Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Mapinduzi CCM
http://www.habaritanzania.com/articles/4229/1/Mapinduzi-CCM
By Marshy Abdu
Published on 11/7/2007
 
HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana ilifanya mabadiliko makubwa kwa nafasi za watendaji wakuu wa ndani ya chama hicho.

Mapinduzi CCM
Sumaye, Wasira, Kusila waangushwa
na Absalom Kibanda na Martin Malera, Dodoma


HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana ilifanya mabadiliko makubwa kwa nafasi za watendaji wakuu wa ndani ya chama hicho.

Tukio kubwa katika mabadiliko hayo ambayo yaliingiza sura mpya ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho (CC) na sekretarieti yake, ni lile la kuanguka kwa kada wa siku nyingi wa chama hicho, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye pia anatajwa kuwa mtu aliyekuwa nguzo kuu ya kisiasa ya Rais Jakaya Kikwete.

Kwa wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa nchini, kuanguka kwa Kingunge katika kinyang’anyiro cha Kamati Kuu, hata baada ya jina lake kuwa miongoni mwa majina 15 ya Watanzania Bara waliokuwa wamependekezwa na Rais Kikwete kugombea nafasi saba, kunaweza kukawa na tafsiri moja ya haraka haraka kwamba, zama za bingwa huyo wa propaganda za kisoshalisti ndani ya chama hicho zimekwisha.

Kukosekana kwa Kingunge ndani ya Kamati Kuu, mtu ambaye amekuwa mmoja wa watendaji madhubuti wa CCM kwa miaka mingi, akianza kuwapo ndani ya sekretarieti enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza, kunaweza kukamfanya ajikute akipwaya kutekeleza ipasavyo majukumu yake ya kiserikali akiwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Jamii.

Mwanasiasa huyo anafikwa na zahama hiyo siku chache tu baada ya watu mbalimbali kumwandama kutokana na kutoa kauli zenye utata za kuibeba serikali kwa hoja nyepesi za kuwaponda wapinzani kuhusu masuala kadhaa ya kitaifa, yakiwamo yale yanayohusu hali ya kisiasa Zanzibar na baadaye taarifa za ufisadi ndani ya serikali.

Viongozi kadhaa wa juu wa vyama vya CUF na Chadema waliozungumza na gazeti hili kwa simu jana, waliielezea hatua ya Kingunge kuanguka kuwa moja ya matukio muhimu kabisa katika maendeleo ya siasa za Tanzania.

Mbali ya tukio hilo, jambo jingine linaloweza kugusa hisia za wadadisi wa mambo wanaofuatilia mwenendo wa kisiasa nchini, ni kuondolewa kwa aliyekuwa Mweka Hazina wa Taifa wa chama hicho, Rostam Aziz na nafasi yake kuchukuliwa na kada kijana na kiongozi wa muda mrefu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM), Amos Makala.

Tukio la kuondolewa kwa Rostam Aziz, mwanamtandao nambari moja, mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa na mmoja wa marafiki wa karibu wa Rais Kikwete kutoka katika sekretarieti ya chama hicho, ndiko ambako kunaweza kukawa gumzo la kisiasa katika siku zijazo.

Hata hivyo, pamoja na kutoka katika sekretarieti, Rostam mmoja wa vijana wa CCM wenye upeo mkubwa wa kuona mambo, anabakia kuwa mwanasiasa mwenye nguvu kutokana na kuendelea kubaki kuwa mjumbe wa Kamati Kuu, baada ya jina lake kushinda kutokana na pendekezo la Rais Jakaya Kikwete.

Kutokana na mchakato huo wa NEC, wana CCM wengine waliofanikiwa kupenya katika CC ni pamoja na Andrew Chenge ambaye katika hali isiyotarajiwa anaonekana kujipatia umaarufu mkubwa ndani ya chama hicho tawala.

Chenge ambaye ameingia katika Baraza la Mawaziri kwa mara ya kwanza safari hii, baada ya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, ni mmoja wa mawaziri ambao wamekuwa karibu kikazi na Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Katika matokeo ya juzi ya kinyang’anyiro cha ujumbe wa NEC, Chenge ndiye aliyeshika nafasi ya pili kwa wingi wa kura akiwa nyuma ya Lowassa na juu ya Katibu Mkuu wa CCM Yussuf Makamba ambaye yeye ameendelea kushikilia wadhifa wake huo, hata baada ya kuwapo kwa tetesi kuwa angeondolewa.

Hata hivyo, wakati Makamba akibaki, wasaidizi wake wakuu wawili, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Jaka Mwambi na Katibu wa Uenezi na Uhamasishaji, Aggrey Mwanri nao majina yao hayakupendekezwa na Rais KIkwete kuingia katika Kamati Kuu na baadaye wakapoteza nafasi zao hizo zilizokuwa zikiwaingiza moja kwa moja CC.

Kwa upande wa Zanzibar, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Saleh Ramadhan Ferouz yeye anaendelea na wadhifa wake huo ambao kimsingi unamfanya aendelee kuwa mjumbe wa CC na sekretarieti.

Kutokana na kuondoka kwa wanasiasa hao wawili katika sekretarieti (Mwambi na Mwanri), Kapteni George Mkuchika ndiye aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wakati John Chiligati akiteuliwa kuwa Katibu wa Uenezi.

Habari ambazo haziwezi kuthibitishwa kwa haraka zinaeleza kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa wanasiasa hao wawili; Mwambi na Mwanri, kuingia katika Baraza la Mawaziri la Kikwete linalotarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa.

Aidha, baadhi ya wadadisi wa mambo wanampa pia Rostam ambaye kitaaluma ni mchumi, nafasi ya kuingia katika baraza hilo jipya la mawaziri akiwa na nafasi kubwa ya kuongoza Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ambayo sasa inashikiliwa na mwanasiasa wa siku nyingi, Basil Mramba.

Wana CCM wengine ambao wamefanikiwa kuwa wajumbe wa Kamati Kuu wakitokea Tanzania Bara ni Pindi Chana, Dk. Abdallah Kigoda, Abdulrahman Kinana, Anna Makinda na Zakia Meghji.

Aidha, mwanasiasa mwingine mgeni ndani ya Kamati Kuu hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anayeongoza Idara ya Mambo ya Nje katika sekretarieti.

Kutoka Zanzibar waliongia katika Kamati Kuu ni Dk. Maua Daftari, Mohammed Gharib Bilal, Muhammed Seif Khatib, Omar Yussuf Mzee, Fatma Said Ali, Yussuf Mohammed Yussuf na Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wa Tanzania Bara, wanasiasa wenye majina makubwa waliopendekezwa na Rais Kikwete kuingia katika Kamati Kuu na majina yao kutupwa kwa kura, ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Stephen Wasira, Mizengo Pinda, Rehema Nchimbi, Kingunge, John Guninita, Adam Kimbisa na Stephen Kusila.

Aidha akitumia uwezo wake wa kikatiba (ndani ya CCM), Rais Kikwete aliwateua mawaziri wakuu wawili wastaafu, David Cleopa Msuya na Dk. Salim Ahmed Salim kuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu.

Kwa sababu zisizo bayana, Rais Kikwete safari hii hakulipendekeza jina la Dk. Salim mmoja wa wanasiasa wenye majina makubwa kuwa miongoni mwa watu ambao angependa waingie katika Kamati Kuu kama alivyofanya miaka miwili iliyopita.

Kwa upande wa Zanzibart wanasiasa waliopendekezwa na wakakosa nafasi za ujumbe wa Kamati Kuu ni Mwajuma Majid Abdallah, Ali Mzee Ali, Machano Othuman Said, Salim Hamad Salehe, Ussi Yahya Haji, Haruna Ali Suleiman na Hamad Masaun Yusuf.

Mjumbe mwingine wa sekretarieti aliyebaki ni Kidawa Hamid Salehe anayeendelea kuwa Mkuu wa Idara ya Mipango na Uendeshaji huku wale wa zamani wakiwamo, Halima Mamuya na Cosmas Hinju wakiwekwa kando na hivyo kuifanya sekretarieti mpya ikiwa na watu saba badala ya 10 kama ilivyokuwa awali.

Wajumbe wa Kamati Kuu iliyopita ilikuwa inaundwa na Rais Jakaya Kikwete, Amani Abeid Karume, John Samwel Malecela, Edward Lowassa, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Shein, Yusuph Makamba, Jack Mwambi, Saleh Ramadhan Ferouz, Samwel Sitta, Pandu Ameir Kificho, Ali Hassan Mwinyi, Rashid Kawawa, Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour, Kingunge Ngombare- Mwiru, Abdulrahman Kinana, Salim Ahamed Salim, Anna Abdallah, Abiud Maregesi, Emmanuel Nchimbi, Rostam Aziz, Aggrey Mwanri, Kidawa Hamid Salehe, Ali Ameir Mohamed, Muhammed Sif Khatib, Samia Suluhu Hassan na Pinda Chana.