MWENYEKITI wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila, amefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana, kupinga serikali kujihusisha na harakati zozote za kutunga sheria itakayohalalisha kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi nchini.
Pamoja na Mtikila, mlalamikaji mwingine katika kesi hiyo ya kikatiba iliyopewa namba 80/2007, ambayo hata hivyo haijapangiwa jaji wa kuisikiliza, ni Kanisa la Wokovu, analoliongoza mchungaji huyo.
Madai ya walalamikaji dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kuitaka mahakama kuzuia uwepo wa Mahakama ya Kadhi kisheria kwa sababu inakwenda kinyume cha Katiba ya Jamhuri.
Mbali na dai hilo la msingi, Mchungaji Mtikila pia amedai kuwa Mahakama ya Kadhi itachochea ugaidi na kuleta vurugu nchini na kuharibu utawala wa sheria au kuwagawa watu katika misingi ya dini.
Kwa madai hayo, Mchungaji Mtikila, aliiomba Mahakama Kuu kulizuia Bunge la Tanzania, kuidhinisha marekebisho ya sheria yatakayoruhusu uwepo wa Mahakama ya Kadhi yatakayofanywa na Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba, kwa kuwa ipo kwenye kitabu cha dini ya Kiislamu cha Kurani.
Katika maelezo yao, kanisa hilo na Mchungaji Mtikila wanaitaka mahakama kuilinda katiba ya nchi dhidi ya harakati zisizo za kikatiba zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne na Bunge, kuanzisha Mahakama ya Kadhi nchini.
Wanadai kuwa kufanya hivyo ni kukiuka katiba na wamezitaja ibara ambazo zitakiukwa kuwa ni 19, 107A, 3, 9a, f, g pamoja na h, na kuwa ukiukwaji wa ibara hizo unaweza kusababisha mapigano ya kidini nchini.
“Ibara ya 26(1) ya katiba inasema kuwa kila mtu atapaswa kuitii katiba hiyo na sheria nyingine, wakiwamo wabunge, rais na mahakama ambao wana kiapo cha kufanya hivyo,” wanasema.
Mtikila na kanisa hilo wanaeleza kuwa Mahakama ya Kadhi ni moja ya taasisi zinazotajwa ndani ya Kurani, hivyo serikali na Bunge haviwezi kuhusika katika uundwaji wake kama ilivyoelezwa katika ibara za 19 na 20(1) za katiba kuwa Tanzania si nchi ya kidini.
Wanadai pia kuwa kuanzishwa kwa mahakama hiyo, ambayo kimsingi itashughulikia masuala yanayowahusu Waislamu tu, kunakinzana na matakwa ya katiba ambayo inatambua usawa wa watu wote katika nchi.
Aidha, Mtikila anadai kuwa Mahakama ya Kadhi ni taasisi ya Kiislamu ambayo mkuu wake anapewa mamlaka ya kuamuru kuuawa kwa watu, wakiwamo Wakristo ambao wanaamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu.
Kutokana na hayo, Mtikila na kanisa lake wanaiomba Mahakama Kuu kuizuia serikali, kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, Tume ya Kurekebisha Sheria na Bunge kutojihusisha kwa namna yoyote ile na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.
Aidha, wanaitaka Mahakama Kuu itoe amri kuwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, au mfumo mwingine wa sheria ambao utawahusu baadhi ya watu, kuwa ni kinyume na katiba ya nchi.
Pia, wanaomba watu wote watakaohusika kukiuka katiba kwa kushiriki katika uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.