WAKATI serikali ikisuasua kufikia uamuzi wa kuzishughulikia tuhuma za ubadhirifu ndani ya Benki Kuu (BoT) zilizotolewa hivi karibuni na Dk. Willibrod Slaa (Karatu-CHADEMA), Benki ya Dunia imesema ni matumaini kuwa, serikali itachukua hatua madhubuti kuhusu tuhuma hizo.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Kanda ya Afrika, Obiagel Ezekwesili, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili nchini kwa ajili ya kuhudhuria mkutano unaohusu masuala ya ukimwi utakaofanyika mkoani Arusha.
Benki ya Dunia imetoa kauli hiyo wakati serikali ikisisitiza kuwa Dk. Slaa na wengine wanaotoa tuhuma hizo wanatakiwa kwenda mahakamani na wala haijawahi kugusia kuwa itafanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo ili kubaini kama ni za kweli au la.
Hata hivyo, Ezekwesili alisema kuwa Benki ya Dunia, inataka kuona hatua za kuchunguza madai hayo zinachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuweka wazi kile kitakachobainika katika uchunguzi huo.
Akizungumzia suala la uchunguzi ambao unaendelea kuhusiana na tuhuma nyingine zinazoihusu BoT, alisema Tanzania kama nchi, inao uhuru wa kufanya uchunguzi wao, na wao kama Benki ya Dunia haingilii bali wanachotaka ni kuona hatua zinachukuliwa.
Serikali, kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imeiagiza kampuni ya kimataifa kufanya ukaguzi BoT kuhusiana na ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi zinazodaiwa kufujwa kupitia akaunti ya kulipia madeni ya nje.
Uchunguzi huo unatarajiwa kukamilika mwezi ujao na Dk. Slaa na wapinzani walioibuka na tuhuma nyingine wanadai kuwa kinachokaguliwa katika BoT ni sehemu ndogo sana ya ubadhirifu ambao umefanywa ndani ya chombo hicho nyeti katika uchumi wa nchi.
Ezekwesili alisema kitendo cha BoT kutuhumiwa hadharani kinaweza kuwa ni matokeo ya kutokuwepo kwa uwazi katika shughuli zake, utekelezaji na ukaguzi wa mahesabu.
Wakati Benki ya Dunia ikitoa mwelekeo huo huo, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, jana alisisitiza kuwa, serikali ndiyo iliyoagiza ukaguzi wa hesabu za BoT na itachukua hatua kulingana na matokeo ya ukaguzi unaofanywa hivi sasa.
Akizungumza na Balozi mpya wa Finland nchini, Juhan Toivonen, aliyekwenda kumtembelea ofisini kwake Mtaa wa Magogoni jijini Dar es Salaam jana, Lowassa alisema kuwa ni vema mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini wakafahamu kuwa Serikali imeamua kwa dhati kupambana na rushwa na kwamba ndiyo iliyoitisha uchunguzi BoT.
“Ripoti ya ukaguzi ikikamilika, Serikali itachukua hatua zinazostahili kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Nne imedhamiria kikweli kupambana na rushwa kwenye ngazi zote,” alisema.Waziri Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Nne kamwe haifanani na serikali inayoendekeza rushwa kama zinavyoonyesha taarifa zinazochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini hivi sasa.
“Kama ingekuwa ni serikali inayoendekeza rushwa, basi ni dhahiri ingeshindwa kukusanya kodi… ingeshindwa kupeleka mabilioni ya fedha za maendeleo kwa wananchi vijijini kama ilivyofanya katika bajeti ya mwaka huu,” alisema.
Hivi sasa Serikali inakusanya wastani wa sh bilioni 250 kwa mwezi, ikilinganishwa na wastani wa sh bilioni 25 tu mwaka 1995/96. Katika bajeti ya mwaka huu, Serikali pia imepeleka sh bilioni 286 kwa halmashauri za wilaya kwa ajili ya kugharimia shughuli za maendeleo.
Bajeti ya mwaka huu vilevile imetenga maeneo ya kipaumbele na kuyapa fedha za kutosha.
Chini ya utaratibu huo elimu imetengewa sh trilioni 1; miundombinu (barabara) sh bilioni 777, afya sh bilioni 589.9; kilimo sh bilioni 379 na maji sh bilioni 309.
Kwa upande wake, balozi huyo alisema hata naye anashangazwa na kasi ya taarifa za tuhuma za rushwa katika vyombo vya habari nchini wakati ukweli ni kwamba taasisi za kimataifa za uchunguzi wa rushwa zinatoa ripoti nzuri kwa Tanzania.
Shirika la Kimataifa la Kupambana na Rushwa (Transparency International) katika ripoti yake ya hivi karibuni, limeeleza kuwa Tanzania inaongoza katika nchi za Afrika Mashariki kwa mapambano dhidi ya rushwa. Tanzania ilikuwa nchi ya 14 katika Afrika wakati Uganda ni ya 22 na Kenya ikiwa nyuma, 42.
Balozi Toivonen alisema kuwa nchi yake inakamilisha taratibu za kuipatia Tanzania msaada wa dola za Marekani milioni 36 (sawa na takriban sh bilioni 45) katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.