Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mahakama ya Kadhi yagonganisha vichwa
Mahakama ya Kadhi yagonganisha vichwa
By Marshy Abdu | Published  10/22/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Mahakama ya Kadhi yagonganisha vichwa
na Tamali Vullu na Safina Tibanyendela


KWA mara nyingine, suala la Mahakama ya Kadhi, limezusha mjadala baina ya wanaharakati wa kidini na wanasiasa, ambao wanabishana mambo kadhaa kuhusiana na mahakama hiyo.

Mjadala huo umeibuka hivi sasa kufuatia hatua ya Mchungaji Christopher Mtikila na Kanisa lake la Wokovu, kufungua kesi Mahakama Kuu, akiitaka izuie harakati zozote za kuanzishwa kwa mahakama hiyo nchini, kwa madai kuwa kuanzishwa kwake kunakwenda kinyume cha Katiba.

Uamuzi huo ulidakwa na Waislamu kwa uopande mmoja na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwa upande mwingine, na kumfanya Mchungaji Mtikila jana kuitisha mkutano wa waandishi wa habari, naye kutoa maelezo kuhusiana na hatua aliyoichukua na kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na pande hizo mbili.

Katika mkutano huo, Mchungaji Mtikila, ambaye pia ni mwenyekiti wa Democratic Party (DP), alimtaka Lowassa kuwaomba radhi wananchi, kwa kuichezea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kuwa Lowassa amekiuka katiba hiyo kwa kulizungumzia suala la Mahakama ya Kadhi, wakati lipo mahakamani.

Alisema Lowassa ametamka maneno mabaya ambayo ni kosa la jinai, na kufananisha kitendo hicho na ufisadi wa kiimani, ambao alidai kuwa umeanza kujitokeza nchini.

Alisema kwa kuwa suala hilo limeshafikishwa mahakamani, serikali na Bunge hawapaswi kulizungumzia, bali wananchi ambao wana uhuru wa kutoa maoni yao katika masuala yanayowahusu.

Akiwa ziarani mkoani Mbeya, Lowassa alikaririwa akisema serikali haina mpango wa kupeleka muswada wa kuanzishwa mahakama hiyo katika kikao kijacho cha Bunge kitakachoanza Oktoba 30, mwaka huu mjini Dodoma.

Badala yake, alisema suala hilo linashughulikiwa na Tume ya Kurekebisha Sheria, ambayo ilikabidhiwa baada ya kupokea maombi ya waumini wa Kiislamu, wakitaka kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

Ufafanuzi huo wa Waziri Mkuu unatokana na kile alichosema kuwa amekuwa akipokea simu nyingi na ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu za mikononi (sms), kutoka kwa watu wanaohoji iwapo kweli serikali inataka kupeleka suala hilo bungeni.

Kutokana na hilo, mchungaji huyo alisema ataitisha maandamano makubwa ya kutaka katiba iheshimiwe na wale watakaoichezea wachukuliwe hatua.

“Lowassa amezungumza mambo mabaya, tena namuonya asiendee kwa kuwa kipindi hiki ni kibaya, kuna suala la rushwa na ufisadi limetawala na watu wamebadilika,” alisema Mtikika.

Alisema kwa mujibu wa Ibara ya 20 2(a) (i), ni marufuku kwa chama au kikundi chochote kujihusisha na kikundi fulani kwa masilahi ya dini, na kusema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya makosa kuingiza suala la Mahakama ya Kadhi katika Ilani yake ya uchaguzi.

Alisema kutokana na hali hiyo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, anapaswa kuiondoa CCM katika orodha ya vyama vya siasa vilivyosajiliwa nchini kwa kosa hilo.

Mchungaji Mtikila alisema CCM walifanya hivyo kwa lengo la kupata kura za Waislamu huku wakijua ni hatari na mwiko kwa chama cha siasa kufanya hivyo.

“Hii si Jamhuri ya Kiislamu… hatuwezi kuachia hili lipite, lazima tushughulike nao. Hii ni nchi ya watu wote na amani ikiharibika watakaoathirika si Waislamu pekee bali wote tuliopo.

“Hatulengi kuwaudhi Waislamu na tafsiri ya Kadhi hatuwezi kuipata kwa viongozi bali ipo kwenye misahafu… na mahakama hiyo lengo lake si ndoa na mirathi kama tunavyoambiwa, kazi yake ni kukata vichwa watu wasiomkubali Allah,” alisema Mtikila.

Kutokana na hali hiyo, Mchungaji Mtikila alieleza kuwa Rais Kikwete anapaswa kujiuzulu kwa kuruhusu masuala kama hayo ambayo ni hatari kwa nchi.

Alitoa mfano kuwa damu zinazomwagika sasa nchini Somalia na kudai kuwa machafuko nchini humo yanatokana na kuwapo kwa Mahakama ya Kadhi na kuhoji Rais Kikwete anataka hali hiyo itokee nchini?

Hata hivyo, alisema ni jambo la faraja kuwa suala hilo mpaka sasa halijawagawa watu.

Aidha, Mtikila alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa Rais Jakaya Kikwete hakumweleza ukweli Papa Benedict XVI, kuhusu kuwapo wa amani ya kiimani nchini na kusema kuwa hawezi kuvumilia suala hilo, hivyo atamweleza papa ukweli halisi.

Alipokutana na Rais Kikwete, Papa Benedict VXI, alisifu hali ya uvumilivu wa kidini iliyopo nchini.

Rais Kikwete aliwaeleza waandishi wa habari anaofuatana nao kwenye ziara nchini Italia kuwa Papa ameeleza kuridhishwa kwake na maelewano ya amani ya kidini nchini.

“Alisema hana malalamiko kuhusu Tanzania na amefurahishwa na serikali zote kuendeleza misingi ya amani na utulivu iliyowekwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere,” alikaririwa Rais Kikwete.

Hata hivyo, Mtikila alisema uvumilivu wa kiimani nchini haupo, na kutoa mfano wa Dibagula alishitakiwa na kufungwa kwa madai ya kukashifu dini nyingine. Hata hivyo, baadaye Dibagula aliachiwa huru.

Kwa upande mwingine, Waislamu wameitaka serikali kumchukulia hatua Mchungaji Mtikila kwa madai kuwa ni mchochezi.

Waislamu hao wameitaka serikali kumchukulia hatua Mchungaji Mtikila kama inavyomchukulia hatua mtu yeyote mchochezi nchini, kutokana na kitendo chake cha kwenda mahakamani kupinga kuwapo kwa Mahakama ya Kadhi kwa madai kuwa ni chombo cha ugaidi, jambo walilosema si la kweli.

Akizungumza katika mjadala uliorushwa hewani juzi na Radio Quran, Imamu wa Msikiti wa Mnyamani uliopo Buguruni, Mohammed Iddi, alisema kitendo hicho cha Mtikila ni cha kuwadhalilisha na kuwatukana Waislamu.

Alisema kutokana na hali hiyo, Mwislamu yeyote hapaswi kusalimiana na Mchungaji huyo wala kumsaidia Mtikila kwa jambo lolote kwa kuwa hawatakii mema.

Alisema katika dini ya Kiislamu wanaruhusiwa kutoa adhabu kama hiyo kwa mtu anayeukashfu Uislamu na kuidhalilisha dini hiyo, hivyo kuwataka Waislamu waliopo kwenye chama anachokiongoza Mtikila kujiondoa mara moja.

“Wabunge wote ambao ni Waislamu waliomo kwenye Bunge nao watoe tamko la kukataa kauli ya Mtikila kwa kukanusha au kukubali, ili tuweze kujua kama na wao wanaungana na Mtikila au vipi,” alisema.

Imam huyo alisena anahisi Mtikila ametumwa na Serikali, Wakristo na hasa viongozi na kusema iwapo hisia hizo si za kweli, Wakristo, hasa viongozi, watoe tamko kuhusu kauli za Mtikila.

Aidha, alimtaka Mtikila kufanya utafiti katika nchi ambazo zimeanzisha Mahakama ya Kadhi ili abaini ni watu wangapi ambao wameuawa na kunyongwa kutokana na hukumu za mahakama hizo, ili atakayoyasema yawe na ushahidi.

Akizungumzia kauli ya waziri mkuu, Imam Idd, alisema kitendo cha Lowassa kusema amepokea sms nyingi na simu na kutaka hilo suala lijadiliwe kwanza na wadau kisha litolewe majibu, ni kutaka kuwapotezea muda Waislamu wasiipate mahakama hiyo.

Alihoji, kwa nini wadau hao, ambao bila shaka watakuwa ni Wakristo, wahusishwe kwenye kutoa maoni kuhusu suala hilo na si Waislamu wenyewe ambao ndio wahusika.

Alisema tume, iliyokuwa na Rosemary Nyerere, Nimrod Mkono, Willibrod Slaa, Dk. Masumbuko Lamwai na wabunge wawili kutoka Zanzibar, ilishaundwa na kufanya kazi yake kuhusiana na uanzishwaji wa mahakama hiyo hapa nchini, hivyo kuitaka serikali itamke imegundua nini baada ya tume hiyo kuwasilisha ripoti yake.

Kwa upande wake, jana Mchungaji Mtikila aliionya radio hiyo na kuitaka kuacha kuendelea kurusha vipindi hivyo na kusema iwapo itaendelea kufanya hivyo, ataifunga kwa kutumia mahakama.

Alisema vipindi vya aina hiyo vinachochea uharibifu wa amani nchini na akatoa mfano kuwa Radio ya Sauti ya Injili iliyokuwapo nchini Ethiopia, ilifungwa kutokana na kuendesha vipindi vya aina hiyo.

Katikati ya wiki iliyopita, Mchungaji Mtikila alifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam akipinga uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi Tanzania.

Mwanasiasa huyo machchari anataka mahakama itamke kuwa kujihusisha kwa namna yoyote kwa Wizara ya Sheria na Katiba, Tume ya Kurekebisha Sheria na Bunge kwenye masuala yanayohusu Mahakama ya Kadhi ni kinyume cha Katiba ya Tanzania.

Pia anaomba mahakama itamke kuwa uanzishwaji wa mahakama hiyo au mfumo wa sheria wa makundi katika jamii ya Tanzania, unakwenda kinyume cha Katiba, na wote wanaojihusisha na utaratibu huo wachukuliwe hatua.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.