MAHUJAJI wapatao 72, ambao walikuwa wafike Saudi Arabia kwa ajili ya ibada ya hija jana, wamekwama visiwani hapa baada ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kudaiwa kushindwa kuwasafirisha.
Meneja wa Kampuni ya Zanzibar Hajj Travelling Agency, Hassan Omar, alisema kuwa mipango yote ya safari ilikamilishwa mapema, lakini safari hiyo ilishindikana kutokana na ATCL kushindwa kuwasafirisha kwa wakati.
Omar alisema kuwa awali, ATCL liliwaarifu kuondoka na ndege ya kukodi kutoka nchini Dubai, lakini ulipofika wakati wa kuondoka, walitoa taarifa nyingine kuwa hakutakuwa na safari kutokana na ndege hiyo kuharibika.
Alisema kuwa hivi sasa shirika hilo limewaahidi kuwaletea ndege nyingine ya kukodi itokayo Saudi Arabia, ambayo itawachukua mahujaji wote 72.
Baadhi ya mahujaji hao, wamekuwa wakihangaika tangu walipopewa taarifa za kutokuwepo safari hiyo na baadhi yao walifika katika vyombo habari kulalamikia hatua hiyo.
Mkurugenzi wa zamani wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Maalim Kassim Suleiman, ni miongoni mwa mahujaji waliokwama kuondoka na alisema hawajui hatma ya safari yao licha ya kukamilisha taratibu zote.
"Kwa kweli kuchelewa kufika Makka kutatukosesha mambo mengi muhimu, kwani kabla ya kwenda mji mtakatifu wa Makka mahujaji hupelekwa kwanza katika mji wa Madina," alisema.
Hujaji mwingine, Burhani Msoma, alisema inashangaza kwa shirika hilo kufanya vituko kama hivyo.
"Nimezungumza na Sheikh Ally sasa hivi kwa simu, anasema hata wao mwaka jana walikwamishwa na shirika hili hili wakakaa wiki nzima hapa… lakini kwa nini?" alihoji kwa hasira.
Kwa mujibu wa taratibu za ibada hiyo, mahujaji wote walitakiwa kufika Saudi Arabia ifikapo Desemba 4 (juzi), kwa jili ya kuanza ibada mbalimbali, ikiwemo kuzuru Msikiti wa Mtume wa Madina.