Kama zisemavyo takwimu nyingi zinazoelezea masuala ya Ukimwi, kundi linalodaiwa kuathirika zaidi ni kundi la vijana kati ya umri wa miaka 16 hadi 40 kote nchini, hii ni kutokana na kwamba vijana ndio walioko katika changamoto kubwa zaidi za mabadiliko ya kibaiolojia pamoja na kijamii pia.
Kila siku vijana wana pata hamu ya kujifunza mambo mbalimbali yakiwemo yanayohusisha ngono sambamba na yale yanayoonesha utashi na mwelekeo wao wa hamu ya mafanikio katika maisha yao.
Vijana wengi hasa wale walioko mashuleni kuanzia darasa la tano hadi la saba kwa shule za msingi na wale wa kidato cha kwanza hadi kidato cha nne kwa shule za sekondari ndiyo ambao kila kukicha wanaingia katika ushindani wa kila aina wa kimaisha.
Wanafunzi hao wanazo tamaa mbalimbali ampapo wanatamani ama kuwa kama Fulani kimavazi na wengine kimaendeleo ya kielimu wakati wengine wanahitaji sana kufanana na watumishi Fulani wa mashirika au serikali ambao wanamiliki magari, simu za bei kubwa na fedha za kutosha mfukoni.
Ni kwa sababu hizo na nyingine nyingi watoto wengi wa shule za msingi na sekondari wilayani Kasulu wanaonekana wakirandaranda mitaani wakiwa na wapenzi wao, sambamba na wengi wao kubainika kuwa na mimba zinazopelekea ama waache shule wenyewe au kufukuzwa pindi tu wanapobainika.
Katika shule za msingi mfano Bogwe, Mwenge, Murubona na nyingine zilizoko katika mji wa Kasulu si ajabu kukutana na mwanafunzi wa darasa la tano au sita na la saba kumkuta akimiliki Simu ya bei kubwa wakati walimu wanaomfundisha wakimiliki simu ya bei ndogo sana au wengine kutokuwa nazo kabisa.
Na ni katika shule nyingi kama hizo matukio ya wasichana kuwa na ujauzito ni mengi ambayo yanaripotiwa kwa idara husika na mengine mengi huishia mikononi mwa wazazi, walimu wakuu na watendaji wa vijiji na hata wa kata ambao ama hushiriki vitendo vya utoaji mimba au msichana mwenyewe kumaliza tatizo bila kuwashirikisha wazazi wake.
Katika kipindi cha januari hadi October mwaka huu jumla ya wasichana 8 walipata mimba na kati yao sita hawakufanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba kutokana na ujauzito wao, jambo hili linasikitisha sana, mwelekeo wa maisha yao ndio ulikomea hapo, lah vinginevyo wajiunge na MMEMKWA kunusuru mwelekeo wao.
Hadi sasa wasichana wawili wa shule ya msingi Nyumbwe darasa la Sita ni wajawazito hali inayopelekea ama kutokana na maumbile yao waogope kwenda shule au kufukuzwa na walimu wakuu, kwaani kupata ujauzito in aibu kwa shule husika.
Kinachosikitisha kama nililvyosema hapo juu, takwimu hizi si sahihi hata kidogo, kwani taarifa za uwepo wa wasichana wenye mimba katika shule za msingi ni nyingi kuliko zinavyoripotiwa na ofisi ya elimu, inaonekana dhahiri kuwa, walimu wakuu na watendaji kwa kushirikiana na wazazi wa pande zote mbili huficha taarifa za matukio mabaya kama hiyo.
Zipo shule za msingi kama vile Shunga, Bobwe na Makere ambazo mwandishi wa makala alibaini kuwa wapo wanafunzi kadhaa ambao wana ujauzito, mfano, Wanafunzi wawili wa shule ya msingi Makere wilayani Kasulu wamesitisha masomo yao baada ya kubainika kuwa wajawazito.
Mwenyekiti wa kijiji cha Makere Bw. Ngurubhe Denis amebainisha amebainisha kuwa mmoja kati ya wanafunzi hao ni miongoni mwa waliotakiwa kumaliza darasa la saba wakati mwenzake alikuwa adarasa la sita.
Bw. Ngurube amesisitiza kuwa serikali ya kijiji ilipata taarifa kutoka kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo kuwa wanafunzi hao hawahudhurii shuleni bila taarifa na kwamba ipo haja ya kuwahoji wazazi.
Amebainisha kuwa wazazi wa wasichana hao pamoja na watoto wao waliitishwa kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ambapo waliwataka wawataje wanaohusika na mimba lakini wasichana hao hawakuwa tayari kuwataja.
Hata hivyo habari kutoka katika kijiji cha makere zinadai kuwa mmoja kati ya wanafunzi hao amepata mimba kutoka kwa shemeji yake na kwamba wazazi wanaficha siri kuepuka aibu.
Vitendo vya uhuni na ngono kwa wanafunzi haviishii katika shule za sekondari pekee, vipo hadi kndani ya shule za sekondari na inadaiwa na wachunguzi wa mambo kuwa huko ndio shina kuu la utovu wa nidhamu na ngono horela miongoni mwa wanafunzi wenyewe pamoja na walimu wao pia.
Katika shule ya sekondari Kasangezi msichana mmoja alilazimika kuendelea na masomo huku akiwa mjamzito baada ya kutolewa kwa mumewe alikokuwa ameolewa mara tu baada ya kumaliza darasa la saba kabla ya matokeo yake kutoka na kukutwa amefaulu, na sasa ameripotiwa kushindwa kuendelea na masomo yake.
Katika shule ya sekondari ya Muayama nako hali ni hiyo hiyo, jumla ya wanafunzi 6 wanaripotiwa kukwama kimasomo kutokana na kufanya ngono isiyo salama na hatimae kupata ujauzito uyliopelekea wasitishe masomo yao.
Mkuu wa shule hiyo mwalimu Juckson Marila alithibitisha hayo wakati wa mahafali ya kidato cha nne mwaka huu, alibainisha kuwepo kwa wanafunzi hao wanaopata ujauzito na kwamba wawili miongoni mwao wanaendelea na masomo baada ya kujifungua.
Maeneo ya burudani hususani Disko na vilabu vya pombe mjini Kasulu si ajabu, bali ni kawaida kabisa kukutana na msichana wa shule akiwa na baba mtu mzima kabisa na wakati mwingine walimu wao wakivinjali kwa pombe na nyama choma na hata wakati mwingine wakicheza muziki pamoja bila hofu wala wasiwasi wa kimaadili.
Kumbi za muziki kama vile FM, Night Club na hata ukumbi wa kituo cha vijana idara ya utamaduni kila ifikapo mwisho wa wiki kwao ni mavuno, hili si tatizo kubwa kama wanaingiza kipato na kulipa kodi na ushuru mbalimbali kwa halmashauri yetu, ni suala la kupambana na umasikini kupitia burudani.
Lakini tujiulize hivi ni lazima wateja wakuu wa kumbi hizo wawe wanafunzi tena wa sekondari na shule za msingi, ndio tujiridhishe kuwa sasa mambo ni shwali kibiashara bila kujali maadili ya utamaduni wetu wa mkoa wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla?
Wengi watasema ni Uongo labda watakaopinga kauli hii ni wale ambao ama hawaoni tatizo kwa kuwa nao ni sehemu ya haya, au wale ambao hata wanapoyaona hawaoni kuwa ni chanzo cha kuporomoka kwa maadili na hatimae kuongezeka kwa virusi vya ukimwi –VVU.
Wajumbe wa kamati ya maendeleo ya kata ya Kasulu mjini waliwahi kulalamikia sana kuwepo kwa kumbi za muziki na video mjni zisizozingatia maadili ya jamii, na kuchambua sababu za kuwepo kwa watoto wengi wanaotembea nusu uchi (kuvaa nguo zinazoonesha maumbile yao) nyakati za mwisho wa wiki ama hata wawapo mashuleni, wote walirushia mziko huo kwa serikali, je! Katika hili la uvaaji mbaya ni serikali ilaumiwe pia? Ni nani aliwawezesha watoto hao kupata mavazi hayo kama si wazazi?
Nitakuwa nimekosea sana kusema kuwa vituko hivi vya watoto wa shule viko mjini tu, lah hasha, hata vijijini dhambi hii imeenea, kijiji kama Manyovu, Kilombero, Kabanga, Makere, Kasangezi na hata Shunga ambapo wanafunzi walioana na mwingine kupachikwa mimba na mwenzake wa sekondari ya TAPA na kukatishiwa masomo akiwa darasala sita.
Shule za sekondari za Bogwe, Ishimwe, TAPA (Kasulu Sekondari) Buseko Hill, na nyingine wanafunzi wake ni usanii mtupu,hadi sasa shuleni Bogwe kunaripotiowa kuwepo kwa wanafunzi wawili waliobainika na ujauzito licha ya watoto hao kuishia kushindana kwa mavazi tena si mavazi yenye akili, yapo yale ya sijui huyaita “Shumileta” na mengine mengi, istoshe hata sare zao za shule huvaliwa kwa mtindo wa kuwaacha (mapaja) kwa nyuma yakiwa nje (uchi).
Katika mazingira kama haya ni dhahiri kuwa elimu ya ukimwi inayotolewa haitoshi ama haieleweki vema kwa watoto wetu kiasi kwamba tishio la kuwepo kwa UKIMWI na kwamba unaua watu wengi haliwapati vijana mashuleni kikamilifu.
Endapo watoto hawa wenye damu moto, wanaotamani kujifunza na kutenda kila jambo wangepelekewa takwimu ya Uambukizo wa magonjwa hayo shuleni, ni dhahiri kuwa kila mmoja wao angeogopa kama si kuacha tabia mabaya na kuanza kuunda mwelekeo mpya kimasomo na kimaadili.
Mfano, hospitali na vituo vya ushauri nasaha, vipatiwe fursa ya kupeleka taarifa zao mashuleni, hususani darasa la nne hadi kidato cha nne, takwimu hizo zioneshe hali ya uambukizo kwa wanafunzi wa shule husika (kama zipo) au hata za shule nyingine, vijana watashtuka.
Chama cha msalaba mwekundu Tanzania chini ya ufadhili wa Chama cha msalaba mwekundu cha marekani kimekuwa kikitoa mafunzo makubwa sana ya UKIMWI kupitia mradi wake wa pamoja tunaweza wamekuwa wakitoa mafunzo mashuleni lakini nadhani ujumbe bado haujawaingia wanafunzi wengi kulingana na wanayoendelea kutenda wawapo ndani na nje ya shule.
Kwa kuwa vijana hawa wanapenda kuiga na kujifunza kila tendo, basi wawezeshwe kujua hali ya maambukizi kwa vijana, watoto na watu wazima katika maeneo yao, naamini watajifunzajambo kuliko ilivyo katika nadharia ya maneno kutoka kwa wawezeshaji wa masuala ya ukimwi na kubadili tabia.
Mwisho wazazi tuwe macho na wakali kwa tabia za watoto wetu, tusiishie kuona watoto wetu wakibadilika kimaumbele na kujipatia mavazi mapya, simu za mkononi na vipodozi bila kujiuliza wamevitoa wapi, hii ni aibu kwetu.
Sikatai watoto kupata maendeleo ya kimaumbile na kiuchumi, hoja yangu ni je maendeleo hayo yametokana na nini? Hii ndiyo hoja kuu, fikiria mzazi umempeleka motto wako Bogwe au TAPA au hata Ishimwe sekondari, Ada tu inakushinda unalipa kwa kusua sua, harafu mwanao huyo anamiliki simu ya shilingi laki mbili, hivi halii hii inaingia akilini? Hujui kama labda amefanya ukahaba au ujambazi na kujipatia pesa za kununulia mavazi na vitu vingine vya thamani?
Wazazi tuache tabia ya kusema eti watoto wa siku hizi wametushinda, wakati sisi wenyewe tumeshindikana, tusirushe mzigo wa dhambi ya malezi mabovi kwa serikali, ebu tutimize wajibu wetu ndipo tuitake serikali isaidie tu pale ambapo msaada wa kitaifa unahitajika, si kuwaacha watoto wanarandaranda harafu tuitake serikali iwatunze, wewe mzazi uko wapi, na je kazi yako kwa mwanao ni nini?. Si kuzaa tu, hapana, lazima tuwajibike kwa maisha bora ya watoto wetu vinginevyo tuaambulia misiba itokanayo na ukimwi au kulea wajukuu tusio jua wazazi wao kwa ufasaha, nii ni aibu.