Neno familia linaweza kutafsirika kutokana na mahali alipo mtu. Ukiongelea wazungu ni baba mama na mtoto au watoto. Ukiongelea waafrika ni zaidi ya hapo. Hata ukoo unaweza kuwa familia kama unaishi pamoja kwa misingi sawa kama ilivyo kwenye darasa la leo.
Katika kuadhimisha miaka nane ya kifo cha mwanzilishi wa taifa letu, safu hii imechukua mwelekeo tofauti na wa walio wengi.
Kwanza imeachelewa ili kuacha wengine wajadili. Wengi wameongelea maisha ya mwalimu tangu kudai uhuru, urais, ustaafu na hatimaye kifo. Wengi tena wazito wamemjadili gwiji huyu. Wamemuangalia katika nyanja tofauti hasa kitaifa na kimataifa wakiusuta utawala wa sasa kukiuka miiko na uadilifu alivyoacha nyuma mwalimu.
Tofauti na wengi, darubini inamulika ukoo wake ambao katika maadhimisho haya umeripotiwa kuwa taabani kiuchumi utadhani ndugu yao hakufanya kazi yoyote tena ya maana kwa taifa!
Mwalimu angeamua kuwa kibaka au fisadi, bila shaka angecha utajiri chekwa wa vitu. Lakini hakufanya hivyo. Kwake hili lilikuwa ni upuuzi na jinai. Aliwaachia tunu ya jina zuri lenye thamani na maana kuliko vitu chekwa. Aliacha utu na tabia njema. Ndiyo maana ndugu zake hawakuona aibu kusema kuwa tangu mwalimu atutoke maisha yao yamedhoofu.
Ujumbe wao licha ya kuwa aibu kwa taifa ni suto kuwa taifa letu linasahau haraka. Haimaanishi kuwa ndugu wa mwalimu hawawezi kujitegemea. Hasha. Wanafanya kila wawezalo, wanashindwa kutokana na ukubwa wa majukumu aliyowaachia. Wanashindwa kutokana na dhima na utu uliojichimbia mingoni mwao. Wangeweza kusema, "Kila mmoja kivyake vyake potelea mbali." Wangeweza hata kulitumia vibaya jina la Mwalimu. Lakini hawawezi kufanya hivyo kutokana na hulka waliyorithi kwa mwalimu. Wanagawana kidogo wanachopata kihalali. Hawafichi udhalili na utepetevu wao.
Mama Maria aliwahi kusema kuwa anajihisi kuelemewa na mzigo kutokana na kutegemewa na watu wengi. Ni kweli anategemewa na wengi hasa watoto. Maana kwa mwalimu watoto hawakuwa wale wa kuzaa bali watoto wote. Alipenda kuwapa watoto wote alichowapa watoto wake. Ndiyo maana katika watoto wa mwalimu hakuna milionea wala profesa. Angeweza kuwadhulumu wengine kuwasomesha na kuwapa mitaji watoto hata jamaa zake. Angeweza kutumia madaraka yake na ushawishi wake kuwapatia nafasi kwenye kamati zenye ulaji chamani mwake hata kwenye taasisi zinazolipa vizuri. Lakini hakufanya hivyo. Kwake huu ulikuwa huu ulikuwa ni ufisi na upanya. Hakuwa fisadi na mpenda mtumwa wa vitu na madaraka hivyo. Hakika ni tunu iliyotukuka.
Twende kwenye hali ya ukoo wa mwalimu. Ukoo huu una haki ya kusaidiwa kutokana na mchango adimu na adhimu alioutoa baba na ndugu yao. Waafrika huzaa na kulea kama akiba ya baadaye. Ninakufaa leo unanifaa kesho.
Hivi marais kama Benjamin Mkapa (mstaafu), Yoweri Museveni rais (Uganda), Joseph Kabila (DRC), Jakaya Kikwete (Tanzania) na watu kama Salim Ahamed Salimu,Cleopa Msuya (mawaziri wakuu wa zamani), Ali Hassan Mwinyi (mstaafu) hata rais Karume, wanajisikiaje kupokea taarifa hizi?
Hakuna kitu kibaya kama kuiba fadhila zitokanazo na matendo ya haki yatokayo rohoni. Safu hii inammurika Mkapa ambaye alifanikiwa chini ya mwalimu kuliko hata watoto wake na watu wengine waliofanya kazi na mwalimu.
Licha ya kuwa mwalimu wake, mwalimu alikuwa mlezi na manju au kungwi (Mentor) wake. Alimchukulia kama mwanaye wa kuzaa. Alimwamini na kumpandisha hadi akafika ambako hata hakuwahi kuota kufika. Kama siyo Nyerere, Mkapa angeupata wapi na vipi urais. Bado tunakumbuka alivyomhangaikia Mkapa mwaka 1995 hadi akaambiwa anahangaikia kinyago chake cha mpapure. Hii siyo kumtukana wala kumdhalilisha Mkapa. Yalisemwa na kila mmoja anajua hivyo.
Hata kama Mkapa alimwangusha mwalimu kwa kupiga mashoka yale aliyosimamia kama usafi, maendeleo kwa watanzania, kutunza raslimali za umma na kutenda haki. Lakini Mkapa angalau anapaswa na kuwajibika kuwa mmojawapo wa wana ukoo wa Nyerere si kwa maneno bali kwa matendo. Hivyo hali mbovu ya wanaukoo wa Nyerere ni suto na ukumbusho kwa Mkapa kuwa amekula fadhila.
Mkapa siyo mtu maskini. Kama ameweza kuwasaidia shemeji zake na watu baki anashindwa nini kuwajibika vilivyo kwa ukoo wa mwalimu? Tunasikia habari za ANBEN ambazo ni ukweli kuwa ina pesa na inafanya biashara tangu Mkapa akiwa ikulu. Kwanini Mkapa asichukue kiasi kidogo akawaokoa ndugu wa mwalimu. Hawahitaji mabilioni. Kwa kampuni yenye mamilioni ya dola kutoa hata dola laki tano kwa mwaka siyo hasara kwa ndugu wa mtu aliyekuwezesha kupata hayo yote.
Nyerere angekuwa hai hawa watu wasingekuwa wanalalamika na kuteseka na angeeendelea kuwatunza ili kuwafundisha uandilifu na usawa. Kama alivyogawana nao vya ujanani angegawana nao uzee wake. Na hakufanya hivyo kuwaendekeza bali kuionyesha dunia jinsi kiongozi wa watu anavyopaswa kuishi. Hakulia chumbani au kwenye vikuta. Hakula vinono na mkewe huku waliomzunguka wakilalia makande. Alikula kila kilichopatikana nao kwa sawa. Je sisi jeuri ya kufakamia vitamu vyumbani tukiwaacha ndugu zetu inatoka wapi?
Inatia kinyaa kusikia kuwa rais Kikwete ana mpango wa kupeleka mahujaji watano kuhiji ilhali ukoo wa mwalimu unakosa hata nauli ya kumpeleka dada yake hospitali. Hijja si jambo baya. Lakini tumeambiwa tuende baada ya kuhakikisha kuwa majirani zetu na ndugu zetu hawalali njaa. Je kuna ndugu wa rais Kikwete kama ukoo wa mwalimu? Hata kama mwalimu, kwa busara aliyoijua alimzuia Kikwete kugombea mwaka 1995 ili akomae nakugombea 2005, bado kama rais wa taifa aliloanzisha mwalimu anawajibika. Hakuna mjadala. Hata rais angekuwa ni Augustine Mrema aliyempiga na kumsababishia "kushindwa" mwaka 1995, tunaamini asingewaacha ukoo wa mwalimu.
Wahusika wanaweza kusema hawakuwa na taarifa ya haya. Hii maana yake ni kwamba hawana mawasiliano na ukoo wa mwalimu. Mbona alipokuwa hai nyumbani kwake ilikuwa Makka yao kila yalipowakuta? Nani amesahau alivyoikoa CCM Zanzibar mwaka 95? Leo CCM ina pesa ya kuharibu kuwatuma mawaziri na matapeli wa kisiasa mikoani kuzomewa lakini inashindwa kuisaidia familia ya mwalimu? Tukumbuke na kukengeuka. Kama siyo mwalimu CCM ingekuwa madarakani hadi leo miaka yapata 50 baada ya uhuru. Kaulize Zambia, Kenya,Malawi, Senegal, Sierra Leone na kwengineko yaliyowakuta wenzenu.
Hiyo haki na maisha bora vinavyonadiwa na CCM viko wapi? Mnapata wapi moyo wa kusamehe hata wawekezaji matajiri ilhali ukoo wa mwalimu ukiteseka? Maskini hata mpishi wake ambaye angetumiwa na mabepari kumuulia mbali mwalimu naye tunaambiwa anateseka akiishi kwa hisani? Yuko wapi dereva wake? Wakati maofisini watu wanachezea simu na umeme tena bila kuilipa TANESCO eti dada yake kipenzi amefia kizani!
Tukubaliane. Bila tabia adilifu ya mwalimu hizi mali na pesa tunazotanulia wengi wasingezipata hasa walioko madarakani. Je tumegeuka wa hovyo kama mbwa ambaye licha ya kupikiwa na kushibishwa nyumbani haachi kwenda jalalani na asimuite mwenzie?
Ili wahusika wajue wazungu waitacho the right thing to do, wajalie wangekuwa wao ndiyo mwalimu wangefanya nini? Kwanini kwenda kutoa sadaka misikitini na makanisani ilhali ndugu na jirani zako wako hoi? Au ni yale yale ya mafarisayo na masadukayo.
Jamani ANBEN, TanPower, kasi mpya na wengine aibu hii ni yenu. Safu hii itafuatilia hata kama iko mbali. Kama mtaendelea kutia nta masikioni kama mbu itawaghasi hadi kieleweke. Waswahili husema, akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli, udugu si kufanana bali kufaana na mwisho, leo kwangu kesho kwako. Nani anajua?