MATOKEO ya kura ya maoni iliyoendeshwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (REDET) yamepokewa kwa hisia tofauti na watu wa kada mbalimbali nchini.
Watu mbalimbali waliotoa maoni yao, wakiwamo wanasiasa, wanataaluma, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida, wameuelezea utafiti huo wa REDET kuwa changamoto muhimu kwa Rais Jakaya Kikwete na serikali yake kuchukua hatua za mara moja kurekebisha mambo.
Akizungumzia utafiti huo na hususan takwimu zinazoonyesha kuporomoka kwa umaarufu wa Rais Kikwete na serikali yake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kanda ya Kati, Ainea Kusenha, amesema baadhi ya matatizo yanayoikabili serikali kwa sasa, yapo nje ya uwezo wa binadamu.
Kutokana na hali hiyo, askofu huyo alisema kuwa hakuna sababu ya watu kuanza kulaumiana hivi sasa na kinachoweza kufanyika ni kwa serikali kujipanga upya kukabiliana na mambo yanayoweza kutatuliwa.
"Yapo mambo yaliyo nje ya uwezo wa kibinadamu kwa mtu mmoja mmoja, hivyo lazima tuelewe, lakini si kulaumiana na kukashifiana, bali kutafuta namna ya kuondoka hapo," alisema askofu huyo.
Akitoa mfano alisema, miongoni mwa mambo ambayo hayawezi kurekebishwa kibinadamu kwa nguvu za mtu mmoja mmoja kama rais, kuwa ni kukithiri kwa upotofu wa kifikra (false assumption), matumizi mabaya ya rasilimali za taifa, ongezeko la kasi la watu na kufa kwa kilimo.
Hata hivyo, askofu huyo alionyesha kutoa lawama kwa viongozi wa juu serikalini na kusema kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni na taratibu ili kuboresha hali ya mambo.
"Hakuna sababu ya kulindana, hata kama ni mjomba wake, rais anapaswa kumwajibisha. Wote wanaoonekana kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo wanatakiwa kuwajibishwa. Kiongozi anatakiwa kuwa 'honest' (mkweli)," alisisitiza askofu huyo.
Profesa Leonard Shayo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ambaye pia ni mwanasiasa, alisema ni mapema mno kuihukumu serikali kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake katika kipindi cha miaka miwili.
Kwa mtazamo wa profesa huyo wa hesabu, watafiti wa REDET hawakupata muda wa kutosha kukusanya takwimu za kutosha, huku akisisitiza kuwa mwezi mmoja hautoshi kufanya utafiti wa nchi nzima.
"Binafsi sina imani na takwimu hizo. Katika kipindi cha mwezi mmoja ni vigumu kupata takwimu sahihi za kuelezea ufanisi wa serikali iliyoingia madarakani miaka miwili iliyopita.
"Kwanza nataka wananchi wafahamu kuwa matatizo mengi yaliyopo sasa ni matokeo ya serikali zilizopita… hivyo si haki kuwahukumu watendaji na mawaziri.
"Mfumo wa utendaji haujakaa sawa kurekebisha kasoro zilizopita… siamini kama hao REDET wapo 'unbiased' (sawa)," alisisitiza Profesa Shayo.
Aidha, msomi mwingine aliyepata nafasi ya kuzungumza na gazeti hili, Profesa Mwesiga Baregu, alisema sababu ya kuporomoka kwa umaarufu wa Rais Kikwete na serikali yake ni uwezo na umakini mdogo kiutendaji.
Alisema, rais ameshindwa kuchagua timu ya kufanya kazi, hivyo akamshauri kuharakisha mabadiliko ya serikali yake hususan Baraza la Mawaziri ili kwenda nao sambamba kiufanisi.
"Katika hili, naona rais anatakiwa kufikiria kwa umakini sana na ajipange upya, kwa sababu kweli yeye na serikali yake wamepoteza mwelekeo… Hebu tazama ndani ya miezi 12 wananchi, hasa wasomi wenye upeo wa kuchambua mambo wamemchoka.
"Siku hizi Watanzania wanaona mbali kuliko serikali, hasa katika rasilimali za taifa na ufisadi… huku uchumi ukizidi kuporomoka kila kukicha," alisema Profesa Baregu na kuongeza kuwa, Rais Kikwete anatakiwa kukubaliana na hali halisi ili kuleta mabadiliko.
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema ni jambo la hatari na lisilo la heri kwa umaarufu wa rais kuzidi ule wa serikali yake.
Alisema utendaji wa rais unatokana na ushauri unaotolewa kwake na Baraza la Mawaziri na hivyo inapotokea rais akaonekana kukubalika kuliko ilivyo kwa mawaziri wake, basi hizo ni dalili za kuwapo kwa tatizo kubwa katika mfumo wa utawala.
"Si jambo zuri hata kidogo umaarufu wa rais kuuzidi ule wa serikali yake. Kwa hakika hizi ni dalili za kuwapo kwa tatizo kubwa la kimfumo na ambalo rais anapaswa kuchukua hatua za makusudi kulimaliza," alisema Zitto.
Akizungumzia hatua hizo, Zitto alisema, Rais Kikwete anapaswa kuchukua hatua za kubadili mfumo wake wa kiutawala, kwa kurejea masuala muhimu ya kitaifa kama yale ya kufungua mjadala wa kitaifa wa katiba na kulimaliza tatizo la Zanzibar.
Kwa mujibu wa Zitto mbali ya hatua hizo, rais atapaswa kuhakikisha anaunda Baraza la Mawaziri jipya akishirikisha wanasiasa wenye ujuzi wa aina mbalimbali, ili kutoa changamoto katika utendaji kama njia ya kurejesha imani ambayo wananchi wameanza kuipoteza kwake na kwa serikali yake.
Kuhusu mawaziri, Zitto alisema upo uwezekano mkubwa kuwa makosa ya kiutendaji au kimaamuzi ya mawaziri wachache tu katika baraza zima yanaweza yakawa ndiyo chanzo cha imani ya wananchi kutokomea.
"Naamini ni utendaji mbovu wa mawaziri wachache tu ndio uliosababisha wananchi wapoteze imani kwa serikali. Ni wazi kwamba wako mawaziri wazuri na wenye uwezo ambao utendaji wao unafunikwa na makosa ya wachache miongoni mwao," alisema Zitto.
Akitoa mfano alisema kitendo cha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Profesa David Mwakyusa kwa mfano kushindwa kujiuzulu kutokana na makosa yaliyofanywa na madaktari wa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), hivi karibuni ni moja ya mambo yanayoipotezea imani serikali machoni mwa wananchi.
Mbunge mwingine kijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini alisema, matokeo hayo yanampa changamoto Rais Kikwete kufanya mabadiliko makubwa katika barazala lake sasa.
"Mimi nadhani huu ni wakati pekee kwa rais kulivunja Baraza la Mawaziri ambalo kimsingi limemwangusha. Kuna mawaziri wanatoa maamuzi ya ajabu na kuja kuyatengua siku chache baadaye, lakini wanaendelea kubakia serikalini. Huku ni kumuangusha rais," alisema mbunge huyo kijana.