Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kingunge ashambulia wapinzani
Kingunge ashambulia wapinzani
By Marshy Abdu | Published  09/19/2007 | Habari za Kitaifa | Unrated
Kingunge ashambulia wapinzani
MWANASIASA mkongwe na bingwa wa propaganda za Chama Cha Mapinduzi, Kingunge Ngombale-Mwiru amewashambulia viongozi wa vyama vinne vya upinzani wanaozunguka katika maeneo mbalimbali nchini wakitoa tuhuma nzito dhidi ya viongozi wa serikali.

Kingunge ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Mahusiano ya Jamii) alitoa mashambulizi hayo mazito jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mwanasiasa huyo anayechukuliwa kuwa ndiye mshauri mkuu wa kisiasa wa Rais Jakaya Kikwete, aliwabeza wapinzani akiwaita wachochezi na wazushi, kwa kuwa wanazunguka wakiwahadaa wananchi kuhusu serikali, viongozi wake na chama tawala.

“Hizi jitihada ya kutaka serikali ihangaike, na tuhuma za hewani hazitafanikiwa. Huu ni mkakati wa kisiasa… wanafikiri tutaacha kazi za kuwatumikia wananchi tuwafuate wao,” alisema.

Mbali ya hilo, Kingunge aliwalaumu viongozi wa upinzani kwa kusahau kwamba uhuru wanaoufaidi wa kusema lolote wapendalo haupatikani katika nchi nyingine.

Akitoa mfano, alisema hapa nchini, wapinzani wanaweza kufanya na kuzungumza maneno wanayotaka, kwa kuwa nchi inaendeshwa kidemokrasia.

“Wanaweza kufanya na kusema wanayoyataka na hiyo inatokana na demokrasia ya vyama vingi kuimarika na uongozi wa CCM kuwa uliokomaa na wenye uvumilivu na uwezo wa kuhimili mapigo,” alisema.

Alisema hivi sasa wapinzani hao wamefikia hatua ya kutoa maneno ya kichochezi, lengo likiwa ni kutaka wakamatwe na wakati huo huo akaonya kuwa endapo watakiuka sheria za nchi katika ziara zao, sheria itachukua mkondo wake.

Akirejea suala la rushwa, alisema CCM na serikali yake wamekuwa wakipinga rushwa na akawataka watu walio na ushahidi wa kuwapo kwa viongozi wala rushwa kuupeleka kwenye vyombo husika, ili hatua zaidi zinazofaa zichukuliwe.

Aidha, aliwalaumu wapinzani hao kwa kusema ziara wanayofanya katika mikoa mbalimbali nchini, ina lengo la kuwapotosha wananchi kuhusu kilichotokea bungeni na kusababisha kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA).

Alisema mbunge huyo alikiuka kanuni za Bunge kwa kusema kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alikuwa amelidanganya Bunge, ilhali ukweli haukuwa huo.

“Bunge haliendeshwi kienyeji, linafuata kanuni, na mbunge yeyote anayekiuka kanuni huadhibiwa, na Zitto ameadhibiwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge zinazokataza mbunge kutosema uongo. Sasa imekuwa nongwa, wametoka nje ya Bunge wanasema wameonewa.

“Mbunge wa Sumve na Makete wa CCM, walisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa sababu walikwenda kinyume na kanuni… tunataka kujenga nchi gani kwenda kuwadanganya watu kuwa wameonewa?” alihoji.

Alisema ni jambo lisilowezekana kwa watu wachache wasio na ridhaa ya wananchi wakaendesha nchi, na akasisitiza kuwa iwapo hilo litaachwa, wananchi watakuwa wamefanya kazi ya bure kuwachagua wao.

Alisema kinachowapa tabu wapinzani ni kuona Serikali ya Awamu ya Nne inavyotafsiri na kutekeleza kwa dhati ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

“Mafanikio ya serikali sasa yamekuwa nongwa. Shule zinajengwa, haijapata kutokea, ni mapinduzi makubwa na hata dunia inajua, lakini rafiki zetu hawapendi kusikia hiyo….hawa ni Watanzania?” alihoji.

Kingunge, alisema katika nchi ya demokrasia, baada ya uchaguzi malumbano yanahamia bungeni na kusema kuwa, kupitia Bunge upinzani unaweza kuisaidia sana serikali kwa kuikosoa. Alisema iwapo hawakubali demokrasia iliyopo nchini, watafute nchi ya udikteta.

Alisema serikali inajitahidi kubadilisha maisha ya Watanzania, wapinzani wamekuwa mahodari wa kuwatetea, lakini kwa kuzuia maendeleo yao.

Alitoa mfano kwamba wanawashawishi wananchi kutochangia ujenzi wa shule na akasema kuwa hilo limewezekana kwa kuwashirikisha wananchi.

Akizungumzia suala la katiba, alisema suala hilo ni la kisera, ambalo linapaswa kuwekwa kwenye ilani ya uchaguzi na kwamba katika ilani yao ya uchaguzi hakuna suala hilo.

“Kwa sasa hatuwezi kuzungumza suala la marekebisho ya katiba kwa sababu katika ilani yetu ya uchaguzi haipo, hivyo hatuna cha kuzungumza, labda ingekuwepo kwenye ilani,” alisema.

Wakati Kingunge akitoa maneno hayo, siku chache tu baada ya wapinzani kutaja orodha ya viongozi 11, wa serikali wakiwatuhumu kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, jana alisisitiza kuwa wao wana ushahidi tosha dhidi ya viongozi wanaowatuhumu.

Mbowe aliyekuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja wa NMC, Arusha mjini, alisema iwapo serikali inadhani maneno waliyotoa hawakuwa na ushahidi nayo, basi iwakamate na kuwafikisha mahakamani.

Alisema kuwa vuguvugu la kulinda rasilimali za nchi linaloendeshwa na vyama vya upinzani haliwezi kuzimwa kwa kuvizuia vyombo vya habari kutangaza au kuandika habari zinazowafichua mafisadi.

Mbowe alisema kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita viongozi hao walihutubia wakazi wa Jiji la Dar es Salaam katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, ambapo walitaja majina ya vigogo waliohusika na kile alichokielezea kuwa ni ufisadi na ufujaji wa fedha za umma lakini hakuna chombo chochote cha habari kilichotangaza wala kuandika majina hayo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuyataja tena majina ya vigogo hao, wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ufujaji wa mali ya umma, majina ambayo kwa sababu za kisheria na kuheshimu misingi ya uandishi wa habari, gazeti hili bado haliwezi kuyataja, pamoja na Mbowe kukerwa na hatua hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema kuwa umoja huo wa vyama vya siasa ni makini na wa uhakika, na aliwaambia waliohudhuria mkutano huo kuwa hata wakitaka wachanjiane damu na Mbowe kuthibitisha hilo yuko tayari.

“Namuomba Mungu nisife kabla ya mwaka 2010 ili niweze kuona CCM ikianguka chali… nikiwa kijijini kwangu Kiraracha, nione rais kutoka upinzani… hapo hata Mungu akinichukua nitakuwa nimetimiza wajibu wangu,” alisema Mrema.

Katika hotuba yake, Zitto alizungumzia juu ya mikataba mbalimbali mibovu, hali inayosababisha nchi kupoteza fedha nyingi.

Imeandaliwa na Tamali Vullu, Dar es Salaam na Grace Macha, Arusha.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
This article has been added to your 'Articles to Read' list.
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.