Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Maajabu kesi ya Balozi Mahalu
Maajabu kesi ya Balozi Mahalu
By Marshy Abdu | Published  10/6/2007 | Habari za Kitaifa | Rating:
Maajabu kesi ya Balozi Mahalu
na Happiness Katabazi


UPANDE wa mashitaka katika kesi ya kuhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Costa Ricky Mahalu na mwenzake, umekiri kwamba hakuna mlalamikaji katika kesi hiyo.

Maelezo hayo yalitolewa na Mwanasheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Abubakar Msangi, wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Pamoja na Balozi Mahalu, mtuhumiwa mwingine katika kesi hiyo ni Grace Martin.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa saa 3:30 asubuhi mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Sivangilwa Mwangesi, huku upande wa utetezi ukiwa na jopo la mawakili wanne wa kujitegemea, ambao ni Dk. Sengondo Mvungi, Cuthbert Tenga, Bob Makani na Alex Mngongolwa, aliyekuwa kiongozi wao.

Jana, upande wa utetezi uliwasilisha maombi manne, la kwanza likiwa ni kutaka wapatiwe maelezo ya mlalamikaji katika kesi inayowakabili wateja wao.

Ombi la pili lilikuwa ni kupatiwa vielelezo vilivyoambatanishwa kwenye hati ya maelezo ya makosa na ushahidi, kwa kuwa awali taasisi hiyo ilitoa hati isiyo na vielelezo vyenye orodha ya mashahidi. Aidha, mawakili wa utetezi waliomba pia kupatiwa orodha ya mashahidi.

Katika ombi la nne, mawakili hao waliitaka mahakama iizuie TAKUKURU isiwabughudhi watuhumiwa. Ombi hilo lilitokana na taarifa kuwa maofisa wa TAKUKURU waliwaita watuhumiwa ofisini kwao na kuwataka waorodheshe mali zao, jambo ambalo ni kuingilia kazi ya mahakama na kudai kuwa watuhumiwa hapaswi kufanya kazi za kipelelezi.

Katika majibu yake, mwanasheria wa TAKUKURU, alikubaliana na ombi la kwanza, kuwa wanayo haki ya kupewa maelezo ya mlalamikaji katika kesi hiyo lakini aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo haina mlalamikaji na kuwa tuhuma za kesi hiyo zilikusanywa kutoka kwenye vyombo vya habari.

“Mheshimiwa hakimu, katika ombi la kwanza, upande wa utetezi unayo haki, lakini kwa bahati mbaya kesi hii haina mlalamikaji kwa sababu tuhuma za kesi hii tulizikusanya kutoka kwenye vyombo vya habari yakiwemo magazeti,” alisema Wakili Msangi na kuwaacha baadhi ya wananchi wakiwamo waandishi wa habari na mawakili wa kujitegemea wakiangua vicheko mahakamani hapo.

Aidha, akijibu ombi la pili, Msangi alidai kwamba upande wa serikali hauwezi kutoa orodha ya vielelezo vya mashahidi kwa sababu kufanya hivyo kutahatarisha usalama wa mashaidi.

Katika jibu jingine, alidai kuwa TAKUKURU iliwataka watuhumiwa hao waorodheshe mali zao kwa sababu kifungu cha 26 na 27 cha Sheria ya Rushwa ya mwaka 2007 vinairuhusu TAKUKURU kumwita mtu yeyote na kumtaka aorodheshe mali zake, endapo itapata taarifa za tuhuma za kujilimbikizia mali dhidi ya mtu huyo.

Kwa msingi huo, Msangi aliitaka mahakama itupilie mbali ombi hilo na badala yake iendelee na usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo.

Baada ya majibu hayo, Mgongolwa alisema iwapo kesi hiyo haina mlalamikaji, inapaswa kuondolewa mahakamani hapo na kunukuu vifungu mbalimbali vya sheria na kuieleza mahakama kwamba kesi yoyote ya jinai huanza kwa malalamiko kutoka kwa mlalamikaji na inashangaza kuwa katika kesi hiyo hakuna mlalamikaji.

Aidha, alisisitiza kuwa ni lazima upande wa utetezi upatiwe vielelezo na orodha ya mashaidi kwa kuwa hilo ni hitaji la kisheria na linaendana na ibara ya 13 ya Katiba ya nchi inayotaka mtu aelezwe vizuri shitaka, vielelezo na mashahidi ili ajue yanayomkabili na kuandaa utetezi wake.

“Kwa kuwa upande wa serikali umekiri wenyewe mahakamani hapa kwamba kesi hii haina mlalamikaji, kwa sababu tuhuma walizipata kwenye magazeti, ndiyo maana wameshindwa kumtaja mlalamikaji, ni nani au idara gani ya serikali inayowashitaki wateja wetu kwa wizi?” alihoji Mgongolwa na kuiomba mahakama kuifuta kesi hiyo kwa kuwa kisheria hakuna kesi isiyokuwa na mlalamikaji.

Baada ya malumbano hayo ya kisheria, Hakimu Mwangesi aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 17 atakapotoa uamuzi.

Kesi hiyo imeanza kusikilizwa wiki mbili baada ya Mahakama Kuu kutoa amri ya kusitishwa kwa usikilizwaji wa ombi la Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), lililotaka kupitiwa upya kwa dhamana ya watuhumiwa hao.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by davy)
    Rating
    Watu wakisema tuna wanasheria feki tanzania watu wanalalamika kuwa si kweli...., prosecutor gani anayepoteza muda wake kutayarisha kesi na kuipeleka mahakamani kutokana na kusoma kwenye magazeti.. hii ni kiboko!!!!!!!!, Cha ajabu prosecutor haohao hawajafanya chochote, kuhusiana na tuhuma za Richmond, BOT na nyingine nyingi?. Tujiulize swali, je PCCB waliweza kumfikisha mahamani Prof Mahalu, sababu alisimamishwa na serikali ama walikuwa na ushahidi kweli????????, je kama waliweza kufanya hivyo iweje sasa wanashindwa kufanya tena kwa waheshimiwa wengine ambao wameandikwa kwenye vyombo hivyohivyo vya habari?????, na tatu mahakama inawezaje kukubali kuanzisha kesi bila kuwa na vielelezo vya kutosha kufungua kesi kubwa kama hiyo???
    Kwa mtazamo wangu mimi nadhani PCCB ni njia ya serikali kuwahadaa wananchi kuhusiana na vita dhidi ya rushwa na wala sidhani kama PCCB ama TAKURU wana uwezo wowote kuchunguza na kushitaki kiongozi yeyote wa serikali. Angalia kilichotokea kwa Mr David Mattaka, akachafuliwa jina na kusimamishwa kazi kama muhujumu uchumi wakati akiwa PPF, kashfa nzito ambazo huwezi kuzungumza hata mbele ya wakubwa zako, lakini wapi kapewa tena nafasi nyingine ATC, mnhhh!!!
    Ndiyo maana labda prosecutor aliambiwa we peleka tu hilo faili mahakamani na hakimu akaambiwa we sikiliza kesi mbele kwa mbele, ilimradi watanzania wameona tumedhalilisha kigogo mwenzetu, potelea mbali matokea huko mbele, mnhhh tutafika kweli kwa mwendo huu?????????
     
  • Comment #2 (Posted by Hemedi Begge)
    Rating
    Takuru inapaswa kuwa makini sana katika kufaatilia mambo yake kwani kwa kuzingatia haya yaliyo semwa mahakamani ni kudhirisha wazi kuwa bado kuna uzembe ndani ya serekali yetu na hii ndiyo inayo mpelekesha mpwenda Raisi wetu JK Kuvikemea vyombo vya habari na vyama vya upinzani kuwa siyo mahakimu.wala wapelelzi wa makosa ya jinai kazi hii iachiwe mamlaka halali zinazo husika na zitatoa taarifa sahii kwa watanzania wote.Vipi chomob cha serekali kama Takuru kinafikia uzembe wa kukubali kuwa kimekusanya habari hizi za walalamikiwa kupitia vyombo vya habari au mtu binafsi pasi na kuzingatia umuhimu wa kazi zao na heshima kwani ni jukumu wamepewa na sereakali kutenda kazi ipasavyo katika kitengo hicho.Ushahisdi halali unahitajika kwa kesi kama hiyo inayo mkabili Mahalu na G.Martin siyo kuleta unafiki na vielelzo vya chukui na kutowa hukumu kabla ya mamlaka husika haija sema kitu.Haki itendeke pale panapo husika tusiwachafulia majina Mahalu na G.Martin hadi watiwe hatiani na mamlaka husika tusiwe sisi ndiyo mahakimu wa mitaani kuwahuku pasi na uhakika wa tuhuma zilizopo.
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.