Na Peter Orwa
SERIKALI imeiagiza Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kupitia upya mishahara mipya ya wafanyakazi wake, baada ya kugundua ni mikubwa sana.
Waziri wa Miundombinu, Basil Mramba, aliiambia jana Kamati ya Bunge inayoshughulikia Miundombinu kuwa licha ya ukubwa huo, pia mishahara hiyo haikupata baraka za serikali. Hakufafanua.
TPA ilikutana na wabunge hao katika warsha maalum ya kuielimisha kamati hiyo, iliyoongozwa na Kaimu Makamu Mwenyekiti Mohammed Missanga, kwa ajili ya kujifunza shughuli za bandari. Warsha hiyo ilifanyika katika hoteli ya New Kunduchi Beach, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mramba, kima cha chini katika mishahara hiyo ni sh. 397,000 kwa mwezi. Hata hivyo, hakufafanua muda uliowekwa wa kukamilisha marekebisho ya mishahara mipya. Pia hakutaja kiwango cha juu cha mshahara.
Hata hivyo, Mramba aliisifu bandari za Tanzania kuwa zina viwango bora vyenye kukidhi viwango vya kimataifa, huku Dar es Salaam ikiwa ni ya pili kwa huduma bora barani Afrika.
Alitoa mfano wa kitengo cha makontena, ambacho sasa hivi kimebinafsishwa, kwamba kina uwezo wa kuhudumia zaidi ya makontena 250 kwa mwaka, jambo lililofanya TPA kuamua kukipatia ghala lake la hifadhi lililoko Ubungo, Dar es Salaam.
Pia katika mazingira ya matakwa hayo hayo ya kukidhi nyongeza ya kasi ya kontena zinazopakuliwa bandarini Dar es Salaam, TPA imelibinafsisha gati namba saba, hivyo kubakiwa na magati manane.
Akizungumzia suala la uongozi wa shirika hilo, Mramba alisema kuwa serikali sasa hivi inakamilisha kazi ya uteuzi wa mtendaji mkuu wa TPA kutoka miongoni mwa waombaji wa ndani na nje, baada ya nafasi hiyo kutangazwa kwa mara ya kwanza, lakini hakupatikana mwenye sifa kamili.
Katika hatua nyingine, Mramba alisema kuwa vyombo vingi vya usafiri majini katika Ziwa Victoria havifai na vinahatarisha maisha ya wasafri.
Baada ya kubaini hilo, alisema serikali imeamua kufungua ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga na Majini (SUMATRA) mjini Mwanza itakayosimamia usalama wa majini katika maziwa yote nchini. Sasa hivi iko katika hatua ya kuajiri wataalamu wa ofisi hiyo.
Sheria mpya ya mwaka 2004 ndiyo iliyounda TPA kutoka iliyokuwa Mamlaka ya Bandari nchini (THA) ambayo ilikuwa inasimamia bandari zilizoko katika bahari Hindi pekee.
Kwa mujibu wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa TPA, Peter Mtandu miongoni mwa washiriki katika warsha ya jana ni kutoka Wizara ya Miundombinu, Msajili wa Hazina, Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC), SUMATRA na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Wengine ni Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), TANROADS na Wakala wa Mizigo na mashirika ya meli.