WAKATI Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, akikanusha taarifa zilizoandikwa na gazeti hili jana na jingine la kila siku, zinazoeleza kuhusu kuzomewa na wananchi wa Mbeya wakati wa mkutano wao wa hadhara uliofanyika juzi, waziri mwingine katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, alikutwa na zahama kama hiyo huko Mpanda, mkoani Rukwa.
Aliyefikwa na mkasa huo hiyo hiyo juzi jioni alikuwa ni Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud, ambaye alijikuta akizomewa na wananchi waliofika katika mkutano aliouhutubia, baada ya kutoa ahadi kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa kikikusudia kulirejesha Jimbo la Mpanda Kati.
Aboud alipata wakati mgumu na kujikuta akizomewa pale alipotangaza mkakati wa CCM kulikomboa Jimbo la Mpanda Kati linaloongozwa na Mbunge wa CHADEMA, Said Alfi.
Awali Aboud aliwaambia wananchi wa Mpanda kuwa malengo ya ziara yake hapo yalikuwa ni kutaka kujua kero zao na hususan zinazohusiana na usalama wa raia na pia kufafanua Bajeti ya Serikali ya mwaka 2007/2008.
Baada ya kuwasalimia wananchi, aliwataka watoe kero zao, maoni na ushauri ndipo apate mwelekeo wa hotuba yake kwa kujibu hoja kwa njia ya hotuba, jambo lililowafurahisha mno wananchi.
Huku wakiwa na matumaini ya ufumbuzi wa tatizo la watu kupigwa nondo na mapanga kwa muda mrefu sasa, wananchi wengi walihoji ubia uliopo kati ya baadhi ya polisi wilayani Mpanda na wahalifu wanaofahamika kwa polisi, ingawa hawachukuliwi hatua zozote za kisheria.
Mambo mengine aliyoulizwa Naibu Waziri Abood ni pamoja na kesi za madai wilayani Mpanda kuamuliwa na polisi badala ya mahakama, baadhi ya polisi kudai fedha za kufuta kesi pale wanaoshitakiana wanaporidhiana, ukosefu wa magari kwa ajili ya usafiri kwa Jeshi la Polisi na kutokuwepo kwa vituo vya polisi mjini Mpanda.
Miguno ilianza pale naibu waziri huyo alipoziponda kauli alizoziita za wapinzani, waliodai kuwa maisha ya Watanzania ni magumu mno katika awamu hii na wananchi lazima wafunge mikanda na kudai mipango ya serikali inalenga maisha bora kwa kila Mtanzania.
“Hawa wanataka kuwakosanisha wananchi na serikali yao, hatutawasikiliza na tunaendelea kuchapa kazi kuwaletea maendeleo, waache gere zao,” alisema Aboud huku akizomewa badala ya kushangiliwa na watu waliosikika wakisema; “umeishiwa, huna la kutudanganya, kodi zetuuu,” na maneno mengi mengine.
Hali ya kuguna ilizidi zaidi pale alipotoa takwimu za kupungua kwa uhalifu nchini kwa asilimia 45, badala ya kujibu hoja za msingi za kwa nini polisi wilayani Mpanda wameshindwa kuzuia vitendo vya watu kukatwa mapanga na kupigwa nondo.
“Tunataka ufumbuzi wa tatizo la ujambazi si kututaka tutoe ushirikiano kwa polisi wanaoshirikiana na majambazi,” alisikika akisema kijana mmoja kwa jazba.
Wakati hayo yakimfika Aboud, Waziri Wasira aliyepiga simu chumba cha habari cha gazeti hili jana asubuhi na akazungumza na Mhariri Mkuu, alizielezea taarifa za wao kuzomewa Mbeya kuwa ni za uzushi na zisizo na ukweli wowote.
“Nimepigiwa simu nyingi na watu wakiniuliza kuhusu kuwapo kwa taarifa za kuzomewa, na mimi nikasema hayo ni mambo ya magazeti. Nilikuwapo pale uwanjani na nilikuwa mtu wa mwisho kuondoka,” alisema Wasira aliyeeleza kuwa alikuwa akizungumza wakati akiwa safarini kutoka Mbeya kurejea Dar es Salaam.
Wakati Wasira akikanusha taarifa hizo, habari nyingine kutoka mkoani Mbeya zinaeleza kuwa, muda mfupi baada ya mkutano huo wa hadhara kumalizika, katibu wa mmoja wa mawaziri waliokuwapo katika mkutano huo, aliwakusanya waandishi wa habari waliokuwapo hapo na akawataka waandike maneno ya viongozi na waachane na matukio ya kuzomea zomea.
“Hawa viongozi walifanya kila waliloweza kuzuia taarifa za wao kuzomewa. Katibu wa waziri (anamtaja jina waziri), aliwaita waandishi na kuwapa shilingi 10, 000 kila mmoja na akawataka kutoandika kuhusu kuzomea kulikotokea na badala yake kuzingatia hoja zilizotolewa,” alisema mwandishi wa habari wa gazeti hili aliyekuwapo katika mkutano huo.
Kwa upande wake Waziri Wasira alipoulizwa jana na Mhariri Mkuu wa gazeti hili ni kwa sababu gani basi, kiongozi wa kikundi cha Sanaa cha Tanzania One Theatre (TOT), John Komba aliyekuwapo katika mkutano huo wa juzi, alilazimika kuwataka wale wote waliokuwa hawataki kukishangilia chama hicho kwa kupunga mikono waondoke uwanjani, iwapo kulikuwa hakuna zomeazomea, alijibu kwa maneno machache bila kufafanua; “Komba yule ni msanii.”
Malalamiko hayo ya Wasira yalimfanya Mhariri Mkuu wa gazeti hili, Absalom Kibanda, awasiliane na watu kadhaa wa Mbeya waliokuwapo katika mkutano ule, wakiwamo waandishi wa habari wa vyombo kadhaa (si wa Tanzania Daima) wanaofanya kazi Mbeya ili kupata uhakika wa kile kilichotokea.
Mkazi mmoja wa Mbeya aliyejitambulisha kwa jina moja la Hiriza, aliyezungumza na gazeti hili jana, alieleza kushangaa baada ya kuelezwa na mhariri mkuu kuwa Waziri Wasira alikuwa akikanusha kuwapo kwa tukio la wao kuzomewa.
“Ni muongo. Tukio lilikuwa ni la wazi kabisa, mimi ni shuhuda, nilikuwa pale na kila mtu aliyekuwapo pale aliliona. Kila aliyepanda jukwaani alipokuwa akizungumza kulikuwa na kuguna, na hali ilizidi wakati msafara ukiondoka, ndipo watu walipoanza kuzomea huku wengine wakirusha mchanga hewani,” alisema Hiriza.
Mwandishi mmoja mwandamizi wa habari wa gazeti moja la kila siku (si wa Tanzania Daima), alipoulizwa kuhusu kile kilichotokea wakati wa mkutano huo wa juzi alikuwa na haya ya kusema:
“Ndugu yangu mkutano wa jana (juzi) ulimalizika kwa aibu. Kwanza walijitokeza watu wachache sana kulinganisha na wale waliojitokeza wakati wapinzani walipokuwa hapa wiki chache tu zilizopita.
“Pili, baada ya baadhi ya viongozi wa CCM mkoani hapa kubaini kuwa walikuwa wakishangiliwa na kikundi kidogo tu cha wanachama wao waliokuwa mbele huku wale waliokuwa nyuma wakiwa kimya, walitoroka mkutanoni mapema, na hali ya kuzomea iliongezeka wakati viongozi hao walipokuwa wakiondoka mkutanoni,” alisema mwandishi huyo mwandamizi wa habari.
Kutokana na majibu hayo, mhariri mkuu alilazimika kumweleza mwandishi huyo wa habari kuwa Waziri Wasira alikuwa amepiga simu chumba cha habari cha gazeti hili akikanusha kuwapo kwa tukio lolote la kuzomea.
“Wasira hasemi kweli. Hapa mjini hivi sasa hiyo ndiyo habari kubwa, kila mtu aliyekuwapo uwanjani jana (juzi) aliiona hali hiyo ya kuzomea iliyokuwa kubwa hasa wakati msafara wa viongozi na makada wa CCM ulipokuwa ukiondoka,” alisema mwandishi huyo wa habari.
Mwandishi mwingine wa gazeti la Mwananchi aliyekuwapo Mbeya wakati wa tukio hilo, alipoelezwa kuhusu taarifa za Wasira kukanusha taarifa hizo alisisitiza kutokea kwa tukio hilo.
“Kilichotokea kwenye ule mkutano ni cha wazi kabisa. Watu walizomea, tena sana. Wasira mwenyewe alizomewa alipoongelea mbolea,” alisema mwandishi huyo wa habari.
Kwa mujibu wa mwandishi wa habari huyo, hali ya kuzomea ilizidi wakati Akwilombe, kada wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) aliposimama na kukiponda chama chake hicho cha zamani akisema ni cha kifamilia.
Kwa mujibu wa mwandishi huyo, kauli hiyo ya Akwilombe ilisababisha watu waliokuwa wakimsikiliza kumzomea na kuanza kuimba ‘Mbowe, Mbowe, Mbowe, CHADEMA CHADEMA CHADEMA’.
Hali kama hiyo ilitokea pia wakati Tambwe Hizza na Salum Msabah, makada wawili wa zamani wa Chama cha Wananchi (CUF) walipopanda jukwaani kwa nyakati tofauti na kuviponda vyama vya upinzani.
Viongozi na makada wa CCM waliokuwapo katika mkutano huo wa juzi mbali ya Wasira, Akwilombe, Hizza na Msabah, ni Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, John Chiligati na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Aggrey Mwanri, aliyekuwa kiongozi wa msafara.
Tukio hili linakuja siku chache tu tangu mawaziri na makada wengine wa CCM watumwe kwenda mikoani kufafanua kuhusu bajeti na kukanusha tuhuma za vyama vinne vya upinzani dhidi ya serikali na viongozi wake wa juu na wa chama tawala, wanaotuhumiwa kwa vitendo mbalimbali ya ufisadi.