Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Prisons yazitimulia vumbi Simba, Yanga
http://www.habaritanzania.com/articles/4199/1/Prisons-yazitimulia-vumbi-Simba,-Yanga
By Marshy Abdu
Published on 10/5/2007
 
MAAFANDE wa Prisons ya Mbeya jana waliendelea ‘kutembeza buti’ katika Ligi Kuu ya Bara kwa kuwapigisha kwata maafande wenzao wa JKT Ruvu. Hilo lilidhihirika jana katika mechi iliyokuwa ya ushindani mkubwa kwa dakika zote 90

Prisons yazitimulia vumbi Simba, Yanga
na David Frank, Arusha


MAAFANDE wa Prisons ya Mbeya jana waliendelea ‘kutembeza buti’ katika Ligi Kuu ya Bara kwa kuwapigisha kwata maafande wenzao wa JKT Ruvu.

Hilo lilidhihirika jana katika mechi iliyokuwa ya ushindani mkubwa kwa dakika zote 90 iliyoisha kwa Prisons kuvuna pointi tatu.

Kwa matokeo hayo, Prions wameziki kukamata usukani wa Ligi Kuu iliyoanza Septemba 22 kwa kufikisha pointi 12.

Matokeo ya mechi hiyo, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, yamezidi kuifanya Prisons kuwa timu ya kutisha zaidi msimu huu.

Si suala la pointi tu, pia ni timu pekee hadi sasa isiyopoteza mchezo isipokuwa kutoa kipigo tu kwa kila ajaye mbele yake. Zikicheza soka ya kutulia na akili zaidi, maafande hao waliweza kuonyesha soka maridadi kwa dakika zote.

Wenyeji JKT Ruvu ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 29 lililofungwa na Sosteness Manyasi. Na kuingia kwa bao hilo kuliwafanya vijana wa Prisons kucharuka na kuanza kutandaza soka ya uhakika.

Juhudi hizo za vinara hao wa Ligi zilizaa matunda katika dakika ya 43 baada ya kupata bao la kusawazisha likifungwa na Said Mtupa.

Mtupa alifunga bao hilo kiustadi baada ya kupata pasi iliyotokana na krosi maridadi kutoka kwa Stefano Mwasika. Maafande hao walikwenda mapumziko wakiwa wamefungana 1-1.

Kipindi cha pili kila timu iliuanza mchezo kwa kasi kubwa kwa lengo la kupata bao la kuongoza. Maafande wa Prisons ndiyo walioonekana kutulia zaidi na kufanikiwa kupata bao la pili katika dakika ya 60.

Bao hilo lilifungwa kiustadi na mshambuliaji wake hatari, Osward Mouris, kwa kufumua shuti lililokwenda wavuni moja kwa moja.

Prisons wanarejea katika Uwanja wao wa Kumbukumbu ya Moringe Sokoine kuwasubiri Coastal Union, Jumamosi.

Naye Anna Makange anaripoti kutoka Mkwakwani kuwa Wagosi wa Kaya Coastal Union jana walichemsha gwaride la Polisi Dodoma kwa kukandamizwa mabao 3-2.

Mabao ya Coastal yalifungwa na Moses Peter na Kudra Saad huku mabao mawili ya Polisi Dodoma yakifungwa na Weston Mwanjali na jingine kupitia kwa Joseph Kabejo.

Katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, Mwandishi Wetu Fatuma Gaffus anaripoti kwamba Pan African jana ilitoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar.

Pan walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 42 lililofungwa na Omar Mkuta kabla ya Michael Katende kuisawazishia Kagera Sugar dakika tatu baadaye.

Mechi nyingine jana ilikuwa katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro ambako Moro United ilitoka sare ya 1-1 na Toto African.