VIJANA wa vyama vinne vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na TLP wametoa tamko la pamoja wakikejeli ‘hekima za kisiasa’ za mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale -Mwiru.
Katika tamko lao, vijana hao waliokutana jana katika Hoteli ya Equator mjini Arusha, wamebainisha kuwa, kauli iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Siasa na Uhusiano wa Jamii, Kingunge Ngombale-Mwiru kuwa ni sehemu ya propaganda zenye lengo la kupotosha hoja zilizotolewa na viongozi wa upinzani kuhusiana na ubadhirifu unaoendelea nchini.
Wakichambua kauli za Kingunge kwa kutumia mifano kadhaa, vijana hao waliokutana chini ya Uenyekiti wa Mkurugenzi wa Vijana wa Chadema, John Mnyika, walieleza kuunga kwao mkono hoja za viongozi wakuu wa upinzani sambamba na kuwataka wananchi kumpuuza Kingunge kwa maelezo kuwa anaupotosha umma.
“Tunaunga mkono uamuzi wa viongozi wetu wa kitaifa kuanika wazi kwa umma orodha ya mafisadi; hii ni kwa
sababu rasilimali zinazofujwa ni za wananchi wa Tanzania, wanaoathirika kutokana na ufisadi, ni umma wa Watanzania na wenye uamuzi wa mwisho wa kuwawajibisha viongozi mafisadi ni umma wa Watanzania,” walisema vijana hao katika tamko lao la maandishi.
Tamko hilo la kwanza na la aina yake tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi miaka 15 iliyopita, liliwahusisha Godbless Lema, ambaye ni Katibu Mwenezi wa TLP mkoani Arusha na msemaji wa ushirikiano wa vyama vya upinzani mkoani humo, Mohammed Maabad, ambaye ni Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Arusha Mjini, na Mwenyekiti wa ushirikiano wa vyama vya upinzani mkoani humo.
Pia walikuwepo Ened Muro, mwakilishi wa NCCR-Mageuzi, Amos Kibanda ambaye ni Katibu wa CHADEMA Arusha na Calist Lazaro, ambaye ni Mwenyekiti wa TLP wa Wilaya ya Arusha Mjini.
Vijana hao pia walieleza kushangazwa kwao na msimamo wa Kingunge kuupondo uamuzi wa wapinzani kuzunguka nchi nzima kwa lengo la kuwaeleza wananchi kile hasa kilichotokea dhidi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ilhali akijua kuwa wanao wajibu wa lazima wa kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa vijana hao, danadana zinazopigwa na serikali dhidi ya tuhuma mbalimbali za ufisadi na wajibu wao wa kuwatumikia wananchi, ndiyo sababu kuu ya wapinzani kuzunguka nchi nzima wakieleza ni nini hasa kinachotokea hapa nchini.
Aidha, vijana hao walisema viongozi wao walikuwa na wajibu wa kuzunguka ili kueleza ukweli kuhusu kupigwa danadana kwa hoja ya kashfa ya ufisadi ndani ya Benki Kuu iliyokuwa iwasilishwe na Dk. Willbrod Slaa wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti uliomalizika hivi karibuni.
Walihoji iwapo kauli aliyoitoa Kingunge ni msimamo halisi wa serikali na kuitaka Ikulu iache ukimya na kueleza kinagaubaga iwapo ilimtuma Kingunge kuisemea.
“Katika hatua ya sasa tunazichukulia kauli hizo kuwa ni maoni binafsi ya Kingunge mpaka hapo Ikulu itakapothibitisha vinginevyo,” walisema katika tamko lao.
Walisema kuwa wana shaka kuwa Kingunge ametoa kauli hizo kwa nia ya kupoteza lengo ili wananchi waanze kuzijadili kauli zake badala ya kujadili orodha ya mafisadi na hatima ya rasilimali za nchi.
Walisisitiza kuwa wapinzani hawawezi kutoa vielelezo vya tuhuma wanazozitoa kwa sababu tayari serikali yenyewe inafahamu kuhusiana na ubadhirifu huo.
“Tunashangazwa na kauli hii kwa kuwa tunaamini Waziri Kingunge anafahamu kabisa kuwa sehemu kubwa ya tuhuma hizi zipo katika Ripoti za Mkaguzi wa Serikali ikiwemo ile ya mwaka 2005/06, na kwamba vyombo vya dola vinafahamu uwepo wa tuhuma hizi lakini kwa zaidi ya miaka miwili vyombo hivyo havijachukua hatua dhidi ya vigogo waliotajwa,” walisema.
Ili kuthibitisha kuwa serikali na vyombo vingine vinafahamu kuhusisna na tuhuma hizo, walisema kuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alishasema kwamba anavipeleka polisi vielelezo vyote vya ushahidi alivyotoa Dk. Slaa, wakati alipowasilisha tuhuma za ubadhirifu BoT, ili vichunguzwe.
“Pengine Kingunge angetoa hukumu hiyo kwa Spika kwa kushindwa kupeleka vielelezo,” walisema.
Aidha, walieleza kushangazwa na madai ya Kingunge kudai ushahidi wakati akijua fika kwamba ni serikali hiyo hiyo iliyowahi kutoa taarifa kwa umma kwamba, tuhuma za ufisadi zikiwemo za BoT zilikuwa zimeshaanza kufanyiwa uchunguzi na TAKUKURU.
Tamko hilo pia lilimtaja Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kuwa mmoja wa viongozi wa juu aliyewahi kukaririwa akisema serikali ilikuwa ikifahamu kuwapo kwa madai ya kashfa ya ufisadi ndani ya BoT hata kabla ya upinzani.
“Kwa upande mwingine, madai ya kutaka kushughulikia rushwa kubwa kubwa zikiwemo za kwenye mikataba, yalianza kutolewa na Rais Kikwete wakati akifungua mkutano wa kwanza kabisa wa Bunge mwaka 2005,” walisema vijana hao na wakaongeza kuwa akiwa mkoani Rukwa mwanzoni mwa mwaka jana, Kikwete huyo huyo alinukuliwa pia akisema kuwa, alikuwa akiwafahamu wala rushwa na kuwa alichokuwa akikifanya ni kuwapa muda wa kujirekebisha.
“Tulitarajia Waziri Kingunge kama mshauri wa rais wa masuala ya siasa, angemshauri apeleke ushahidi katika vyombo vya dola na si kuwahukumu viongozi wa upinzani ambao wametoa orodha ya mafisadi na ushahidi kutoka kwenye taasisi za serikali yenyewe,” walisema.
Walisema kuwa madai kuwa ziara za wapinzani ni upotevu wa fedha usio na msingi, hayana msingi, kwa sababu kiasi cha sh trilioni 1.3 zinazodaiwa kuibwa na viongozi wa serikali zingeweza kutumika kuboresha maisha ya Watanzania.
Pia walisema kuwa hawana imani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwani mwenendo wake umeonyesha kuwa inatumika kuwasafisha baadhi ya vigogo serikalini.
“TAKUKURU inajipotezea yenyewe imani kwa wananchi kutokana na taarifa zake na kwamba wamekuwa wakiipa changamoto TAKUKURU kuchukua hatua. Mathalani TAKURU kuisafisha Kampuni ya Richmond,” walibainisha.
Baada ya TAKUKURU kubainisha kuwa mkataba wa uzalishaji umeme baina ya serikali na Richmond haukuwa na shaka ya rushwa, bado imeshindwa kueleza: Ni kwanini kamati ya Waziri Mkuu iliipa tenda Richmond baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kuitaka bodi yake ya zabuni kutangaza upya zabuni hiyo kwa kutumia zabuni za kimataifa?
Walisema kuwa kauli ya Waziri Kingunge kwamba wasomi nchini wametathmini uamuzi wa Bunge wa kumsimamisha Mbunge Zitto Kabwe kwa kutanguliza jazba badala ya busara, kuwa ni maoni yake binafsi.
“Tunaamini kwamba kauli hii ni maoni binafsi ya Bwana Kingunge ambayo ni ishara ya kulewa madaraka kutokana kung’ang’ania serikalini toka wakati nchi hii inapata uhuru, kwani hii si mara ya kwanza kutoa kauli za kubeza.
“Tunapenda kumkumbusha Waziri Kingunge maneno ya Shaaban Robert kwamba “Elimu ilipokuwa bado kujulikana, mvi zilihesabika kuwa alama ya hekima, lakini fikra hizo wakati wake umeshapita, haupo na wala hauji tena. Kisichobadilika ni kwamba mtu mzima bado anastahili heshima kutoka kwa mdogo,” walisema.
Walimtaka Waziri Kingunge afahamu kwamba wasomi kama Profesa Issa Shivji na makundi ya kijamii, mathalani Mtandao wa Jinsia (TGNP), Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), walifanya tathmini yao kwa lengo la kulinda masilahi ya taifa bila kujali itikadi.