Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Waziri Sophia Simba mgonjwa
http://www.habaritanzania.com/articles/4223/1/Waziri-Sophia-Simba-mgonjwa
By Marshy Abdu
Published on 10/27/2007
 
WAKATI aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, anazikwa leo mkoani Kilimanjaro, imefahamika kuwa Waziri wake, Sofia Simba, ni mgonjwa na hawezi kufanya kazi.

Waziri Sophia Simba mgonjwa
WAKATI aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, anazikwa leo mkoani Kilimanjaro, imefahamika kuwa Waziri wake, Sofia Simba, ni mgonjwa na hawezi kufanya kazi.

Kutokana na maradhi yanayomkabili, Waziri Simba alishindwa kujitokeza juzi na jana kwa ajili ya shughuli za kuupokea na baadaye kuuaga mwili wa marehemu, Salome Mbatia, aliyepoteza maisha kwa ajali ya gari wilayani Njombe, Jumatano wiki hii.

Mmoja wa viongozi wa juu wa wizara hiyo, aliyezungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa yeye si msemaji alithibitisha kuhusu kuugua kwa Waziri Simba.

Kwa mujibu wa ofisa huyo wa cheo cha juu, Waziri Simba alianza kuugua siku chache zilizopita akiwa nchini Afrika Kusini, alikokwenda kuhudhuria mkutano.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, David Mathayo, jana aliizungumzia kwa undani ajali iliyosababisha kifo cha Mbatia. Mathayo ni mmoja wa watu wa mwanzo kufika katika eneo la ajali, Lupembe Factory, wilayani Njombe.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Mathayo alisema kuwa alifika muda mfupi eneo la tukio, akiwa njiani kuelekea Tunduru. Alisema akiwa analikaribia eneo hilo, aliona gari dogo aina ya Nissan likiwa limelaliwa na lori.

Alisema ajali hiyo ilitokea kilomita sita kutoka Njombe na barabara katika eneo hilo imenyooka na wakati huo magari mengi yakiwemo mabasi na magari mengine yalikuwa yakipita na kuendelea na safari zao.

"Wakati nakaribia eneo hilo, niliona ajali na gari dogo likiwa limelaliwa na lori, kwa ubinadamu na kama kiongozi wa kiserikali niliona nawajibika kusimama na kutoa msaada.

"Nilipofika nilimuona mtu amebanwa na gari, nilienda katika Kiwanda cha Tancot ambacho kipo jirani na eneo hilo kuomba trekta kwa ajili ya kuondoa lori lile," alisema.

Alisema kiwanda hicho kilitoa matrekta mawili kwa ajili ya kazi hiyo na kwamba kabla ya kuliondoa walipunguza mbao zilizokuwa zimesheneni.

"Baada ya kuliondoa gari hilo nilimwona dereva wa gari hilo akiwa amebanwa na pembeni yake kulikuwa na bahasha iliyokuwa na barua… nilipoiangalia niliona jina la Salome Mbatia.

"Pia kulikuwa na kipochi (hand bag), nilipoifungua nilikuta vitambulisho vyenye jina la Salome Mbatia na ndipo nilipomwangalia maiti yule mwanamke na kubaini alikuwa Salome Mbatia, ambaye ni Naibu Waziri mwenzangu," alisema.

Alisema alipofika eneo la tukio watu waliokuwapo walimweleza kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, naye alikuwepo eneo la tukio na aliwachukua majeruhi wawili na kuwapeleka hospitali.

"Mtu wa kwanza kumpigia simu alikuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, lakini wakati huo simu yake ilikuwa haipatikani kwa sababu alikuwa kwenye ndege. Nilimpigia IGP, Said Mwema, Ikulu, Spika na viongozi wengine kuhusu ajali hiyo," alisema Mathayo.

Pia alisema alimpigia simu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Said, ambaye alilazimika kukatisha ziara na kufika eneo la ajali baada ya muda mfupi.

Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete, jana aliongoza viongozi wakuu wa kitaifa na maelfu ya waombolezaji kuaga mwili Mbatia, nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Alipomaliza kutoa salamu za mwisho akiwa ameandamana na mkewe, Rais Kikwete alionekana akitokwa machozi.

Baada ya kutoa heshima za mwisho alikwenda kuwapa mkono wa pole watoto wa marehemu; Yolanda, Philipo, Charles na Boniphace.

Vilio vya watoto hao vilianza kusikia wakati Waziri Mkuu, Edward Lowassa na mkewe, Mama Regina, alipokwenda kumuaga.

Waliofuata katika kutoa heshima za mwisho ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein na mkewe, Rais wa Zanzibar, Aman Karume na mkewe, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mkewe, na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na mkewe.

Baada ya viongiozi hao kumaliza kuaga mwili wa marehemu Mbatia, walimuaga mume wa marehemu, Dk. Joseph Mbatia, kisha kuondoka, na ndipo viongozi wengine wa kitaifa, kisiasa na kichama walipopewa nafasi ya kuaga mwili huo.

Mwili wa marehemu Mbatia, uliwasili nyumbani kwake Oysterbay, Mtaa wa Uganda, nyumba namba 120, saa 2:13 asubuhi na dakika chache baadaye ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Methodius Kilaini ilifanyika.

Akizungumza jana baada ya kumuaga marehemu, Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, alisema kwa kuwa marehemu Mbatia alikuwa mchapakazi, jambo la kujifunza kutoka kwake ni kutekeleza majukumu kwa uadilifu.

Alisema alimfahamu Mbatia katika masuala ya chama akiwa Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema kwamba alikuwa akitekekeza majukumu yake bila kutetereka.

Naye Waziri Ofisi ya Rais, Ikulu, Uhusiano wa Jamii na Siasa, Kingunge Ngombale-Mwiru, alisema marehemu Mbatia alifanya kazi nzuri na akiisaidia CCM kuweka utaratibu mzuri wa kutunza fedha.

"Marehemu Mbatia alikuwa mchapakazi si kwenye masuala ya fedha pekee, bali pia katika shughuli za kichama. Alikuwa kiongozi mahiri," alisema Kingunge.

Mbunge wa Mtera, John Malecela, alisema kifo cha Mbatia ni pigo kubwa, lakini kifo kwa binadamu si kitu cha kuepukika.

Alisema marehemu Mbatia alikuwa mwepesi kujifunza na akiwa Mweka Hazina alikisaidia chama kupata fedha.

Baada ya kumalizika kwa shughuli ya kuaga mwili wa kiongozi huyo, ulipakizwa kwenye gari maalumu la kubebea wagonjwa aina ya Land Rover Defender, 1776 JW04 na kupekekwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kusafirishwa Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika leo.

Manaibu waziri, Joel Bendera, Lucas Siame, David Mathayo, Daniel Nsanzugwanko, William Ngeleja na Loduvick Mwananzila, ndio walibeba jeneza baada ya kuagwa na kulipakiza katika gari hilo.

Mwili huo baada ya kufikishwa uwanja wa ndege ulipakizwa katika ndege ya serikali aina ya Fokker 50, yenye namba za usajili 5H-TGH kwa safari ya Moshi.

Kabla ya mwili wa marehemu kupandishwa kwenye ndege, mvua ilinyesha eneo hilo, hali iliyosababisha baadhi ya waombolezaji kujibanza pembeni kujikinga mvua.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mazishi hayo, Andrew Chenge, alisema viongozi waliotakiwa kupanda ndege moja ya maiti hiyo ni Naibu Waziri wa Maji, Shamsa Mwangunga, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk. George Mlingwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Said.

Wengine ni Katibu Muhtasi wa marehemu Mbatia, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mariam Mwaffisi na familia ya marehemu.

Katika ajali hiyo, gari la naibu waziri huyo, T 724 AGZ Nissan Safari, liligongana uso kwa uso na gari T 299 AFJ Mitsubishi Fuso, mali ya Jackson Kilagwa wa Rujewa, Mbeya.

Mbali na ajali hiyo kusababisha kifo cha naibu waziri huyo na dereva wake, pia msaidizi wa dereva wa roli hilo, Castory Kilangwa, naye alifariki.

Dereva wa lori hilo, Peter Mangula, mkazi wa Makambako, wilayani Njombe, aliyenusurika katika ajali hiyo, alitoroka baada ya ajali hiyo na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka.

Wakati huo huo, aliyekuwa dereva wa naibu waziri huyo, ambaye pia alifariki katika ajali hiyo, Anakleti Mogella umezikwa jana katika makaburi ya Mburahati.

Kutoka Iringa, Godfrey God anaripoti kuwa mmiliki wa lori lililohusika katika ajali iliyosababisha vifo vya watu watatu, akiwemo aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, Jackson Kilangwa, mkazi wa Rujewa, Mbarali, Mkoa wa Mbeya, anashikiliwa na polisi huku dereva wake akiendelea kusakwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Said Mwema, Mkurugenzi wa Mafunzo na Utendaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paulo Chagonja, alisema kuwa jeshi hilo linaendelea kumsaka kwa nguvu zote dereva wa lori hilo aina ya Fuso lenye namba za usajili T 299 AFJ, Peter Mangula (26) mkazi wa Makambako, Wilaya ya Njombe kwa tuhuma za kusababisha ajali hiyo.

Aidha, Kamishna Chagonja aliwataja watu wengine waliofariki dunia kutokana na ajali hiyo pamoja na Mbatia kuwa ni dereva wa gari lenye namba za usajili T 724 AGZ aina ya Nissan Patrol mali ya Mbatia, Anaclet Magole, mkazi wa Dar es Salaam na Castory Kilangwa, ndugu wa mmiliki wa Fuso.

Aliwataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Nicholaus Lubava (35), mkazi wa Mufindi ambaye ameumia ubavu na Dastun Gonze (26) mkazi wa Igowole, Mufindi aliyevunjika mkono wa kushoto. Wote wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Njombe kwa matibabu zaidi.

Chagonja alisema kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uamuzi wa dereva wa Fuso kupita upande wa barabara ambao si wake huku akiwa katika mwendo mkali.

Kutoka Moshi, Charles Ndagulla, anaripoti kuwa mamia ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa jirani, leo wanatazamiwa kushiriki mazishi ya Mbatia.

Mwili huo wa marehemu Mbatia uliwasili mjini hapa jana majira ya saa 8:25 mchana na kupelekwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambako ulihifadhiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanajro, Mohamed Babu, aliyekuwa ameongoza msafara wa viongozi waliousindikiza mwili wa marehemu kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alisema mwili huo utachukuliwa leo asubuhi saa 2:30 na kupelekwa nyumbani kwake Mtaa wa Mnazi, Kata ya Msaranga mjini hapa.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, wananchi watapata muda wa kutoa heshima za mwisho kabla ya mwili huo kupelekwa Kanisa Kuu la Kristo Mfaume, kwa ajili ya ibada itakayoongozwa na Askofu Amedeus Msarikie wa Jimbo Katoliki la Moshi.

Mara baada ya ibada hiyo ya mazishi, mwili huo utapelekwa moja kwa moja hadi kwenye makaburi yaliyopo Parokia ya Mbokomu, Wilaya ya Moshi Vijijini ambako mazishi yatafanyika kwa heshima zote za kiserikali na kidini.

Mkuu huyo wa mkoa, alisema mara baada ya mazishi, waombolezaji watakwenda nyumbani kwa marehemu huko Msaranga kwa ajli ya kutoa mkono wa pole.