Wakati wa udogo safu hii ilizoea kuwasikia wazazi wakiongelea habari za TANU. Walikumbushana ahadi za mwana-TANU na miiko ya uongozi uzalendo na maendeleo ya jamii. Waliongelea ufugaji bora huku wakirejea na magazeti maarufu kama ukulima na ufagaji wa kisasa.
Kila nyumba angalau ilionja raha ya siasa za wakati ule huku picha ya Mwalimu Nyerere ikionekana kila ukuta. Leo hii imebakia kuwa historia.
Zama zile nilizoea kuona mbunge na gari lake la gongo la chura, au vox wagon, kama ilivyokuwa ikiitwa. Wengine walikwenda mbali hata kuliita kaa au kombi mradi ilieleweka. Nilizoea kuona gari la mbunge likisafirisha wagonjwa kwenda zahanati huku mbunge akisimamisha gari lake mara kwa mara kuwasalimia wananchi hata kuwapa lifti.
Hakika hii imebakia kuwa historia baada ya kupata wabunge wabuge na matajiri wa kutupwa wanaojihudumia migongoni mwa jamii maskini.
Wakati ule ubunge ulikuwa ni uongozi utokanao na watu na kwa ajili ya watu. Maana wakati wa uchaguzi kwa kumbukumbu. watu wawili wanachama wa TANU wenye sifa safi walishindana kwa kutumia alama ima ya jembe na nyuma, kuku na yai na nyingine kama hizo huku wakizunguka jimbo zima kuhutubia mikutano na kujibu maswali bila uongo na mizengwe.
Leo hii kadhali haya ni historia.
Zamani viongozi walikuwa viongozi tena wakitokana na kufanana na wale waliowaongoza. Wabunge walikuwa wakitumwa na wapiga kura wao kwenda bungeni kuwasemea siyo kujisemea kama sasa. Walikuwa wakitoa taarifa kila baada ya kikao cha bunge na siyo kuishia Dar es salaam kwenye miradi yao.
Zamani wabunge waliwafuata wananchi na siyo wananchi kuwavizia bungeni kama sasa. Hata walipokutana na wananchi wao hawakuwa na haja ya kuita wapiga picha kama sasa. Uongozi ulikuwa uongozi siyo uongo wala kutafuta umaarufu wa bei nafuu.
Zamani rais alikuwa mtu na heshima zake akizunguka mikoani mara kwa mara kukagua maendeleo na kutoa maelekezo siyo sawa na sasa ambapo rais anatumia muda mwingi ziarani ughaibuni.
Zamani hata serikali iliundwa na watu wenye ujuzi na uzalendo siyo ushikaji wala ukubwa wa mfuko wa mtu au udugu na uana-mtandao.
Huwezi kuamini yanayoendelea leo. Watu wanajikomba wapewe vyeo.
Safu hii leo itaongelea rushwa kwa waandishi wa habari wakubwa na wadogo. Siyo siri kuwa kama kuna mtoa rushwa mkuu kwa wandishi wa habari si mwingine bali mwenye habari ambaye kwa nchi yetu ni serikali. Bado kuna kumbukumbu za waziri mmoja kwenye awamu ya tatu aliyepaswa kufukuzwa kazi kwa kutoa bahasha.
Bahati mbaya kutokana na siasa na vyeo vya kulindana, mtoa rushwa huyu hadi leo anatesa kwenye serikali ya awamu ya nne! Aibu iliyoje!
Siyo uzushi wala wivu wa kike, wala wa kiume, kusema: kuna mtu au taasisi ya kupambana nayo kuhusu rushwa kwa waandishi wa habari ambayo imeua taaluma si mwingine bali serikali na viongozi wake.
Tutafakari. Kwa mfano, waandishi waandamizi waliopewa vyeo serikalini ni kwa sababu gani kama siyo rushwa ambayo ni kulipa fadhila kwa kuuhadaa umma kupitisha watu wasiofaa?
Hata kama vyeo walivyopewa ni vikubwa hata vitengo kwenye idara za serikali, ukweli unabaki pale pale: hawa ni wala rushwa. Hakuna jina jingine wanalostahiki kupewa.
Kila siku tunaona watu wasio na historia ya kisiasa wala kuwa wana harakati, zaidi ya kutumia kalamu na vyombo vyao vya habari kuwanufaisha wanasiasa, wakiteuliwa kwenye nyadhifa serikalini.
Wapo wanaojikomba hadi inatia kinyaa. Wanasahau taaluma zao hata utu wao ilmradi wapewe rushwa ya vyeo! Wapo wanajulikana na wanaowalipa fadhila hata kama wanaitwa waheshimiwa. Ajabu ni wala na watoa rushwa hawa hawa wanaotuaminisha kuwa wanaweza kuongoza vita dhidi ya rushwa wakati rushwa ni wao na wao ni rushwa!
Serikali kwa kuwatumia mamluki wake imefikia hata kununua vyombo vya habari! Walioviuza na kujiuza kwa serikali utaona mmoja mmoja akiibuliwa na kupewa cheo hata asichokiweza! Yote hii juu ya nini? Kulipa fadhila na kujenga mazingira kwa watu wabovu kuselelea uongozini wakati hawafai hata kuongoza familia zao.
Bahati mbaya tuna ugonjwa wa makengeza wa kuwaangalia wadogo na kujifanya hatuwaoni wakubwa. Hivi kati ya waandishi wadogo wanaohangaika kutafuta pesa ya nauli na mkate "mshiko" na hawa wanaohongwa vyeo serikalini wakati hawafai wakilipwa pesa ya kodi yetu ni nani wa kushughulikia kwanza?
Tusiangalie rushwa ya kwenye bahasha tu. Tuangalia na rushwa ya madaraka au vyeo. Tangu kumalizika kwa uchaguzi na kuingia kwa serikali ya awamu ya nne, tumeshuhudia waandishi wengi wakijitokeza kama wanachama wa CCM. Je hawa wanaweza kuvitendea haki vyama vya upinzani au kufichua uovu unaofanywa na wanaowafuga?
Je kwa kuvichafua vyombo vya habari ambavyo ndiyo jicho na mdomo wa wananchi (voice of voiceless and eye of eyeless), mapambano dhidi ya rushwa siyo kiini macho? Je wala rushwa hawa wanaowahonga waandishi vyeo nyuma ya pazia huku mbele wakijinadi kama makamanda wa kupambana na rushwa siyo wanafiki wa kutupwa?
Tuulizane wewe cheo chako umekipataje wakati hukuwa na muda hata na siasa zaidi ya kujitokeza wakati wa kampeni? Kama ulikuwa mkereketwa ukificha uanachama chako, je katika majukumu yako hukukipendelea chama chako ukiviumiza vyama vingine? Polisi, wanajeshi, majaji nao wakiwa na upofu kama huu kweli nchi yetu itafika? Tunamkomoa nani iwapo tunazaa ambao wataishi baada ya sisi kutoweka?
Mtu huyu aliyepata cheo kwa rushwa anaweza kuwaambia walioko chini yake wasijihusishwe na rushwa wakati wanamjua wazi kuwa ni tunda la rushwa? Mkuu wa wilaya au mkoa aliyeupata ukuu kirushwa anaweza kuing’aoa rushwa wilayani au mkoani mwake wakati yeye ndiye rushwa yenyewe? Kama akiweza ima awe mwendawazimu au afanye hivyo bila kujua.
Uroho wa madaraka yapatikanayo kwa rushwa yametujazia majambazi, matapeli, wala rushwa hata vyangudoa kwenye ofisi za umma! Anayebishia hili aanze kuzisoma historia za watendaji wetu katika eneo lake iwe la kuishi au la kazi. wilayani angalia mkuu wako wa wilaya. Wizara au idarani angalia bosi wako mwenye kutokea kwenye vyombo vya habari.
Anayebisha hili aangalie misheni tauni wanaotanua kwenye ofisi ziwe za vyama au serikali. Aangalie vyangudoa waliotoa rushwa za ngono na kupata ajira. Hawapo hawa? Kama hawapo rushwa ya ngono inayolalamikiwa kila uchao anatoa nani na kupokea nani akimuajiri au kuajiriwa wapi kama siyo taasisi zinazoendeshwa kwa kodi zetu?
Hata kwenye wale waliopewa nyumba zetu utakuta waandishi wamo. Wamo hata wanaotumwa kwenye balozi zetu nje wakafanye kazi za ukuadi! Hawa mafisi na mafisi mbweha kwenye siasa wataifikisha nchi yetu pabaya.
Kwani hatujuani? Kwanini mtu anayejulikana kwa uovu wa miaka nenda rudi apewe ofisi ya umma na kuvumiliwa hata akilalamikiwa? Rejea akina Richmonduli,BOT, TanPower, ANBEN,Fosnik na madude mengine.
Wahusika wakiri kuwa hawana nia ya kupamba na rushwa na vita imewashinda vinginevyo kuendelea kuimba nyimbo za kulaani rushwa wakati ndiyo inawalisha wengi ni unafiki.
Hitimisho. Rushwa ipigwe vita kwa kutumia akili badala ya visingizio kama kushughulikia vidagaa huku papa wakizidi kuzaliana na kupanua ukoo kutoka kwenye siasa kwenda kwenye vyombo vya habari siasa na sehemu nyingine za jamii zenye ulaji.Tubadilike.