SUMU iliyomwagwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zubeir Zitto (CHADEMA), kuhusiana na kuwepo kwa shaka ya rushwa katika mkataba wa mradi wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi mkoani Shinyanga, imeanza kuwaingia wananchi.
Hayo yalithibitika juzi katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alipohutubia mkutano wa hadhara katika Wilaya ya Geita, mkoani mwanza.
Katika mkutano mmoja, wananchi waliokusanyika kumsikiliza, walikataa kuyasikiliza maneno yake na huku wakizomea, walimpasha naibu waziri huyo kuwa, wanachofahamu wao ni kuwa, katika mkataba wa Buzwagi, kuna kiongozi wa serikali alipokea rushwa.
Sambamba na hatua hiyo wananchi hao, pia walisema kusimamishwa kwa Zitto ni kitendo cha uonevu, kwani kilifanywa ili kumlinda Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.
Ngeleja alifanya mkutano huo katika kile kinachoonekana kujibu hoja zilizotolewa na viongozi wa upinzani ambao hivi karibuni walimaliza ziara yao ya mikoa takriban 10 kuelezea jinsi rasilimali za nchi zinavyoibwa na viongozi wachache serikalini.
Katika hotuba yake, Ngeleja alisema kuwa hakuna ukweli, ingawa wapinzani wanaihusisha serikali na rushwa kuhusiana na kusainiwa kwa mkataba wa Buzwagi, hoja iliyoamsha kelele za wananchi ambao walisisitiza kuwa ni kweli rushwa ilitawala mazingira ya kusainiwa kwa mkataba huo.
“Wapinzani wamepita hapa na kuwaeleza. Hivi kuna watu wameamini kuwa ni kweli waziri wangu alisaini mkataba ule wa Buzwagi kwa kupewa kitu kidogo?” alihoji Ngeleja na kujibiwa na wananchi kwa pamoja katika mkutano huo kuwa “Ni kweli alipata kitu kidogo.”
Akauliza tena: “Mnaamini hivyo?” Wananchi walijibu ‘ndiyo’ kwa sauti na kupiga miluzi ya kelele na kushangilia, wakisisitiza kukubaliana na upande wa hoja za Zitto.
Kutokana na majibu hayo, Ngeleja aliwasii wananchi kutulia na kuanza kuwaeleza kuwa si kweli kwamba kusimamishwa kwa Zitto bungeni kulikuwa ni kwa kuonewa, isipokuwa alisimamishwa kutokana na kushindwa kujibu hoja yake aliyoitoa kuwa Waziri Karamagi alisema uongo.
Akiongea na kuonyesha karatasi alizodai kuwa ni waraka mahsusi wa bungeni (hansard), alieleza kuwa Zitto hakuonewa bali alisimamishwa kutokana na kushindwa kulithibitishia Bunge uongo wa Karamagi.
“Alishindwa kuthibitisha kauli hiyo, sasa hapa alionewa vipi? Na bungeni Spika alimtaka kuthibitisha kauli yake na kuwasilisha mkataba ama ushahidi kuhusiana na ukweli halisi wa mkataba anaoujua ili Bunge liweze kumbana Karamagi kwa kusema uongo, lakini alishindwa kuthibitisha, hapa ndipo alifungiwa,” alieleza naibu waziri huyo.
Baada ya maelezo yake, alikaribisha maswali, ambapo katika watu saba waliojitokeza, alielezwa na kijana Hamimu Kahamba, kuwa iwapo serikali inawataka wananchi waamini kuwa hakukuwa na mazingira ya rushwa katika kusaini mkataba huo, ni vema mkataba ukawekwa hadharani ili kila mtu auone unasema nini.
“Nakushukuru waziri umetueleza uongo wa Zitto na ukweli wa Karamagi, lakini sasa mbona mikataba mnaifanya siri? Basi itangazeni hadharani tuijue na tusadiki kama (wapinzani) walikuwa waongo,” alieleza Kahamba.
Katika majibu ya jumla, Ngeleja alieleza kuwa suala la mikataba ni gumu kisheria na kwamba ni siri kati ya wawekezaji na serikali.