Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Serikali yamtetea Zitto
Serikali yamtetea Zitto
By Marshy Abdu | Published  11/23/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Serikali yamtetea Zitto
na Ratifa Baranyikwa


IKIWA imebaki siku moja kabla ya Kamati Kuu ya Taifa ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutoa uamuzi wa iwapo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto ashiriki katika kamati ya kupitia mikataba ya madini au la, serikali imesema mbunge huyo ana kila sababu ya kushiriki.

Imesema kinachoangaliwa katika kamati hiyo si mtu, bali maudhui yaliyo ndani ya kamati hiyo.

Kauli hiyo ya serikali ilitolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Daniel Nsanzugwanko wakati alipotembelea ofisi za Kampuni ya Free Media inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari.

"Hoja si Zitto kuwemo kwenye kamati, hoja ni maudhui ya kamati, katika siasa mambo mengi yanaweza kuongelewa na hoja ya mtu 'individual' si hoja ya msingi sana… mtu hawi hoja, mtu anakuwa kama 'player', mkianza 'personality' hamfiki, hizo hoja zinazotolewa na kina Tundu Lissu au kina (Chacha) Wangwe ukiangalia ni hoja za kisiasa zaidi kuliko hoja za kimaudhui," alisema Nsanzugwanko.

Aidha, alisema kuwa yeye anaungana na hoja zilizotolewa na Bob Makani na muasisi wa CHADEMA, Edwin Mtei.

Katika maelezo yake siku kadhaa zilizopita, Mtei alisisitiza kuwa, hakuna sababu ya Zitto kujiondoa ndani ya kamati hiyo, na akasisitiza kuwa chama hicho kinapaswa kutumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yake serikalini.

Alionya kuwa ni vigumu kuendesha nchi kwa kususia, badala yake aliwataka walio kwenye makundi kutoa mawazo ndani ya kamati husika za chama kwa ujasiri na uwazi.

"Tangu tulipounda chama, tunaamini katika uwazi na ukweli, lakini 'view' zetu zinakuwa 'recorded', huwezi kurekodi kama tunasusa, ni vizuri kwamba Zitto amekubali kushiriki na kushawishi endapo mawazo yake yatakubalika, atakuwa 'ame- influence policy' ya nchi yetu na kama atapuuzwa, anaweza akatoa 'minority report'. Mchango wetu uwe ni wa kuchangia na si wa kususia," alisema Mtei.

Alisema: "Wanaosema kuna 'vested interest' ni lazima wajue kuwa masilahi ya kwanza ni nchi yetu… kama kuna mtu anaogopa 'views' zake zitakuwa 'influenced', hana msimamo."

Kuhusu hoja zilizotolewa na Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu kwamba hii ni kamati ya sita kuundwa na rais na kwamba kamati zilizopita hazijawahi kutoa ripoti yake hadharani, Nsanzugwanko amepinga kauli hiyo na kudai kuwa ripoti zilizopita zilitolewa bungeni na kuzifanyia majadiliano na kwamba kamati zilizopita hazifanani maudhui, kila kamati ina maudhui yake.

" Ripoti zipo, hata ukienda katika maktaba za Bunge utazikuta, mimi nakumbuka ripoti ya mwisho iliyotolewa na Kipokola bungeni tuliijadili kweli kweli bungeni," alisema na kuongeza:

"Hoja ya madini imekuwepo kwa muda mrefu na kwamba haimpendezi kila mtu hata rais mwenyewe, ndiyo maana ameunda hii kamati ambayo itatusaidia kisera."

Akirejea historia ya nyuma kuhusu suala hili, Naibu Waziri huyo alisema kuwa matatizo hayo yote yamesababishwa na sheria ya iliyoruhusu kuanzishwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kilichoanzishwa kwa lengo la kuvutia wawekezaji.

"…Ndiyo inayotoa nafuu za kodi, na kuruhusu wageni katika makampuni ya hapa ndani, sasa wawekezaji wameingia, wageni kibao wameajiriwa, tunafanya nini sasa? Je, TIC haihitaji mapitio?" alisema na kuhoji.

Wakati huohuo, Nsanzungwanko akiwa Naibu Waziri ambaye amepewa dhamana katika masuala ya habari, alisisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao, ikiwa ni pamoja na kuzifanyia tafiti taarifa wanazozipata kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya habari na kusema kuwa kwa kuzingatia hayo, vyombo vya habari vitaheshimika.

Alisema kuwa bila kuangalia chombo hiki kinamilikiwa na nani, kikubwa cha kuzingatia ni kile kinachoandikwa kikiwa na maslai ya jamii kwa ujumla, chenye kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Aidha, Nsanzugwanko alisisitiza vyombo vya habari kulinda na kuheshimu haki za watoto na wanawake, hasa kwa upande wa luninga, kutoonesha picha za vitisho na zile zisizofaa kimaadili kwa watoto.

Awali, akimkaribisha Naibu Waziri huyo, Mhariri Mkuu wa magazeti ya Tanzania Daima na Sayari, Absalom Kibanda, alisema kikubwa kinachoangaliwa na magazeti anayoyaongoza ni maslahi ya taifa.

"Msimamo wetu ni katika kuangalia utaifa, msimamo huo katika gazeti hili (Tanzania Daima) ni mkubwa sana, tuko tayari kukosolewa, tuko tayari kuweka mbele maslahi ya taifa hili," alisema.

Aidha Meneja Matangazo wa magazeti hayo, Twalib Mungulu, alisema changamoto kubwa wanayokabiliwa nayo ni pamoja na uchache wa matangazo ambayo ni muhimili mkubwa wa uendeshaji wa vyombo vya habari.

"Sisi hatuna ruzuku tunayopata sehemu yeyote na muhimili mkubwa ni matangazo, kwa upande wa serikali, imekuwa 'haitu-support' sana," alisema.

Akijibu hilo, Naibu Waziri huyo alikiri kuwa gazeti hili linasomwa na watu wengi, na serikali imekuwa ikijifunza baadhi ya mambo kupitia gazeti la Tanzania Daima. Alisema kuhusu suala la kunyimwa matangazo analifahamu na kuahidi kuleta mabadiliko.

"Hilo suala mimi nalifahamu, najua chimbuko lake kulikuwa na hisia nyingi kuhusu gazeti hili, mambo yatabadilika," alisema.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.