WIKI moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Kagera kutengua matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Phares Kabuye (TLP-Biharamulo Magharibi), balaa jingine linaelekea kuiangukia kambi ya upinzani, baada ya jana Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Kagera, kumkuta na hatia, aliyekuwa Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (CUF).
Lwakatare ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), alikutwa na hatia ya kosa la shambulio la kudhuru mwili baada ya kumkaba mwandishi na mpiga picha wa ITV, Renatus Mutabuzi.
Mbele ya umati mkubwa wa mashabiki wa vyama vya CCM na CUF waliozingira mahakama hiyo jana, Hakimu Mkazi Cleophas Waane, alisema Lwakatare alikutwa na hatia katika kosa moja la kumshambulia Mutabuzi na alikuwa akitarajia kuisoma hukumu yake hiyo leo saa 2:00 asubuhi.
Mwanasiasa huyo ambaye hadi hivi sasa ana ushawishi mkubwa wa kisiasa katika Jimbo la Bukoba Mjini, alishitakiwa kwa makosa mawili na akatiwa hatiani kwa kosa moja kati ya hayo.
Mahakama ilishindwa kumtia hatiani mwanasiasa huyo katika tuhuma za kuharibu vitendea kazi vya mwandishi wa habari aliyejeruhuwa wakati wa harakati za kugombea ubunge wa Bukoba Mjini mwaka 2005 ambao Lwakatare aliangushwa na Balozi Khamisi Swedi Kagasheki.
Katika shauri hilo ambalo mlalamikaji alikuwa ni Jamhuri, shahidi wa kwanza Mutabuzi aliwasilisha ushahidi wa hati maalumu ya polisi (PF3) iliyothibitisha kuwa alikuwa ameumizwa katika maeneo ya shingoni.
Aidha, Mutabuzi aliwaleta mashahidi wawili mahakamani hapo kuthibitisha kuwa alikuwa amepata maumivu hayo kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa Lwakatare.
Katika kesi hiyo, Lwakatare yeye alikuwa amewaleta mashahidi sita mahakamani hapo, ambao hata hivyo Hakimu Waane aliukataa ushahidi wao.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu kutoka Bukoba jana, Lwakatare alisema alikuwa akisubiri hukumu yake inayotarajiwa kusomwa mahakamani hapo leo hii.
Lwakatare ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa katika misafara ya vyama vikuu vinne vya upinzani vinavyoshirikiana, alisema, wakati Hakimu Waane akimtia hatiani jana, wakili wake Twaha Taslima anayemtetea, hakuwapo mahakamani hapo kutokana na kukosa ndege ya kumfikisha Bukoba.
Kwa mujibu wa Lwakatare, Taslima, wakili maarufu ambaye amekuwa akiwatetea viongozi mbalimbali wa CUF, alikuwa akitarajia kuwasili Bukoba jana jioni.
Habari zaidi kutoka Bukoba zinaeeleza kuwa kesi hiyo dhidi ya Lwakatare ambayo imevuta hisia nyingi kutoka kwa mashabiki wa CCM na wale wa CUF, imekuwa ikionekana kuchukua mwelekeo wa kisiasa zaidi kuliko kisheria.
Lwakatare alipoulizwa na Tanzania Daima jana kuhusu hali hiyo, alisema: “Siku mbili zilizopita mashabiki wa CCM walikuwa wakipita mitaani wakiimba, tumemmaliza Lwakatare. Sijui iwapo nyimbo hizo zilikuwa na uhusiano na kesi yangu hii, ingawa watu wengi wanafikiri hivyo.”
Baadhi ya wanasheria waliozungumza na Tanzania Daima walisema kuna uwezekano mkubwa kuwa kwa kosa alilofanya Lwakatare anaweza akahukumiwa kifungo kisichozidi mwaka mmoja jela, kinachoweza kwenda pamoja na kulipa faini au kutozwa faini.
Alipoulizwa na Tanzania Daima iwapo alikuwa tayari kukabiliana na adhabu katika hukumu inayosomwa leo, Lwakatare alisema: “Tuombeeni Mungu. Hukumu yoyote ambayo hatutaridhika nayo tutaikatia rufaa.”
Lwakatare alisema anatambua kuwa, iwapo atahukumiwa kifungo cha zaidi ya miezi sita, basi atajikuta akishindwa kugombea ubunge katika uchaguzi wowote ujao, hatua ambayo alisema ataipinga na kwamba ana uhakika kuwa hatimaye atashinda rufaa yake.
Wakati hukumu dhidi ya Lwakatare inayotarajia kuvuta mamia ya watu mahakamani hapo leo ikisomwa, kesi aliyoifungua akipinga ushindi wa Kagasheki katika kinyang’anyiro cha ubunge mwaka 2005 inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu ya Kagera.