Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Ukimya wa Mkapa , Ushahidi wa Kutoka Kapa Darasani!
http://www.habaritanzania.com/articles/4220/1/Ukimya-wa-Mkapa-,-Ushahidi-wa-Kutoka-Kapa-Darasani!
By Mzee Mwanakijiji
Published on 10/23/2007
 
Makala hii ilitoka kwenye gazeti la "Kulikoni" siku ya Jumatatu Octoba 22, 2007. Niliandika makala hii kufuatia kuendelea kwa Rais mstaafu Mkapa kuwa bubu kufuatia tuhuma mbalimbali zinazomkabili. Kwanini yuko kimya?

Ukimya wa Mkapa , Ushahidi wa Kutoka Kapa Darasani!

Kuna sababu nyingi zinazomfanya Rais Mstaafu Ndg. Benjamin William Mkapa kuamua kukaa kimya. Sababu mojawapo ni hii aliyoitoa mwishoni mwa juma kuwa yeye amestaafu siasa na hivyo asibughudhiwe.  Bila ya shaka anazo sababu nyingine nyingi za kwanini hataki kujibu tuhuma zilizoelekezwa kwake kwa karibu mwaka mzima na watu mbalimbali na hivi karibuni zikitolewa na viongozi wa vyama vya kisiasa na wazee wa nchi hii. Hata hivyo katika hayo yote Rais Mkapa hataki kujibu tuhuma hizo zote.  

 

Binafsi sijui ni kitu gani kinamfanya Rais Mkapa aamue kuwa kimya kuhusu madai na maneno mbalimbali yanayoelekezwa kwake. Hata hivyo ninaamini kuwa kuna sababu nyingine kadhaa ambazo zinamfanye aamue kuwa bubu na kubwa  ya hizo na ambayo naamini imempa ububu huo ni kuwa miongoni mwa wanafunzi wa karibu wa Mwalimu, Rais Mkapa amefeli vibaya sana katika darasa hilo. Nitaeleza kwa nini naamini hivyo.

 

Nitawakumbusha kitu kimoja ambacho naamini wengi yawezekana wamekisahau au hawakukitilia maanani kilipotokea wakati mwili wa Baba wa Taifa umelala kule London. Serikali ilituma ujumbe kule London ukiongozwa na makamu wa Rais Marehemu Dr. Omar Ali Juma pamoja na Mzee Malecela. Walipofika Ubalozini kwetu pale London ambapo Mama Maria na wandugu wengine walikua pale kupokea rambirambi za watu, mama Maria alipowaona alianza kulia na kusema wanafunzi wako wamefika. Alirudia maneno hayo katika dimbwi kubwa la huzuni na uchungu na mzee Malecela na Dr. Omar walijibu ndio mama tumefika.

 

Ninapofikiria suala la ukimya wa Rais Mkapa ninapata jibu katika maneno hayo ya mama Maria kuwa baadhi ya watu ambao walikuwa karibu na Mwalimu walikuwa ni kama wanafunzi wake na kwa kweli kwao alikuwa ni Mwalimu. Paul Sozigwa wakati fulani akihojiwa na Public Broadcasting Corporaton ya Marekani alikiri ukweli huu kuwa kwa wale waliopata nafasi ya kufanya kazi chini ya Mwalimu kwa kweli walikuwa ni wanafunzi wake, na aliona fahari kujifunza toka kwa Baba wa Taifa.

 

Miaka nane baadaye tunaweza kuamua kwa uhakika kabisa ni nani kati ya wanafunzi wa Mwalimu alihitimu vizuri kabisa na ni nani aliyefeli vibaya kabisa. Naomba nitangaze hadharani kuwa waliofanya vizuri wapo na wanajulikana wa kwanza kati yao bila shaka anaendelea kubakia kuwa ni Dr. Salim Ahmed Salim. Na wa mwisho katika darasa hilo ni Rais Benjamin Mkapa. Bila ya shaka umesoma mahojiano ya Dr. Salim na KLH News mwishoni mwa juma na ni jinsi gani anaonesha darasa la Mwalimu lilivyomwingia. Kwa upande mwingine ukimya wa Rais Mkapa unadhihirisha ni jinsi gani aliingia darasa la Mwalimu lakini darasa la Mwalimu halikumuingia!!

 

Ukimya wa Rais Mkapa unadhihirisha dharau na dhihaka yake dhidi ya Watanzania. Mwalimu kati ya vitu alivyotufundisha ni heshima kwa kila mtu na hata watu ambao hawana nguvu ya kusababisha jambo kufanyika. Paul Sozigwa alisimulia katika mahojiano yake ya na PBS  juu ya kisa kimoja cha Mwalimu ambapo walikuwa wanajiandaa kwenda mahali fulani na wakati viongozi wote walikuwa wameshakula na tayari kuondoka Mwalimu aliuliza kama dereva wake ameshakula. Wakamwambia bado hajala. Mwalimu akasema hawawezi kuondoka hadi huyo dereva ale, na alishangaa kwanini hakula tangu mwanzo. Mwalimu hakudharau mtu, na zaidi ya yote licha ya maneno yaliyokuwa yakitolewa dhidi yake  aliwajibu kwa heshima japo wakati mwingine alionesha kwa kejeli jinsi gani hoja fulani zilikuwa dhaifu.

 

Ukimya wa Rais Mkapa unadhihisha kutokujali kwake wananchi waliompa nafasi ya kutumikia nchi yake. Tuhuma zinazoelekezwa kwake kuanzia ya matumizi ya dola milioni 1 (250,000 toka mchango wa ahadi na 750,000 toka UNICEF) za mapambano ya Malaria, ujasiriamali wake, na hisa zake katika mradi wa Makaa ya Mawe huko Kiwira ni tuhuma na madai mazito. Ukweli ni kwamba siyo madai yote yanahusu rushwa  ila haya mengine yanahusu matumizi mabaya ya cheo chake na matumizi mabaya ya ofisi yake. Anapokataa kuzungumzia na kujibu maswali ya wananchi wenzake ambao walimpa dhamana ya kuwaongoza, Rais Mkapa anaonesha kilele cha kiburi cha mtu aliyelewa madaraka. Anajaribu kupuuzia hoja hizi kwa vile anajua ni za kipuuzi au hazina msingi. Ukimya wake hata hivyo hauzifanyi hoja hizo kuwa za kipuuzi bali unathibitisha kuwa yawezekana hana la kusema kwani amekamatwa pabaya.

 

Ukimya huo ni kama ukimya wa mtoto ambaye mzazi anaporudi toka kazini anakuwa wa kwanza kusema mimi sijalamba Sukari. Anachosahau ni kuwa chembe za  sukari zimezunguka mdomo wake na mzazi anapomwonyesha hilo anajikuta anainama kwa aibu na badala yake kudai kuwa hakulamba sukari peke yake. Rais Mkapa hawezi na hana ujasiri wa kusimama hadharani kujibu madai hayo au kuyaonesha kuwa hayana msingi kwani akifanya hivyo atafungua maswali mengine lukuki. Hivyo ni bora (anavyoona yeye) awayeyushe Watanzania kwani hawana mpango na ni watu wasio na shukrani.

 

Ukimya wa Rais Mkapa unadhihirisha jambo jingine pia. Yeye hana shukrani kwa wananchi waliomuamini na kumpa nafasi kubwa kabisa ya kuwaongoza. Mara baada ya Uhuru kulikuwa na tetesi za ubaguzi wa kikabila katika utumishi wa Umma. Tetesi hizo zilimlazimisha Rais Nyerere kuunda tume ya kuchunguza ukweli wa tuhuma hizo. Mwalimu hakupuuzia hoja au maneno ya chini chini. Alipokufa Waziri Mkuu Sokoine, watu walianza maneno ya chini chini, Mwalimu alilizungumzia hilo na akawataka wananchi waamini kuwa ilikuwa ni ajali, hakupuuzia. CCM walipobadili Katiba na kufuta haki ya wananchi kuchaguliwa bila kuwa na chama chochote Mwalimu hakupuuzia alisimama na kuwaambia uamuzi huo ulikuwa ni wa kipumbavu.

 

Mwalimu alijua kabisa kuwa nafasi aliyokuwa nayo ya kutumikia Tanzania na Watanzania wenzake haikuwa kwa sababu yeye alikuwa ni bora kuliko watu wote au alikuwa ndiyo mwenye uwezo wa kuongoza kuliko wote. Alijua kuwa nafasi hiyo ilitokana na imani ya Watanzania kwake, na wakati wote aliongozwa na hisia hiyo ya kuwa na deni kwao. Hata alipochangiwa kwenda Umoja wa Mataifa kwenda kujenga hoja ya kuwa huru, Mwalimu alihakikisha fedha zisizohitajika zinarudishwa kwenye Chama, ni wazi angeweza kutumia kwa manunuzi huko majuu  lakini yeye hakutaka kuanzisha ujasiriamali Ikulu!  Alijua kuwa uongozi ni dhamana na ni dhamana ambayo waliokudhamini wanapohitaji maelezo wanastahili kupewa. Somo hilo bila ya shaka Rais Mkapa limempita pembeni.

 

Ukimya wake unadhihirisha kitu kingine pia. Kwamba, Rais Mkapa anaamini kwa moyo wake wote (japo kwa makosa) kuwa hawezi kulazimishwa kujitetea na kutoa maelezo ya matumizi ya ofisi yake au cheo chake kinyume cha sheria. Imani hiyo inatokana na ukweli kuwa mtu pekee ambaye anaweza kumfanya azungumze tayari amemkingia kifua! Rais Kikwete alimkingia kifua Mkapa kule Sweden kuhusu suala la Rada na akafanya hivyo tena kule Kisarawe. Hicho ndicho kinachompa kiburi mzee wetu na haoni sababu ya kuzungumza na wananchi kuhusu madai haya kwani kama mwenye kaya kasema aachwe mzee wetu nani anathubutu kufanya vinginevyo?

 

Hata hivyo ukweli utaendelea kuwa ukweli. Rais Mkapa kuna mambo aliyoyafanya ambayo si yote anastahili pongezi kwani mengine ni jasho la watu wengine. Suala la uchumi kutengemaa siyo matunda ya Mkapa peke yake kwani msingi wa mabadiliko makubwa ya kiuchumi yaliyotokea mwanzoni mwa utawala wa Mkapa havikutokana na juhudi za Mkapa mwenyewe bali zilitokana na juhudi za wazi za Baba wa Taifa kuongoza kampeni ya kutaka madeni yetu yasiyobebeka yasamehewe. Mkapa alilijua hilo na wakati fulani kule Afrika Kusini alisikika akisema kuwa miaka ya mwanzo hakuweza kufanya lolote kutokana na kivuli cha Mwalimu.

 

Uwepo wa Mwalimu ilikuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa Mkapa na wenzake kufanya kila watakalo. Ni wazi kuwa kama Mwalimu angekuwa hai Mkapa leo hii angeona kiboko cha Mwalimu. Lakini sasa hivi hana wasiwasi wowote kwani jumuiya ya kimataifa inamsifia na kumtuza na amejijengea marafiki kila kona duniani. Hata hivyo akumbuke kuwa isije ikaja siku na yeye akajikuta anazungumzwa kama alivyozungumzwa Mobutu au viongozi wengine ambao waliamua kuzikimbia nchi zao! Ni wazi kuwa baada ya kifo cha Mwalimu Mkapa na genge la viongozi waliokwepa darasa la Mwalimu waliona kuwa hatimaye mwalimu katoka darasani na walikuwa na uwezo wa kupiga kelele watakavyo, kwani kiongozi wa kelele hizo ni monita mwenyewe!

 

Matokeo ya utawala huu wa panya baada ya paka kuondoka ndiyo haya tunayoyashuhudia leo hii. Uongozi wa kibabe, kiburi cha madaraka, uleaji wa wazembe na tumefikia mahali tunawazawadia watuhimiwa wa uhalifu jukwaa la kututukania wake zetu na hakuna kiongozi yeyote ambaye anaona kitendo hicho ni kibaya na cha kufedhehesha. Ni wazi kuwa kifo cha Mwalimu kwa Mkapa ilikuwa ni ufunguo wa bahati kuwa ile miradi na ujasiriamali ambao asingeweza kuufanya wakati Mwalimu yuko hai, sasa alikuwa anaufanya pasipo hofu ya kukemewa na mtu yeyote kwani yeye ndiye mwenye Kigoda cha Taifa. Ikawa kama Kichaa kapewa rungu sokoni.

 

Ni matokeo ya uongozi wake yeye mwenyewe Rais Mkapa ndipo alipojikuta katika hotuba yake ya Januari 31 (mwisho wa mwezi) mwaka 2005 alijikuta anazungumzia suala la Uaminifu na alijenga hoja kuwa Watanzania wamekosa uaminifu. Katika hotuba yake ile alizungumza kana kwamba yeye ndiye Mwaminifu Mkuu wa Tanzania na ya kuwa wengine wote siyo waaminifu. Leo hii tunatambua kuwa maneno yale yalikuwa ni propaganda za kisiasa tu na hayakuwa yanatoka moyoni mwa mtu mwaminifu. Hotuba ile ilitoka kwa mtu wa kwanza kabisa kukosa uaminifu! Kwa kushiriki kununua rada ya bilioni 50 (yenye rushwa ya karibu bilioni 12) Rais Mkapa alikosa uaminifu; Kwa kuacha Tanzania iingie kwenye mkataba mbovu na wenye gharama kubwa, Rais Mkapa alikosa uaminifu; kwa kushindwa kuwaambia wananchi matumizi ya dola milioni 1  ambazo Tanzania iliahidiwa kule Davos Mkapa alikosa uaminifu; Kwa kuamua kuanzisha biashara akiwa Ikulu na kutumia anuani ya Ikulu kufanya biashara hiyo, Mkapa alikosa uaminifu; kwa kushirikia kununua hisa za kampuni ya Kiwira (yeye na Waziri wake) na baadaye kuipatia Kiwira mkataba mnono wa Tanesco na hivyo kutumia vibaya madaraka yake, Mkapa alikosa uaminifu; Na kwa kitendo cha yeye kuendelea kupuuza madai na kukejeli hoja zinazohitaji maelezo yake, Rais Mkapa anaonesha ni jinsi gani amekuwa kilele na mfano wa Watanzania waliokosa Uaminifu.

 

Hata hivyo nina imani kuwa baada ya kufikiri kwa kina na akizingatia hukumu ya historia iliyo mbele yake, Rais Mkapa ataamua kuzungumza na wananchi na kujibu maswali yao na pale penye upungufu akakiri hivyo. Watanzania watamheshimu kama atakubali kuwa kwa kufanya biashara akiwa Ikulu ilikuwa ni kukosea kimaadili kwa kiasi kikubwa na akaamua kuachilia hisa zake na za familia yake toka Kiwira basi watu watamheshimu. Kama atamuomba Rais Kikwete aidhinishe ile barua aliyokataa yeye kuiweka hadharani toka Benki ya Dunia kuhusu rada, watu wataanza kumwamini; na akiamua kuomba radhi na kutoa ufafanuzi wa kuridhisha basi watu watamsamehe na tutaendelea na mambo mengine.

 

Hata hivyo kuendelea kukaa kimya kana kwamba anayezungumzwa ni mtu wa nchi ya kufikirika ni kiburi ambacho lazima kipingwe na kiitwe kwa jina hilo. Ukimya wake lazima uvunjwe na mapema ni bora zaidi kwani hana mkataba na mbinguni na kesho haijahaidiwa kwa mtu yeyote. Asiendelee kukaa kimya na kuona Watanzania hawana mpango na kubakia kusema kama wale waliokosa uaminifu katika hotuba yake ile mtajiju. Rais Mkapa awe jasiri, asimame hadharani na azungumze na wananchi wenzie ili jambo hili liishe kiungwana. Vinginevyo, asije kujikuta licha ya mema aliyoyafanya anaanza kufutwa katika historia ya Tanzania kama Wamisri walivyofuta historia za viongozi waliowachengua.

 

Rais Mkapa asimame aseme sasa, vinginevyo na anyamaze milele! Mimi ni Mjenga hoja, na hiyo ni hoja yangu, ukijibu ijibu kwa hoja.

 

Nitumie ujumbe: mjengahoja-at-jamboforums.com