Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Mkapa: No way, nimeshastaafu
http://www.habaritanzania.com/articles/4212/1/Mkapa:-No-way,-nimeshastaafu
By Marshy Abdu
Published on 10/19/2007
 
RAIS wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ameamua kujiepusha kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake, kuhusiana na kile kinachodaiwa kuwa matumizi mabaya ya madaraka akiwa mkuu wa nchi na uongozi mbaya alipokuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkapa: No way, nimeshastaafu
na Tamali Vullu


RAIS wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ameamua kujiepusha kujibu tuhuma zinazoelekezwa kwake, kuhusiana na kile kinachodaiwa kuwa matumizi mabaya ya madaraka akiwa mkuu wa nchi na uongozi mbaya alipokuwa mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Jana, Mkapa alikuwa na nafasi ya kujibu tuhuma hizo zinazoelekezwa kwake kupitia vyombo vya habari, pale alipokutana na kundi la waandishi wa habari katika Hoteli ya Kunduchi Beach, alikokwenda kuhudhuria mkutano wa taasisi yake ya Mkapa Foundation.

Hata hivyo, alishindwa kuzima kiu ya waandishi, ambao wengi wao waliamini kuwa Mkapa atazungumzia tuhuma hizo, pale alipoeleza kuwa hawezi sasa kuzungumzia mambo hayo.

Hatua hiyo ya Mkapa inaweza kuonekana ni kukengeuka kwa hali ya juu kutoka katika sera yake aliyoiasisi akiwa madarakani ya ‘Ukweli na Uwazi’.

Hatua ya Mkapa kuamua kukaa kimya inakuja siku chache baada ya msaidizi wa karibu wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, kumwandama kwa shutuma nzito za kukiharibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuigeuza Ikulu kuwa pango la walanguzi.

Hata hivyo, katika kile kinachoonekana msimamo wake kutokana na tuhuma zinazoelekezwa kwake, akizungumza katika mkutano huo jana, alisema kuwa yeye hivi sasa ameshastaafu siasa. Hivyo hawezi kusema lolote.

Kauli hiyo ya Mkapa inatokana na pongezi zilizotolewa na mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo kwamba ana ujasiri pamoja na tuhuma zinazotolewa dhidi yake.

“No way, nimeshastaafu… sipo kwenye siasa,” alisema Mkapa kwa kifupi bila kufafanua na kufungua mkutano huo ambao yeye alikuwa mgeni rasmi.

Baada ya kumaliza kufungua mkutano huo, waandishi wa habari walitanda katika njia aliyokuwa apite Mkapa kuelekea kwenye chumba cha chai, hali iliyomfanya mmoja wa wasaidizi wake kuwaomba waandishi wa habari wapishe njia ili Mkapa apite.

Hata Mkapa alipoelezwa na mmoja wa wasaidizi wake kwamba waandishi wa habari walitaka kuzungumza naye, alimwelekeza mkurugenzi wa asasi hiyo kuzungumza nao.

Mkurugenzi huyo, Dk. Hellen Senkoro, alipokwenda kuzungumza na waandishi wa habari aliwaeleza kuwa mkutano huo si wa kisiasa na kwamba ulikuwa ukihusu masuala ya ukimwi.

Hivi karibuni, Butiku aliyekuwa mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Mwalimu Nyerere kwa zaidi ya miaka 20, alinukuliwa akisema CCM imepoteza dira na kwamba Agosti 10, mwaka 2005 alimwandikia barua Mkapa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Rais wa Tanzania, kumweleza kuhusu hali hiyo.

Butiku ambaye alisema aliamua kuifanya siri barua yake hadi hivi sasa anapoiweka hadharani, alimtaka Mkapa kuisoma kwa umakini barua yake yote, ili aweze kutambua kile alichokiona kuwa ni mpasuko mkubwa uliokuwa ndani ya chama hicho tawala.

Alieleza kuwa katika barua hiyo alimweleza kuhusu ubaguzi, rushwa na maovu ya CCM wakati wa mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2005 na kusema mpaka sasa barua hiyo bado ina maana, kwani mambo hayajabadilika.

Kama hiyo haistoshi, Butiku alilaumu jinsi Mkapa akiwa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho alivyomuengua mapema Makamu Mwenyekiti wake, John Malecela, ili asigombee, hatua ambayo ameielezea kuwa ilizusha mabishano aliyoyaita ‘aibu’.

Pia, mkurugenzi huyo alieleza wakati wa utawala wake, Mkapa alipafanya Ikulu, sehemu ya kufanyia biashara. Alieleza Mkapa aliruhusu Ikulu kuwa mahali pa walanguzi na wanyang’anyi, hata yeye kupageuza eneo la biashara.

Na kama ilivyoelezwa na mkurugenzi wa taasisi hiyo, akifungua mkutano huo jana, Mkapa alijizuia kabisa kuzungumzia masuala ya siasa.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, alisema taasisi hiyo imefanikiwa kuwapatia mafunzo watoa huduma za afya 99, ambao 69 kati yake wamepelekwa katika wilaya 23 kufanya kazi na 30 waliosalia Novemba mwaka huu watapelekwa katika wilaya 10 tofauti.

Alisema jihitada zote hizo zimefanikiwa kutokana na kupata ufadhili wa fedha kutoka Norway na asasi ya Bill Clinton Foundation na Serikali ya Tanzania.

Alisema masuala hayo pia yamefanikiwa kutokana na ushirikiano kutoka Halmashauri Kuu na mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na juhudi za Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Mkapa alisema kwa kuwa lengo la asasi hiyo ni kusaidia juhudi za serikali katika kupambana na ukimwi na kuondoa unyanyapaa, asasi hiyo inapaswa kuongeza juhudi za ushirikiano na serikali na asasi nyingine katika kuondoa unyanyapaa nchini.

Naye Dk. Senkoro, alisema katika nchi za Afrika bado kuna uhaba mkubwa wa watoa huduma za afya kwa wagonjwa na watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na pia waliopo ari ya kazi bado ipo chini.

Akielezea mafanikio ya asasi hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja tangu ianzishwe, alisema watu wamepatiwa mafunzo jinsi ya kutoa tiba za ukimwi na kwamba hivi sasa huduma kwa watu wenye VVU zinatolewa kwa uhakika.

Alisema hivi sasa hata watu waliokuwa mbali na huduma hizo, wamefikiwa na huduma hizo.

Hata hivyo, alisema changamoto iliyopo ni unyanyapaa miongoni mwa jamii na kusema kuwa ingawa watu wana uelewa kuhusu ugonjwa huo, lakini si wa undani zaidi.