WATU wanaoishi katika maeneo aghali jijini Dar es Salaam, sasa wataanza kuonja joto ya kukatiwa maji, katika kampeni mpya iliyoanzishwa na Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco).
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirika hilo, Alex Kaaya, aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana kuwa chini ya utaratibu mpya uliobuniwa na kampuni hiyo, maji sasa yatakuwa yakikatwa kwa maeneo na si kwa mteja mmoja mmoja kama ilivyozoeleka.
Kaaya alisema badala ya mteja mmoja mmoja, maji yatakatwa katika eneo lote ambalo wateja wake wamebainika kuwa sugu kwa kutolipa ankara zao.
Akifafanua, alisema kuwa Dawasco imelazimika kuchukua hatua hiyo ili kuiokoa na kifo kinachoinyemelea, kutokana na ukosefu wa fedha za kuendeshea shughuli zake, kunakosababishwa na wateja wake wengi kuwa sugu kulipa ankara zao licha ya kupatiwa huduma ya maji kwa kiwango cha kuridhisha.
“Tumebaini kuwa yapo maeneo ambayo wateja wamekuwa wakipata maji kwa wingi, lakini kinachosikitisha ni kuwa hawataki kilipia huduma hiyo. Pia yapo maeneo ambayo hayapati maji kwa wingi, lakini watu wapo tayari kulipia.
“Utaratibu tunaouanzisha hivi sasa utatuwezesha kukata maji katika maeneo ambayo wateja wake wamekuwa sugu kwa kutolipa ankara za maji ili tuweze kuwahudumia vizuri wateja ambao wapo tayari kulipa ankara zao,” alisema Kaaya.
Kaaya aliyaainisha maeneo ambayo licha ya kupata huduma ya maji kwa kiwango cha kuridhisha, wateja wake wamekuwa wagumu kulipia ankara zao kuwa ni pamoja na Mbezi Beach, Ada Estate, Regent Estate, Mikocheni, Masaki na Mwenge.
Alibainisha kuwa kwa kuanza, zoezi hilo la kukata huduma ya maji litaanza kwa maeneo ya Mbezi Beach na Masaki, ambako kuna jumla ya wateja 4,341.
Akifafanua, Kaaya alisema kuwa eneo la Masaki lina wateja 1,270 na limekuwa likipata maji kwa kiwango cha kuridhisha, lakini wateja ambao hadi hivi sasa hawadaiwi na shirika hilo ni asilimia tano tu ya wateja wote wanaopata maji.
Kwa upande wa Mbezi Beach, alisema kuwa kuna wateja 2,171 lakini wateja ambao wameshalipa ankara zao na hawadaiwa na Dawasco ni asilimia kumi tu.
Kutokana na hali hiyo, Kaaya alisema Dawasco imetoa notisi ya siku tatu kwa wateja wa maeneo hayo kuanzia leo, kuhakikisha kuwa wanalipa ankara zao na kufikia kiwango cha kuridhisha, la sivyo, maeneo hayo yatakatiwa huduma za maji baada ya muda huo.
“Tunawapa Jumatatu, Jumanne na Jumatano… hatuwezi kuendelea kuwapatia huduma asilimia 90 na 95 ya watu ambao hawalipii huduma hiyo ipasavyo,” alisema Kaaya na kubainisha kuwa hatua hiyo imechukuliwa baada ya utafiti wa muda mrefu.
Hata hivyo, Kaaya alisema kuwa kampuni hiyo imeandaa utaratibu ambao utahakikisha kuwa wateja ambao wanalipa ankara zao vizuri ambao wapo katika maeneo hayo, hawaathiriki na zoezi hilo.
“Hatuwezi kusema hivi sasa tutafanya nini, lakini ninawahakikishia wateja wetu wazuri kuwa hawataathirika… tunawafahamu na tunafahamu walipo,” alisisitiza.
Dawasco hutumia wastani wa sh bilioni 2.1 kwa mwezi kuzalisha na kusambaza maji kwa wateja wake wote katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wakati makusanyo kwa kipindi kama hicho yamekuwa ni wastani wa sh bilioni 1.7.
Kaaya alisema kuwa wakati hali ikiwa hivyo, wateja wa Mbezi Beach wanadaiwa na shirika hilo jumla ya sh milioni 578 wakati wale wa Masaki wanadaiwa sh milioni 574 na kufanya deni la jumla ya zaidi ya sh bilioni moja katika maeneo mawili tu.
“Tumeona sasa badala ya kuhangaika na mteja mmoja mmoja, twende kwa maeneo, wasiolipa watashughulikiwa kama eneo. Kwa nini tuendelee kuwapa maji wakati hawalipi?” alihoji Kaaya.
Alisema kuwa Dawasco inalazimika kuchukua hatua hiyo kwa sababu isipofanya hivyo, inaweza kushindwa kuendelea kutoa huduma zake ipasavyo.
Alisema kuwa madeni ambayo Dawasco inayazungumzia si ya zamani, ni ya kipindi cha miaka miwili na nusu ambayo kampuni hiyo imekuwepo.
“Tukiendelea namna hii shirika litakufa, lakini mimi ninapaswa kulisaidia lisife, liwe endelevu,” alibainisha na kusema kuwa iwapo wakazi wa maeneo haya wanataka kunusurika na kukatiwa huduma hiyo, wanapaswa kulipa madeni yao yote, lakini shirika linaweza kuwafikiria iwapo wataweza kulipa angalau theluthi mbili ya madeni hayo.
Alipoulizwa kuwa anapata wapi jeuri ya kuyakatia maji maeneo hayo ambayo yanaaminika na wengi kuwa yanakaliwa na watu wenye fedha, Kaaya alisema: “Wateja wetu sisi si watu wenye fedha… wateja wetu ni watu tunaowapatia huduma ya maji na wanatakiwa kuilipia huduma hiyo.”
Alisema kuwa tangu ashike wadhifa huo, hajawahi kufanya kazi na kisha kuingiliwa na mtu yeyote ingawa wakati fulani aliwahi kuulizwa maswali kutokana na hatua alizozichukua.
“Nilichukua hatua, nikaulizwa maswali na nikatoa majibu. Majibu niliyotoa yalikuwa ni ya kuridhisha na sikusumbuliwa tena,” alisema.
Alisema mpango wa kuyakatia maji maeneo ya Mbezi Beach na Masaki ni mwanzo tu kwani baada ya hapo watahamia kwenye maeneo mengine ambayo yamebainishwa kuwa ni sugu kwa kutolipa ankara.
Aliyataja maeneo ambayo yapo katika orodha ya zoezi hilo kuwa ni Ada Estate, lenye wateja 475 ambao deni lao limefikia sh milioni 527, Mikocheni lenye wateja 697 wanaodaiwa sh milioni 566, Mwenge ambako kuna wateja 733 waliojilimbikizia deni la jumla ya sh milioni 463 na Regent Estate, ambako wateja wake 222 wanadaiwa sh milioni 200.
Akizungumzia mpango wa shirika hilo kufunga mita kama zile za Luku katika umeme, Meneja wa Operesheni, Jackson Midala, alisema kuwa mpango huo bado haujakamilika na upo katika majaribio.
Akifafanua, alisema kuwa mita hizo zimefungwa kwa wateja 15 katika eneo la Namanga kwa majaribio, lakini matokeo yake si ya kuridhisha.
“Ni teknolojia mpya na kwa bahati mbaya watu tayari wameshaanza kuzichezea mita hizi kwa lengo la kutaka kulipa kidogo na kupata huduma kubwa.
“Pia tumebaini kuwa ili zifanye kazi sawasawa, tunahitaji kuufanyia marekebisho mfumo wetu na hivi sasa tunafanya mpango wa kuzungumza na wenzetu wa Windhoek Water Authority ambao wanautumia mfumo huu kwa asilimia 100,” alisema Midala.