Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mwinyi: Tuhuma zisipuuzwe
Mwinyi: Tuhuma zisipuuzwe
By Marshy Abdu | Published  10/16/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Mwinyi: Tuhuma zisipuuzwe

na Tamali Vullu na Irene Mark


MADAI dhidi ya kushamiri kwa ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, jana yalipata sura nyingine baada ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, kuibuka na kusema kuwa madai hayo hayapaswi kudharauliwa na viongozi.

Akizungumza katika kongamano la kuadhimisha miaka minane tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere jana, Mwinyi alisema kuwa watu wanaotoa madai hayo wana akili na wameamua kufanya hivyo kutokana na hali ya mambo wanayoishuhudia.

Wakati Mwinyi akitaka kutopuuzwa kwa tuhuma hizo, mwanaharakati mwingine, Jenerali Ulimwengu, naye ameonya kuwa watu wanaodaiwa kuwa mafisadi, wanahatarisha kuanzishwa kwa vita nchini.

Akizungumza katika kongamano hilo lililoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam na kufanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Mwinyi alisema akili za watu hivi sasa zimepanuka na ndiyo maana wanaweza kuikosoa serikali hadharani.

“Haya yote ni matunda ya miti aliyoipanda Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alikazania suala la elimu, ili watu waondokane na ujinga,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, hivi sasa watu wako huru kuikosoa serikali na akasema kufanya hivyo ni ‘ruksa’.

“Sasa watu wanaikosoa serikali left, right and centre (kushoto, kulia na katikati), lakini hakuna anayetishiwa wala kukamatwa… haya ni matunda ambayo tunavuna kutokana na juhudi za Mwalimu Nyerere, ambaye alitoa uhuru wa watu kuzungumza na kukosa.

“Kuna mambo mengine yanazungumzwa katika magazeti, yanakereketa, lakini (mimi) sikasiriki… na baadhi yanayokosoa yana maana na yakifanyiwa kazi yanaweza kuleta maendeleo katika nchi yetu,” alisema Mwinyi.

Alisema siasa ya kujitegemea haina makosa na wala haitakuwa na makosa, na akashauri iendelee, kwani kinachotokea sasa ni kutofautiana katika njia za kutafuta maendeleo ya nchi.

Pia, alimsifia hayati Baba wa Taifa kwa kueleza kuwa hakuwa mbinafsi na kwamba mpaka anastaafu hakuwa na nyumba wala shamba.

Alisema Mwalimu Nyerere aliacha kazi ya ualimu iliyokuwa na mshahara na kuingia kuongoza chama kilichokuwa na posho pekee, kwa lengo la kutetea wanyonge na kwamba alikataa kujinufaisha binafsi.

“Nani kati yetu anaweza kufanya hivyo? Hii inaonyesha Nyerere alikuwa mtu wa aina gani. Hakuwa na tabia ya ubinafsi,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo kuieleza CCM Mkoa wa Dar es Salaam kuwa, wamechelewa kuanzisha kongamano la aina hiyo, kwani walipaswa kuanza mapema baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere.

Naye Waziri katika Ofisi ya Rais, anayeshughulikia Siasa na Uhusiano wa Jamii, Kingunge Ngombale-Mwiru, alitoa mada kuhusu tafakari ya falsafa ya Mwalimu Nyerere, alisema njia nzuri ya kumuenzi ni kusikiliza hotuba zake.

“Kwa kutumia hotuba za Mwalimu Nyerere tunaweza kujifunza zaidi na kuyafanyia kazi, hii ndiyo njia kubwa ya kumuenzi Mwalimu Nyerere,” alisema.

Alisema hivi sasa watu wengine wanasahau adui dhuluma, lakini akasema hiyo inawezekana akawa ni adui mkubwa kuliko wengine wanaotajwa.

“Tumezoea kusema Mwalimu alitufundisha kupambana na adui ujinga, maradhi na umaskini na kusahau dhuluma. Hii inawezekana ndiyo ikawa inasababisha haya mengine kutokea.

“Watu wa CCM hili tulitafakari sana, kwani tuna viongozi wanaopenda kufanya dhuluma,” alisema Kingunge.

Alisema kuwa rushwa ni aina ya dhuluma, kwani inamnyima mtu haki yake, lakini cha kushangaza wakati mwingine watu wanaishangilia. Alisema hivi sasa viongozi wengi wanaweka mbele masilahi binafsi na kusahau ya taifa.

Akizungumza katika kongamano kama hilo, lakini lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ulimwengu alisema watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi wanahatarisha amani ya nchi iwapo hawatakuwa tayari kutekeleza maagizo ya hayati Mwalimu Nyerere ya kujikosoa na kujirekebisha.

“Wachochezi wa vita ya baadaye ni mafisadi wa leo,” alisema Ulimwengu, hali iliyosababisha makofi na nyimbo kutoka kwa wanazuoni na baadhi ya watu waliohudhuria wakiwemo viongozi wa serikali, wanasiasa, mabalozi, maprofesa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU), Dk. Salim Ahmed Salim.

Ulimwengu alibainisha kuwa sera na mipango mizuri inayotekelezwa ndiyo matokeo ya amani na utulivu ulioimarishwa na hayati Baba wa Taifa.

Kuhusu mwelekeo wa nchi, Ulimwengu alisema hivi sasa ukoloni unarudi kwa kasi kuliko ilivyokuwa kabla ya uhuru.

“Tanzania na Afrika nzima inazidi kuwa koloni la weupe kuliko ilivyokuwa wakati wa ukoloni, siku hizi viongozi hakuna, hawa ni watawala,” alisema na kushangiliwa tena.

“Uongozi umegeuka kuwa ni bidhaa inayonunuliwa, mtu anakaa Marekani anapiga hesabu ya kununua jimbo hadi jimbo kwa dola zisizozidi bilioni tatu.

“Wananchi tupo sokoni tunauzwa, mtu anakupigia hesabu ya kuchukua Ikulu ili kutawala nchi kwa dola bilioni kadhaa… fedha inanunua nchi,” alisema.

Ulimwengu aliwataka watawala kumuenzi Baba wa Taifa kwa kutekeleza aliyokuwa akipigania ili kudumisha haki, amani na ujamaa kwa kukataa kutawaliwa.

Aidha, aliwataka kufahamu kuwa wananchi si wajinga na kuwashauri wanazuoni hao kuanzisha chama cha ujamaa kwa lengo la kupambana na nguvu mpya ya ukoloni na ubeberu.

“Nyerere kabla ya kifo chake alikuwa mzee lakini alikuwa na mawazo ya ujana, nawashauri vijana wasomi, undeni chama cha ujamaa halafu mwende kwa Msajili wa Vyama vya Siasa muone kama mtasajiliwa,” alisema.

Aliongeza kuwa woga wa watawala baada ya Mwalimu Nyerere unasababisha vurugu za mara kwa mara, huku akitolea mfano migomo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Kuhusu misaada tunayopata, Ulimwengu alibainisha kuwa enzi za uhai wa Baba wa Taifa wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1967, aliwataka wananchi kufahamu kuwa misaada ya wahisani itaifikisha nchi mahali pa kushindwa kuwa na sera binafsi na kuzitekeleza.

“Nilitamani kukutana na (Waziri wa Fedha) Meghji, siku chache kabla ya kusomwa kwa bajeti ili nimuulize amekuja lini kutoka Washington… siku hizi bajeti inapangwa Ulaya kwa e-mail tu, hapa waziri ana-download kisha anaenda bungeni kuisoma,” alisema Ulimwengu.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.