MAISHA ya mwanamuziki maarufu wa reggae, Lucky Philip Dube, yalikatishwa ghafla juzi kwa kuuawa kwa risasi na watu wasiojulikana.
Kifo cha mwanamuziki huyo aliyekuwa na umri wa miaka 43, kilitokea katika kitongoji cha Rosettenville kilichopo kusini mwa Jiji la Johannesburg, majira ya jioni.
Habari za kipolisi kutoka Afrika Kusini zinasema kwamba kabla ya kuvamiwa, Dube alikuwa na mtoto wake wa kiume aliyekuwa akiteremka kwenye gari la kifahari. Halikulezwa.
Taarifa hizo zinasema kwamba kijana huyo baada ya kuona watu hao wakimvamia baba yake alikimbia mbali ya tukio na kuomba msaada kabla ya watu hao kutoweka na gari hilo.
Hakika kifo chake kimehuzunisha mashabiki wengi wa muziki wa reggae duniani, kwani alikuwa mmoja kati ya wanamuziki walioweka historia ya kuutambulisha muziki huo nje ya bara la Afrika.
Dube anatajwa kama msanii wa kwanza wa Afrika Kusini kuachia CD nyingi zaidi na nzuri na zenye ubora kuliko mwanamuziki mwingine yeyote wa nchini humo. Alizaliwa Agosti 3, 1964.
Katika uhai wake mwanamuziki huyo alifanikiwa kutengeneza jumla ya albamu 20 zilizokuwa katika lugha ya Kizulu, Kiingereza na Kiafrika. Pia aliwahi kutwaa tuzo 20.