu, Erasmus Tarimo.
Kuondolewa kwa Severe kunakuja baada ya jitihada zilizofanywa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili, Anthony Diallo kumng’oa bila ya ridhaa ya rais mwaka jana kugonga mwamba.
Severe anaondoka akiacha kumbukumbu ya kukataa waziwazi kung’olewa madarakani na Diallo, hata kufikia hatua ya kusema mtu pekee aliyekuwa na ubavu wa kumng’oa alikuwa ni yule aliyemteua, akimaanisha rais.
Baada ya kauli hiyo ya kijeuri ya Severe, maneno mengi ya chinichini yalikisika yakisemwa juu yake, na namna uongozi wa juu serikalini ulivyokuwa ukimkingia kifua.
Miongoni mwa viongozi wa juu serikalini waliotajwa kuwa walikuwa wakimlinda Severe asing’olewe madarakani, alikuwa ni Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo ambaye zama za Serikali ya Awamu ya Tatu, alipata kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakifanya kazi kwa karibu.
Aidha, tukio hili la sasa linakuja baada ya vyombo kadhaa vya habari likiwamo gazeti hili, kuwa mstari wa mbele kuandika habari mbalimbali kuhusu matatizo ya idara hiyo ya wanyamapori kwa muda mrefu sasa.
Mbali ya vyombo vya habari kupigia chapuo haja ya lazima ya kubadilishwa kwa uongozi katika idara hiyo ya wanyamapori, Benki ya Dunia katika taarifa yake moja ya mwishoni mwa mwaka jana, iliainisha jinsi nchi inavyopoteza mabilioni ya shilingi kila mwaka kutokana na njama zinazowahusisha viongozi ndani ya wizara hiyo, wanaoshirikiana na wageni waliohodhi vitalu vya uwindaji wa kitalii hapa nchini.
Aidha kabla na baada ya ripoti hiyo ya Benki ya Dunia,
ripoti mbalimbali za uchunguzi zimepata kueleza namna taifa hili lisivyofaidika na uwindaji wa kitalii kutokana na sababu mbalimbali zilizo wazi, zikihusisha maamuzi mabaya ya kiuongozi katika Idara ya Wanyamapori na wizara.
Uongozi wa Severe umekuwa ukituhumiwa kukataa kutekeleza mapendekezo mbalimbali ya kitaalam ya kuboresha sekta ya wanyamapori, ambayo yalitolewa miaka 12 iliyopita.
Mapendekezo hayo yalihusu mabadiliko ya sera na menejimenti; na kwamba yalihusu kuufumua muundo mzima wa idara ili iweze kuwatendea haki wadau, hasa Watanzania wazalendo, lakini hakuna kilichotekelezwa.
Miongoni mwa sababu ambazo Severe alikuwa akihusishwa nazo, ni bei ndogo ya uwindaji wa wanyama katika mbuga, ambazo zilikuwa zikitumika kabla ya mabadiliko ya hivi karibuni yaliyoongozwa na Waziri Maghembe.
Chini ya uongozi wa Severe, bei ya kuwinda tembo ilikuwa ikifikia dola 4,000 za Marekani kiasi ambacho kilikuwa kikionekana kuwa kidogo kuliko ilivyo katika mataifa mengine duniani kama Botswana ambako mnyama huyo huuawa kwa dola 19,000.
Aidha, bei ya simba kuuawa ilikuwa ni dola 2,000 ilhali nchini Botswana simba huyo huyo alikuwa akiuawa kwa dola za Marekani zaidi ya 5,000.
Wakati malalamiko hayo yakitolewa, idara hiyo ilikuwa ikichangia wastani wa sh bilioni 10 kwa mwaka, kiasi ambacho wachunguzi wa mambo wanasema ni kidogo kwa mara tatu ya kile ambacho taifa lingekipata iwapo mabadiliko ya kisekta yangefanyika.
Akitangaza mabadiliko zaidi jana, Waziri Maghembe aliwataja wakurugenzi wasaidizi wa Idara ya Wanyamapori kuwa ni Obedi Mbangwa (Mkurugenzi msaidizi matumizi ya Wanyamapori), Boneventura Midala (Mkurugenzi msaidizi kupambana na Majangili) ambaye amechukua nafasi ya Felix Lyimo.
Maghembe aliwataja wasaidizi wengine kuwa ni Maria Zakaria (Mkurugenzi msaidizi maendeleo ya Wanyamapori) ambaye amechukua nafasi ya Mdoe, huku Mkurugenzi msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu akipewa Nebbo Mwina. Nafasi hii awali ilikuwa ikishikiliwa na Rehema Tibanyenda.
Katika hatua nyingine, Benjamin Andulege aliteuliwa kuwa Meneja Mfuko wa Wanyamapori (TWPF) nafasi iliyokuwa ya Sarakiki.
Waziri Maghembe alisema kwa upande wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dk. Felician Kilahama ameteuliwa kuwa Mkurugenzi, nafasi ambayo ilikuwa ikikaimiwa na Dk. Aloyce Tango ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Misitu.
Nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Ufugaji Nyuki sasa inachukuliwa na Gladness Mkamba, huku Hadija Ramadhani akiteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi ya Misitu (Utilization).
Katika mabadiliko hayo, Monica Kagya aliyekuwa Naibu Mkurugenzi amepandishwa cheo na kuwa Mkurugenzi Msaidizi Mafunzo, Utafiti na Takwimu.
Maghembe alisema katika Idara ya Uvuvi hakuna mabadiliko yaliyofanywa na hivyo kumuacha, Godfrey Nanyaro akiendelea na wadhifa wake wa ukurugenzi.
“Tumefanya mabadiliko ya wakurugenzi wasaidizi ambapo, Winfried Haule ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu katika idara hiyo,” alisema Maghembe.
Katika mabadiliko hayo, Hosea Mbilinyi ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Usimamizi na Udhibiti wa Uvuvi, wakati Mwanaidi Mlowa akiteliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ubora wa Samaki na Masoko na Esther Mndeme akichukua nafasi ya kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Uvuvi.
Kwa upande wa Idara ya Utalii, Maria Mmari ameteuliwa kuwa Mkurugenzi huku aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo Ibrahimu Mussa akikabidhiwa jukumu la kuwa Mkurugenzi Msaidizi Mafunzo, Utafiti na Takwimu.
Aloyce Nzuki anaendelea kushika nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Mendeleo ya Utalii na Uzeeli Kiangi akipewa nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Udhibiti wa Leseni (Licensing and Quality Control).
Idara ambazo pia hazijakumbwa na mabadiliko hayo ni pamojua na Idara ya Mipango ambayo inamfanya mkurugenzi wake T.F Killenga kuendelea na kazi na ile ya Mambo ya Kale ambayo inaongozwa na D.M.K Kamamba.
Maghembe alibainisha kuwa serikali itawapangia kazi nyingine wakurugenzi na wakurugenzi wasaidizi waliobadilishwa na akakataa kusema wamepangiwa kazi gani.