LICHA ya kushinikiza uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini, safari hii viongozi wa dini ya Kiislamu wameibuka na madai mengine, wakitaka serikali ikomeshe mahusiano yake na Vatican.
Wakizungumza katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jana, viongozi hao waliitaka serikali kufuta mara moja Ubalozi wa Vatican nchini, kwa madai kuwa upo kwa ajili ya Wakristo pekee.
Viongozi hao waliojitambulisha kuwa ni kutoka madhehebu yote yanayounda dini hiyo, walifika MAELEZO na kuzungumza na waandishi wa habari wakiongozwa na Sheikh Mohamed Idd Mohamed wa Msikiti wa Mnyamani, Buguruni.
Sheikh huyo, ambaye alitajwa pia kuwa ni katibu wa kikao cha viongozi wote wa taasisi na dini ya Kiislamu, ndiye aliyesoma tamko kwa niaba ya Mwenyekiti wa kikao kilichoandaa tamko hilo, Alhajj Abbas Sykes.
Katika tamko hilo, viongozi hao walisema kuwa viongozi wa dini ya Kiislamu, maimamu, masheikh na viongozi wa taasisi mbalimbali walikaa kwa pamoja na kujadili mambo mengi yanayohusu dini hiyo.
Katika mkutano huo waliazimia kwa pamoja kutoa tamko la kulikumbusha Bunge na kulitaka lipitie muswada uliowasilishwa na kamati mbili za Katiba na Sheria na kutoa maamuzi yaliyoanishwa.
Pia walikishauri Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuvunja ukimya na kitoe tamko la wazi la kutekelezwa au kutotekelezwa ahadi yake iliyomo katika ibara 108 ya Ilani yake ya uchaguzi kuhusu urejeshwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini.
Akitangaza maamuzi mengine yaliyofikiwa katika kikao hicho, Sheikh Mohamed alisema kuwa viongozi hao waliafikiana kufungua kesi dhidi ya Mchungaji Christopher Mtikila, kutokana na matamshi yake yanayoukashfu Uislamu.
Alisema mipango ya kufunguliwa kwa kesi hiyo inakamilishwa kabla kesi yenyewe haijafunguliwa hivi karibuni.
Pia walitumia fursa hiyo kumkumbusha Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Mchungaji Mtikila, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), kwa kutumia jukwaa la siasa kushambulia dini.
Walimkumbusha pia Rais Jakaya Kikwete kufuta mkataba wa serikali na makanisa kwani itakuwa inakiuka uadilifu, pia walimwomba aufute kwa kuwa una upendeleo wa dini moja dhidi ya dini nyingine.
Pia walimkumbusha rais kuvunja mahusiano kati ya serikali na Ubalozi wa Vatican nchini kwa kuwa Tanzania haifuati dini, kwa hiyo uhusiano wa kibalozi kati ya serikali na Vatican ni kinyume cha katiba ya nchi.
Pamoja na kuitaka serikali kusitisha uhusiano na Vatican, viongozi hao walisema kuwa wanaipinga ziara ya Papa Benedict XVI, aliyepanga kuitembelea Tanzania kutokana na mwaliko wa Rais Kikwete.
Walisema wanaipinga ziara hiyo kutokana na huko nyuma kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki kutoa matamshi ambayo yalielezewa kuwa kashfa kwa Uislamu na Mtume Muhammad (SAW).