Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Wanaharakati jitokeze shitaki familia ya Mkapa
http://www.habaritanzania.com/articles/4213/1/Wanaharakati-jitokeze-shitaki-familia-ya-Mkapa
By Nthelezi Nesaa
Published on 10/19/2007
 
Rais mstaafu Benjamin Mkapa amekuwa bubu ghafla baada ya kuondoka madarakani! Hakuna aliyetegemea kuwa Mkapa bingwa wa kuandika hotuba ndefu na kuzodoa wapinzani wake angefikia hatua hii! Hakuna aliyetegemea Mkapa bingwa wa kujua kila jambo angedondoka chali hivi!



Rais mstaafu Benjamin Mkapa amekuwa bubu ghafla baada ya kuondoka madarakani! Hakuna aliyetegemea kuwa Mkapa bingwa wa kuandika hotuba ndefu na kuzodoa wapinzani wake angefikia hatua hii! Hakuna aliyetegemea Mkapa bingwa wa kujua kila jambo angedondoka chali hivi!

Kweli nguo ya kuazima haisitiri maungo. Safu hii ni katika wachambuzi wa kwanza kumtolea uvivu Mkapa kuwa ajieleze. Maana mali anazodaiwa kujipatia akiwa kwenye ikulu ya wananchi ni za wananchi pia. Pia hata hao anaowadharau kiasi cha kukataa kutoa maelezo juu ya tuhuma zake ndiyo waliomuwezesha kufikia hapa alipofikia ingawa alipachafua.

Sasa kuchele waswahili husema. Wale wanaomjua kuliko hata wananchi wamejitokeza kumshauri afanye jambo la kiutu uzima. Kwenye kumbukumbu ya miaka minane ya kifo cha Mwalimu Julius Nyerere, watu wazito wawili wanaoheshimika sana nchini Ali Hassan Mwinyi na Joseph Butiku waliamua kuungana na wananchi kuwataka watawala wafanye yapaswayo kufanya kama walivyoahidi.

Mwinyi aliutaka utawala wa sasa kuacha visingizio na ujanja ujanja bali upambane na rushwa vilivyo.

Mada ya leo itatuama kwa Mzee Butiku ambaye licha ya kumshukuru tunampongeza kwa kutofanya unafiki kama baadhi ya wakubwa wamekuwa wakifanya. Butiku ameamua kupingana na rais Jakaya Kikwete ambaye alisema hana mpango wa kumfungulia mashitaka wala kumchunguza Mkapa kana kwamba pesa inayodaiwa kuliwa na Mkapa kwenye mradi wa Kiwira ni yake!

Sasa tuliishaambiwa kuwa Mkapa yuko juu ya sheria na inamlinda kama rais mstaafu ingawa hata sheria yenyewe ikichunguzwa na kutafsiriwa vizuri haimlindi kwenye makosa ya jinai ya kibinafsi kama wizi na ufisadi.

Watu wazima wenye akili bado wanajiuliza. Je na mshirika na mke wake Anna Mkapa ambaye ni mkurugenzi mwenza kwenye kampuni inayolalamikiwa ya ANBEN yenye kumaanisha Anna and Benjamin naye analindwa na sheria ipi?

Na huyo mtoto wao Nicholas Mkapa na Mkewe Foster Nicholas wakurugenzi wa kampuni itokanayo na ushawishi wa wazazi wao ya Fosnik nao wana kinga gani kwa kazi gani kwa taifa zaidi ya kulihujumu?

Pia anatajwa Daniel kwenye "dili" jingine la kampuni iitwayo TanPower ambayo kwa kushirikiana na Mkapa na Mkewe waliiunda na kujipatia mradi wa makaa kule Kiwira wakatumia vyeo vyao kuibambika mkenge Tanesco, shirika la umeme la taifa kiasi cha kujipatia tenda ya kuliuzia umeme kwa bei ya kulangua. Je na Yona anayo kinga gani na kwa kazi gani?

Tukijitenga na unafiki na roho chafu za kupenda rushwa na kulindana, kuna haja ya wanaharakati wa kisheria kama Kituo cha haki za binadamu cha Dar es salaam (Legal and Human Rights Center (LHRC), National Organisation for Legal Assistance (NOLA), TGNP na wengine kujitokeza na kuzishitaki familia za Mkapa na Yona.

Tumetoa ushauri huu kwa wadau hawa kutokana na kazi yao nzuri na pevu ya kukemea hata na kupambana na uoza katika nchi yetu. Nani mara hii amesahau jinsi NOLA ilivyoiporomosha sheria chafu ya mgombea binafsi?

Wahusika wanapaswa kufanya hivi kutokana na ukweli kuwa serikali iliyopo haina tofauti na iliyopita wala haina uadilifu bali kucheza mchezo ule ule.

Tukirejea kwa Butiku, kwanza ni mwanachama mzuri na mwanzilishi wa CCM ambaye anaijua nje ndani kuliko hata Mkapa na Kikwete walioingia chamani kikiwa kimeishakuwa na mafanikio.

Hebu tuangalie nukuu yake moja kali. "….Mkapa ameruhusu Ikulu kuwa mahali pa walanguzi na wanyang’anyi, hata yeye alipageuza kuwa eneo la biashara…Ikulu ni mahali patakatifu, kila mtu anayeingia pale anakula bure na kulala bure, lakini sasa pamechafuka….. tushirikiane sasa kurejesha heshima, tusiogope kuwaambia viongozi ukweli, wanaoogopa ndio wabaya na Mkapa ajitokeze ajieleze wazi ni namna gani aligeuza Ikulu kuwa mahali pa walanguzi," alisema Butiku.

Nukuu hii inaweza kuandikiwa kitabu kwa mtu anayejua nchi yetu ilivyonajisiwa na kudhulumiwa. Watu wamekuwa wakihoji usafi wa Mkapa na Kikwete. Wahusika wamejitahidi kujirusha na kujifanya kama hawasikii. Sasa watu wenye sauti wameamua kusema na inavyoonekana wataendelea kusema.

Mwalimu Nyerere alipokuwa ikulu si yeye wala mkewe walijiingiza kwenye umachinga wowote. Hata mzee Mwinyi hakufanya uchafu huu ingawa kuliwahi kutokea shutuma za bi mkubwa wake kutoa vimemo.

Lakini alipoingia Mkapa na mkewe msaka mali, mara wananchi tukashangaa kusikia EOFT ambayo wajanja huiita Economic Opportunity for the First-lady. Wenye kujua miiko ya uongozi tulishangaa na kuchelea hatari ya ofisi ya rais kuanza kutumiwa kuchumia pesa chafu na watu binafsi hasa familia ya rais.

Baada ya kampuni hii ya mama kuanzishwa, wafanyabiashara wenye mabaka wengi wakiwa majambazi hata wakwepa kodi wangeweza kuitumia kupata upendeleo na ushawishi kwa mzee.

Kutokana na Mkapa wakati wa utawala wake kupenyeza wahariri wengi wanaojikomba ili kupewa madaraka au mabaki toka meza ya bwana mkubwa, ilikuwa vigumu kwa magazeti mengi kushupalia jinai hii.

Waulize watanzania kama wanajua jinsi EOTF ilivyokuwa ikiendeshwa. Hawajui. Watajuaje wakati ilikuwa mali binafsi ya mke wa rais aliyejificha kwenye mgongo wa kutoa huduma kwa umma ilhali kuna wizara zilizoundwa kushughulikia hayo.

Kikwete alipoingia naye mkewe akaona hawezi kupitwa na ulaji rahisi kwa kutumia jina la rais. Aliunda WAMA ambayo siku inaanzishwa iliishapata misaada ya mamilioni! Safu hii iliandika makala kuuliza WAMA iliwezaje kupata pesa nyingi kufikia zaidi ya milioni 500 hata kabla ya kusajiliwa? Bahati mbaya hatukujibiwa.

Ukiangalia inachodai kufanya WAMA sawa na EOTFL ni kile kile kinachofanywa na wizara ya wanawake na watoto. Kimsingi kinachofanyika ni kuwatumia wanawake wa nchi yetu kuuibia umma.

Kwanini watu wanahoji hizi NGO? Ni kwa sababu mke wa rais hawezi kutaka mkopo au msaada akaukosa popote. Hii mara nyingi husababisha watoaji misaada au mikopo ambao ni wafanyabiashara kuutumia mwanya huu kupitisha mambo yao kama kukwepa kodi, kukwepa hata maofisa wa vyombo vya usalama na vile vinavyoshughulikia biashara na mambo mengine. Nani amesahau Gullamali wakati wa awamu ya pili alivyotumia ushawishi wake hata kupata ubunge ingawa alikuwa hafai?

Kamuangalia yule mhindi Raza aliyekuwa mpambe wa Salmin Amour. Baada ya Salimin kung’oka naye mbwembwe zake zimekwisha. Hii maana yake ni kwamba ufanisi wake ulikuwa unategemea ikulu ambayo kimsingi inalalamikiwa kuwa pango la wevi.

Siyo uzushi kwa mzee Butiku kusema kuwa ikulu sasa ni pango la wanyang’anyi. Hebu angalia tulivyogeuka vyangudoa wa kisiasa kiasi cha waziri mzima kuhongwa tiketi ya ndege na chumba hotelini kiasi cha kusaini mkataba wenye maslahi ya nchi hotelini!

Angalia jinsi serikali iliyopo inavyoelemewa na mizigo itokanayo na walafi wachache waliomo serikalini kutokana na kujuana na rais.

Je watu kama hawa ambao wengi wao wamethibitika kuwa wachafu, wanapoingia ikulu kwa madaraka yao siyo kuigeuza ikulu chaka la wezi? Anayeshuku hili ajiulize ni kwanini kwa sasa serikali imewatuma mawaziri mikoa yote kutetea ufisadi ambao kimsingi ungeshughulikiwa kwa kuwatimua watuhumiwa ili kuwapa fursa wakasafishwe na mahakama au tume?

Lakini nani amfukuze nani iwapo kilichopo ni sawa na wafu wawili wanaokokotana?

Kwa vile rais ameishajitoa na hataki kuokoa mali zetu wala kulinda heshima ya ikulu ya watanzania,wanaharakati wajitokeze na kutoa somo. Itasaidia kuepusha kuendelea kuwalelea wezi ndani ya ikulu yetu.
nesaa1977@yahoo.com