WANAFUNZI wanane wa Shule ya Msingi ya Ntokela, Wilaya ya Rungwe, katika Mkoa wa Mbeya, na mtoto mdogo wa mwaka mmoja na nusu, wamekufa papo hapo na wengine wanane wamejeruhiwa vibaya baada ya kugongwa na gari la Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola, walipokuwa wakilifuata kwa nyuma gari la matangazo ya kidini.
Ajali hiyo mbaya ya barabarani ilitokea juzi usiku kwenye Kijiji cha Ntokela, Rungwe mkoani Mbeya, na hivyo kusababisha majonzi makubwa kwa wakazi wa kijiji hicho na kufanya idadi ya watu waliokufa mkoani Mbeya kutokana na ajali katika kipindi kisichozidi siku 12 kufikia 37.
Hiyo ikiwa ni ajali ya pili mbaya kutokea mkoani Mbeya, ajali ya kwanza ni ile ya basi la SABCO iliyotokea eneo la Igurusi kwenye barabara kuu itokayo Mbeya kwenda Iringa, iliyoyahusisha magari mengine matatu, kuua watu 28 na kujeruhi wengine 44.
Ajali ya juzi iliyotokea katika kijiji hicho majira ya saa 2:00 usiku ililihusisha gari aina ya Ford Ranger Pick Up, lenye namba za usajili T 872 ALM, mali ya Kampuni ya Coca Cola, kugonga kundi la watoto hao waliokuwa wakilifuata kwa nyuma gari jingine aina ya Canter, likiwa halina namba za usajili, lililokuwa likitoa matangazo ya mkutano wa Injili uliokuwa ufanyike jana kijijini hapo.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, ambaye pia ni Ofisa Upelelezi wa mkoa, Emmanuel Kabwogi, alisema kuwa gari hilo la Coca Cola, lililokuwa likiendeshwa na Mbonike Mwinuka, lilikuwa linaelekea jijini Mbeya likitokea Tukuyu na lilipofika eneo hilo ilikutana na hiyo Canter ikielekea Tukuyu huku ikitoa matangazo ya mkutano huo wa Injili.
Alisema gari hilo la Coca Cola likiwa linapanda mlima kijijini hapo, lilipishana na gari la matangazo na mara baada ya kulipita ndipo alipokutana na watoto hao wakilifuata gari la matangazo kwa nyuma na hivyo kuwagonga, ambapo wanane walikufa papo hapo na mtoto mmoja wa mwaka mmoja na nusu alifia hospitali.
Kabwogi aliwataja waliokufa papo hapo, wote wakiwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Ntokela, kuwa ni Zawadi Kalawa (12), Elisha Robert (11), Hussein Mrisho (10), Sara Anania (13), Emmanuel Tumaini (9), Arnold Charles (9), Asiah Mkono (11) na Eva Kallaghe.
Mwingine ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu aliyetajwa kwa jina la Agrey Nguli, ambaye alifariki mara baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Misheni ya Igogwe iliyopo wilayani Rungwe.
Aliwataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na Enea Sanga (20), Kisa Kassim (22), Nuru Ezekia (17), Hanifa (10), Tegemeo Simbeye (15), Janeta John (1.5), Tumaini Thomas (17) na Rahel Eli (15).
Mkuu huyo wa Upelelezi mkoani hapa aliongeza kuwa dereva wa Ford Ranger alifanikiwa kutoroka mara baada ya ajali na kisha kujisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya ambako bado anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo, dereva wa gari la matangazo, alitoweka baada ya kubaini kuwa ndio chanzo cha ajali hiyo na hadi jana jioni polisi walikuwa bado wakimsaka.
Kufuatia ajali hiyo, wananchi wenye hasira walilivuta pembeni gari la Coca Cola na kuliteketeza kwa moto baada ya kulilipua kwa wakitumia mafuta aina ya petroli.
Alisema polisi mkoani hapa wanaendelea kumsaka dereva wa gari la matangazo pamoja na uchunguzi wa mazingira ya ajali hiyo ili kubaini chanzo na mhusika mkuu wa ajali hiyo.