Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Warioba siyo msemaji wa Mkapa wala serikali.
http://www.habaritanzania.com/articles/4218/1/Warioba-siyo-msemaji-wa-Mkapa-wala-serikali.
By Nthelezi Nesaa
Published on 10/22/2007
 
Hakuna ubishi kuwa nchi yetu imo matatani. Wala hakuna ubishi kuwa ufisadi upo tena kwa kiwango kikubwa. Ushahidi upo hata kama kuna watu wanaupuuzia. Nani haoni wanasiasa wanavyotajirika ghafla bila hata maelezo wala stahiki? Huyu ni kipofu hata kama ana macho.

Hakuna ubishi kuwa nchi yetu imo matatani. Wala hakuna ubishi kuwa ufisadi upo tena kwa kiwango kikubwa. Ushahidi upo hata kama kuna watu wanaupuuzia. Nani haoni wanasiasa wanavyotajirika ghafla bila hata maelezo wala stahiki? Huyu ni kipofu hata kama ana macho.

Leo safu hii inataka kudurusu tamko lililochefua wengi la jaji Joseph Sinde Warioba. Hauna ubishi kuwa Warioba ni mmojawapo wa viongozi adimu waadilifu iliobaki nao Tanzania. Lakini kutokana na mwelekeo alioamua kuuchukua kwa sababu anazojua mwenyewe, usafi wake unaanza kutia shaka. Je ni msafi kweli au ni kwa vile yake hayajulikani kama yapo? Je kwanini ameamua kujipinga? Kuna nini hapa?

Kwa mtu anayemjua vizuri Warioba, baada ya Mwalimu Nyerere ni mtu pekee aliyekuwa angalau na uthubutu wa kukemea rushwa. Sasa hii imebakia kuwa historia. Maana kwa tamko lake la hivi karibuni rekodi yake imeingia doa.

Ingawa wengi wameishaandika juu ya kadhia hii, safu hii bado haiamani kuwa Warioba angeweza kujichafua kama alivyofanya. Ila kwa vile ni mwanadamu tena mwanasiasa huwezi kushangaa sana. Maana waingereza husema, you can trust everybody but not a politician. Hatujui sababu za hitimisho hili.

Kwanza Warioba anapaswa kufahamu kuwa pamoja na usafi na umaarufu wake, hawezi kutoa jibu lenye kukidhi kutokana na ufisadi uliotamalaki. Hii kazi wangeachiwa Rais Jakaya Kikwete na watuhumiwa wote.

Je ni kwanini Warioba licha ya kujichafua ameamua kuwasaliti wananchi na kupinga msimamo wake? Wapo wanaosema ametumwa. Wapo wanaosema amepewa kitu. Na wengine wamefikia kusema kuwa uzee ndiyo unaaza hivyo. Je Warioba anaanza kukukumbwa na hali inayomkumba babu yetu mzee Kingunge Ngombale Mwiru ambaye umma haumpi uzito kutokana na umri wake? Je ni kweli Warioba ametumwa, na nani? Je anayotaka kuyatetea yanaweza kutetewa? Je jibu alilotoa ni sahihi?

Huwezi kuwashauri wananchi wazalishe ilhali shambani wamejaa nguruwe wala mazao wakakuelewa? Huwezi kuwaambia wananchi kuwa washikilie kilimo kilichouawa na utawala wa kichuuzi wakakuelewa wala kuendelea kukuheshimu. Huwezi leo kumtetea Mkapa akawa safi kutokana na mazonge yanayomkabili. Huwezi kumtetea Kikwete akarudisha imani ya wananchi bila kupambana na ufisadi wala kutimiza ahadi alizotoa.

Huwezi kuwanyamazisha wananchi wasihoji usafi au uchafu wa watawala wao wanaoimba haki na uadilifu majukwaani nyuma ya pazia wakacheza dhuluma na ufisadi. Huwezi. Ukiweza utajiridhisha kuwa umeweza. Lakini ukweli unakuwa pale pale kuwa umma unataka maelezo yanayoingia akilini. Umma unataka matendo na siyo maneno. Umma unataka jawabu na siyo hoja za kupotosha.

Kama Warioba ameona ni bora ajigeuze msemaji wa watuhumiwa,serikali na hata Mkapa hao wanaolipwa kwa kazi hiyo watafanya kazi gani? Je serikali imekuwa ya hovyo kiasi cha kushindwa kuwatetea watendaji wake? Mkapa anafahamika kuwa hawezi kujibu kwa vile hana la kujibu bali kuomba ima umma usahau au umsamehe kwa uchafu anaoshutumiwa kuutenda.

Leo hata angekuja malaika hawezi kutetea serikali isiyokuwa tayari kujitetea na kujirekebisha akafanikiwa. Hivyo wanaojidanganya kuwa wanaitetea serikali hawaisaidii bali kuzidi kujenga dhana na maswali mbali mbali. Ingekuwa vizuri kama Rais angejitokeza;
Mosi akajitetea na kuwaamuru watuhumiwa wajitetea wenyewe.

Pili akavunja baraza la mawaziri na kulisuka upya.

Tatu akaanza kupambana na rushwa kwa vitendo badala ya maneno.

Nne akaanza kutekeleza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchanguzi.

Na mwisho akawajibika kwa umma huku akiwawajibisha wote wanaotuhumiwa ili mahakama iwasafishe. Vinginevyo siasa na urongo unaoingizwa kwenye kashfa hizi ni kuzidi kuitia serikali kwenye matatizo.

Watanzania wamekuwa wavumilivu mno. Huwezi kuwambia kitu wakakuelewa iwapo pale Mwananyamala wanalazwa watatu kitanda kimoja. Hawawezi kukuelewa iwapo ziara za nje tena nyingine zisizo na ulazima zinafanikiwa kwa kodi yao.
Hawawezi kumuelewa mtu hata awe maarufu kutokana na kutaka kupindisha hata kuficha ukweli wanaoushuhudia kila siku.

Hawawezi kumuelewa iwapo watendaji wengi wa serikali wanajulikana historia zao chafu na utendaji mbovu. Hivi kwa mfano nani anaweza akamsafisha waziri kama Andrew Chenge aliyetoa ushauri mbovu kwa serikali ya awamu ya tatu kwenye uwekezaji?

Nani anaweza kumsamehe waziri kama Nazir Karamagi anayetishia kwenda mahakamani huku ushahidi wa mazingira uko wazi kuwa mkataba aliosaini huko Uingereza hauna maslahi kwa umma?

Nani atakuelewa iwapo maisha kila siku yanazidi kuwa magumu huku serikali ikisema uchumi unakua? Je uchumi unakuwa kwenye makabrasha na takwimu au kwenye maisha ya kila siku ya mwananchi? Kama unakua kwa upande wa serikali huku kwa wananchi ukiendelea kuporomoka, je uchumi upo kwa ajili ya serikali au wananchi? Nani atakuelewa iwapo wananchi wanashuhudia madini yetu,pesa, hata michanga vikitoroshwa kila siku?

Nani atakuelewa iwapo kila siku anasoma taarifa za unyanyasaji na ubaguzi vinavyofanywa na wawekezaji? Nani atakuelewa iwapo kuna ndoa ya wazi ingawa ya mashaka baina ya watendaji wa serikali na wawekezaji?

Nani atakuelewa iwapo kashfa zinaongezeka kila uchao? Nani atakuelewa iwapo utegemezi kwa wafadhili unaongezeka? Nani atakuelewa iwapo mwelekeo wa nchi unabakia kuwa kitendawili?

Kwa mtu anayejua hali ilivyo nchini hana haja ya kujaribu kujaza maji kwenye gunia au hata kujaribu kukojoa baharini akidhani anaongeza ujazo wake. Kwa mtu anayeipenda nchi yetu kweli kweli aseme ukweli kuwa mambo yanaenda kombo. Aseme ukweli kuwa kujuana kumechukua nafasi ya maadili kiasi cha nchi kuanza kuelekea kwenye maangamizi. Maneno ya watu maarufu hayawezi kutatua matatizo ya wananchi wala kuzima hasira yao.

Hivyo basi yeyote kama Warioba mwenye mawazo ya kutusaidia siyo acheze mchezo wa mbuni kumuona adui akaficha kichwa chake au mkwezi kusingizia mwezi.

Watanzania wanataka majibu yenye kuleta suluhu badala ya kuwazidishia mkanganyiko na visingizio. Ni wakati muafaka kwa Rais Kikwete kujibu swali gumu kuhusiana na mstakabali wa nchi yetu kwenye lindi hili la tuhuma hata uwepo wa ufisadi. Mungu wajalie taamuli watawala wetu hata marafiki zao wawasaidie badala ya kuwaongozea mzigo.