JUMUIYA na Taasisi za Kiislamu imemtaka Papa Benedict XVI kuwaomba radhi Waislamu wa Tanzania kabla ya kuja nchini kutokana na maneno yake aliyoyatoa akimkashfu Mtume Muhamed mwaka jana, wakati akihutubia katika chuo kikuu kimoja nchini Ujerumani, la sivyo hawataitambua ziara yake.
Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Jakaya Kikwete amualike Papa kuja kutembelea Tanzania, wakati wa ziara yake aliyoifanya hivi karibuni nchini Italia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Msikiti wa Kichangani, Magomeni Mapipa, Katibu wa kikao hicho, Sheikh Ponda Powela, alisema kuomba radhi kwa Papa huyo itakuwa hatua muhimu na ishara ya kusafisha dhamira yake dhidi Uislamu na Waislamu.
Alisema endapo hatafanya hivyo, Waislamu wa Tanzania hawatatambua ziara na wataipinga kwa kufanya maandamano makubwa nchi nzima.
"Akihutubia katika chuo kikuu nchini Ujerumani, Papa alitoa mhadhara unaohusu imani ya dini ya Kiislamu, ambapo katika mengi aliyozungumza mwisho alihitimisha kwa madai kuwa Mtume anayefuatwa na Waislamu katika uhai wake wote hana lolote jema alilofundisha hapa ulimwenguni.
"Kwa upande wa mawakala wa kanisa waliojaa katika mamlaka mbalimbali, huo ulikuwa ni waraka wa 'Kiungu' unaotoa maagizo ya kuwashughulikia Waislamu na dini yao popote walipo ulimwenguni.
"Lakini kwa upande wa jamii ya Waislamu huo ulikuwa ni waraka wa chagizo kwa mataifa ya Marekani na washirika wake wanaoamini kuwa Uislamu haufundishi mema yoyote duniani zaidi ya mafundisho ya kigaidi," alisema Sheikh Powela.
Kauli hizo za Papa zilizua tafrani kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu na kusababisha maafa katika nchi kadhaa ulimwenguni.
Alisema ujio wa Papa mwenye msimamo kama huu ni hatari kwa umoja wa kitaifa na ni hatari zaidi kwa Waislamu hasa ukizingatia misingi ya utawala iliyojengwa hapa Tanzania.
Hivyo anao wajibu wa kuwaomba radhi Waislamu wa kila taifa analotaka kutembelea kwani hii itakuwa ni hatua muhimu na ishara ya kusafisha dhamira yake dhidi ya Uislamu na Waislamu,"alisema Katibu huyo .
Akijibu kuhusu kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Mtikila kuhusu kurejeshwa kwa Mahakama ya Kadhi, Powela alisema wenye haki ya kujibu shtaka au kutetea uwepo wa mahakama ya hiyo ni Chama Cha Mapinduzi na serikali yake kwani ni moja ya ilani ambazo zipo kwenye chama hicho.
Alisema mahakama ya kadhi kamwe haiwezi kuwa demokrasia kwani katika dini ya Kiislamu ni faradhi isiyoepukika na kuongeza kwamba mchakato wa kuwepo kwake upo na unaendelea chini ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu.
Kwa mujibu wa katibu huyo, alisema mchakato huo utakapokamilika, Mahakama ya Kadhi itakuwepo hata kama wanasiasa na watu wa itikadi na dini nyingine hawatairidhia.