Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Mbunge mwingine aingia matatani
http://www.habaritanzania.com/articles/4215/1/Mbunge-mwingine-aingia-matatani
By Marshy Abdu
Published on 10/20/2007
 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Ilabila Industries Ltd ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Momose Cheyo, akamatwe.

Mbunge mwingine aingia matatani
na Happiness Katabazi


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Ilabila Industries Ltd ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Momose Cheyo, akamatwe.

Amri hiyo imetolewa Oktoba 12 mwaka huu na Hakimu wa Mahakama hiyo, Catherine Revocat. Alisema ametoa amri kwamba Cheyo akamatwe na afikishwe katika mahakama hiyo kwa ajili ya kujieleza ni kwanini asifungwe kwa kushindwa kutekeleza amri ya Baraza la Nyumba la Mkoa wa Mwanza.

“Naamuru Cheyo akamatwe mara moja, afikishwe mahakamani hapo ili ajieleze mbele ya mahakama hii kwanini asifungwe kwa kushindwa kutekeleza amri ya Baraza la Nyumba la Mkoa wa Mwanza,” alisema Hakimu Revocat.

Baraza hilo lililokuwa chini ya Mwenyekiti Msaidizi S.T. Kessy, Mei 20 mwaka 2003, katika maombi namba 39 ya mwaka huo yaliyowasilishwa na Alex Banturaki dhidi ya Kampuni ya Ilabila Industries Ltd, alitaka alipwe sh 3,704,000 zinazotokana na malimbikizo ya ankara ya maji, simu na umeme.

Kwa mujibu wa hati ya madai, kampuni hiyo iliingia mkataba na mwenye nyumba ambaye ni Banturaki ili wampangishie Cheyo nyumba hiyo iliyopo Mwanza mjini.

Kwa mujibu wa uamuzi wa baraza hilo lililokuwa likiongozwa na Mwenyekiti Msaidizi S.T. Kessy, Mei 20 mwaka 2003 , liliamuru kampuni hiyo kulipa kiasi hicho cha fedha na Cheyo aondolewe katika nyumba hiyo ya mlalamikaji na ilipe gharama za kesi.

Na tangu hukumu hiyo itolewe hadi sasa, kampuni hiyo haijatekeleza hukumu hiyo hadi sasa na kisheria mlalamikaji anatakiwa kutafuta mali za mdaiwa zilipo na kubainika kuwa mali zake nyingi ziko Dar es Salaam.

Wakili wa mlalamikaji, Thomas Brash kutoka Kampuni ya wakili ya Rutabingwa, alieleza kwamba waliandika barua Juni 23 mwaka 2004 kwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza wakiomba ruhusa ya taratibu za kukaza hukumu hiyo zifanyike jijini Dar es Salaam kwa sababu ni mahali ambapo mdaiwa anaweza kupatikana na mali zake.

Ombi hilo lilikubaliwa na kufunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na tangu Januari 17 mwaka jana, mahakama hiyo imekuwa ikitoa amri ya kukamatwa kwa mbunge huyo zaidi ya mara 15 bila mafanikio na hadi jana saa 9 alasiri alikuwa hajakamatwa.

Wakati huo huo, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu kifungo cha miezi 18 nje, wakili wa kujitegemea, Gabriel Mnyere, kutokana na kosa la kumuua mkewe bila kukusudia.

Hukumu hiyo iliyovuta hisia za watu wengi, ilitolewa jana na Jaji Willian Mandia, baada ya kupatikana na hatia katika kosa hilo.

Wakili Mnyere, alikuwa akikabiliwa na shitaka la kumuua mkewe, Pamela Mnyere, Novemba 20, mwaka 2003.

Akisoma maelezo ya hukumu hiyo, Jaji Mandia alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani na upande wa mashitaka umethibitisha kuwa shambulio lililofanywa na mshitakiwa Novemba 10 mwaka 2003 katika ofisi yake dhidi ya mkewe ndilo lililosababisha kifo chake.

Alisema mahakamaa imeridhika kuwa mshitakiwa alikuwa na kinyongo na marehemu na kwamba kulikuwa na matumizi ya nguvu dhidi ya marehemu.

“…na ndiyo maana sababu ya kifo haikujulikana na hakuna daktari aliyethibitisha chanzo ch kifo hicho hadi uchunguzi wa mwili wa marehemu ulipofanyika.

“Mahakama imemtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, hivyo inakuhukumu kifungo cha miezi 18 nje na ukiwa kwenye kifungo hicho hupaswi kutenda kosa lolote la jinai, vinginevyo utakwenda jela moja kwa moja,” alisema Jaji Mandia.

Katika usikilizaji wa kesi hiyo, upande wa utetezi ulipeleka mashahidi wawili na upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi wane, akiwemo mtaalamu wa uchunguzi wa vifo, Dk. Adam Mwakyoma, kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Katika ushahidi wake, Dk. Mwakyoma, alieleza kuwa alipoufanyia uchunguzi mwili huo aligundua ulikuwa na mikwaruzo eneo na shingo na kidevu, mkono wa kulia na majeraha katika mguu wa kushoto.

Alieleza alipomfanyia uchunguzi kwa ndani alibaini ubongo wa marehemu ulikuwa umevimba na unatoa maji, na kwamba nyuma ya fuvu kulikuwa na mpasuko. Alieleza kuwa vitu vyote hivyo ndivyo vilivyosabaisha kifo cha marehemu.

Pia, alisema katika uchunguzi alibaini marehemu alikuwa na uvimbe kwenye kizazi na mapafu yalikuwa yamevimba, na kueleza kuwa hali hiyo si sababu ya kifo hicho.

Hata hivyo, Jaji Mandia alikataa ushahidi wa dereva na walinzi wawili waliombeba marehemu kutoka katika ofisi ya mshitakiwa kumpeleka Hospitali ya Dar Group.

Mashahidi hao waliieleza mahakama kuwa wakiwa nje, walisikia marehemu akimpiga mshitakiwa na pochi, na jaji kueleza kuwa wakati marehemu anatolewa kwenye ofisi ya mshitakiwa hakuwa na nguvu, hivyo isingekuwa rahisi kumpiga na pochi mshitakiwa.

Akijitetea, wakili Mnyele, aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio, saa 12 jioni, mkewe alimfuata ofisini kwake na kumtaka waende Baa ya Hugo kunywa bia.

Alieleza wakiwa huko walikuwa wakizungumza masuala ya kifamilia, na baada ya muda mfupi mkewe alimweleza kuwa alipigiwa simu na kuelezwa kuwa mumewe ana wanawake wengine ofisini.

Mnyele, aliendelea kueleza kwamba hata hivyo alikanusha tuhuma hizo, lakini mkewe aliendelea kusisitiza kuwa ni kweli na kumtaka warejee ofisi wakapekue.

Akiendelea kujitetea, Mnyele aliiambia mahakama kuwa alipingana na mkewe kwa kuwa alikuwa ameshafunga ofisi. Mkewe alimweleza alikuwa amepigiwa simu na mtu aliyemweleza kwamba ana wanawake wengine ofisini, hata hivyo mkewe aliingiza mkono kwenye mfuko wa shati alilokuwa amevaa na kumpora funguo.

Alieleza hata hivyo mkewe alipokwenda hakufanikiwa, na ndipo aliporejea katika baa hiyo huku akitoa maneno ya kashfa dhidi yake na kueleza kuwa hali hiyo ilimfanya akubali kwenda kufungua ofisi na kupekua bila mafanikio.

Wakili Mnyele, alieleza lengo la mkewe liliposhindikana ndipo alipoanza kumrushia vitabu usoni na stuli, lakini akawa anamzuia.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mawakili waliokuwa wakimtetea Mnyele, Mabere Marando na Deogratius Lyimo, waliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mteja wao ambayo itamwezesha kufanya kazi, ili aweze kutunza familia, kwani ana watoto wanne wanaomtegemea, ambao hawana mama. Pia mshitakiwa ni mgonjwa wa kisukuri na shinikizo la damu.