Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Lowassa apata shida kumtetea Karamagi
Lowassa apata shida kumtetea Karamagi
By Marshy Abdu | Published  10/17/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Lowassa apata shida kumtetea Karamagi
na Christopher Nyenyembe


JARIBIO la Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kutaka kumsafisha na kumkingia kifua Waziri wa Nshati na Madini, Nazir Karamagi, kuhusu mkataba wa Buzwagi liliingia dosari jana baada ya wakazi wa Mbeya kupinga kwa sauti za juu utetezi wake kuhusu mkataba huo.

Hali hiyo ilitokea baada ya mwananchi mmoja kumuuliza Lowassa sababu zinazomfanya Karamagi asijiuzulu wakati akikabiliwa na tuhuma za waziwazi za kusaini mkataba wenye utata wa madini huko London, Uingereza.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu Lowassa alianza kwa kuwasifu wakazi wa Mbeya kwa uelewa wao wa mambo na akasema Karamagi alikuwa hajafanya kosa lolote la kimaadili au kisheria kwa kusaini mkataba huo.

Hata baada ya wananchi kuanza kuguna wakionyesha dhahiri kutokubaliana na majibu hayo, Waziri Mkuu alisema hoja za wapinzani kupinga mkataba huo kusainiwa London Uingereza hazijitoshelezi.

Aidha, aliwataka wananchi wa Mbeya kutambua kuwa mkataba wa Buzwagi hauna matatizo yoyote kisheria kwani uliandaliwa na kuboreshwa kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete.

“Mkataba wa Buzwagi ni mzuri, isipokuwa umepigwa maneno mengi ya kisiasa na sijaona kosa la Buzwagi hata kama ungesainiwa Sumbawanga au Kamachumu, bado ungekuwa vile vile. Kwa nini hili hamtaki kuliona?” alihoji Lowassa.

Lowassa alikutana na zahama hiyo ya kisiasa katika uwanja ule ule wa Shule ya Msingi ya Ruanda Nzovwe, ambao mawaziri na makada kadhaa wa CCM walikutwa na tukio la kuzomewa siku chache tu zilizopita.

Wakati hilo likitokea, hali ilikuwa tete kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile, aliyejikuta akikabiliwa na wakati mgumu kujibu maswali ya wananchi mbele ya Waziri Mkuu.

Kikubwa kilichomtia matatizoni Mwakipesile kilikuwa ni utata katika majibu aliyokuwa akiyatoa, hatua ambayo ilimfanya awaombe wananchi waache kumsulubu mbele ya kiongozi wake.

Swali lililoonekana mwiba kwa mkuu huyo wa mkoa ni juu ya mabilioni ya Rais Kikwete, yaliyogawiwa kwa wananchi, ambao wengi hazijawafikia, na kinyume chake akijikuta akitoa mchanganuo tofauti wa fedha zilizokopeshwa kutoka benki mbili, ya CRDB na NMB, tofauti na sh bilioni moja zilizoahidiwa.

Huku watu wakiguna, mkuu huyo wa mkoa alisema wazi kuwa mkoa huo umepokea kiasi cha sh milioni 500 tu za Rais Kikwete na si bilioni moja, na kwamba mkoa huo umeweza kukopeshwa kiasi cha sh bilioni 4.7 kwenye SACCOS na mtu mmoja mmoja kutoka kwenye benki hizo.

“Mimi ndiye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Nawaomba wananchi msinisulubu sana mbele ya Waziri Mkuu, najua kuwa mahitaji ya mbolea ya ruzuku kwa mkoa wetu ni makubwa kuliko kiasi tulichotengewa, na mkoa wetu unaoongoza kwa kukopeshwa benki kuliko mikoa yote Tanzania,” alisema Mwakipesile.

Kauli hiyo ilisababisha watu waendelee kuguna zaidi kutokana na utofauti wa maelezo kuhusu mbolea ya ruzuku na bilioni za Kikwete kama ilivyoelezwa awali na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika kuwa mkoa huo umepatiwa mbolea ya ruzuku tani 18,000 kwa mwaka huu, huku mkuu wa mkoa huo akidai kuwa umepokea tani 16,000 tu.

Katika kujibu hoja na maswali ya wananchi ambao hawakuwa na mwelekeo wowote wa kufurahia majibu hayo na kuendelea kuguna, ulifika wakati ambao waziri mkuu aliwaomba watu wamshangilie kwa majibu yake na yale yaliyotolewa na watendaji wengine wa serikali na kuonekana kundi dogo tu ndilo lililoweza kutii.

Maeneo mengine yaliyoonekana kero kwa wakazi wa mkoa huo na kuzusha maswali ni umilikaji wa viwanja, bei ya saruji na barabara ya Mbeya hadi Chunya, ambayo kwa kiasi kikubwa kulisababisha Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, aitwe na waziri mkuu ili kutolea maelezo kufuatia madai ya wazi kuwa tenda nyingi za ujenzi zinatolewa kwa makandarasi wa nje.

Waziri mwingine aliyejikuta akikumbwa na wakati mgumu ni Naibu Waziri wa Elimu na Ufundi, Ludovick Mwananzila, aliyeulizwa swali na mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Mbeya, aliyehoji upungufu wa walimu, huku wengi wakiwa wamejikita kwenye usimamiaji wa mitihani ya kidato cha nne na kusababisha wengine wakose masomo.

Akijibu swali la mwanafunzi huyo, Tito Benny, alikubali na kukiri mapungufu hayo kuwa mkoa huo una upungufu wa walimu zaidi ya 476 wanaopaswa kufundisha katika shule mbalimbali za sekondari zilizofunguliwa, huku mahitaji ya walimu wapya ni zaidi ya 7,000 wanaotakiwa kusambazwa kwenye shule zaidi ya 1,090 zilizofunguliwa nchi nzima.

Akihitimisha kipindi cha maswali na majibu katika mkutano huo, Lowassa aliwaasa wananchi kuwa yule mtu anayeitwa ‘bure’ alikwisha zikwa muda mrefu na matanga yakaanuliwa, akiwataka wananchi waache kukaa vijiweni, wafanye kazi, na hivyo kusababisha watu wengi wanune.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.