Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Siasa  »  Tulichofanya Kulisaidia Taifa Letu - Najibu Swali la Waziri Mkuu
 »  Home  »  Mzee Mwanakijiji  »  Tulichofanya Kulisaidia Taifa Letu - Najibu Swali la Waziri Mkuu
Tulichofanya Kulisaidia Taifa Letu - Najibu Swali la Waziri Mkuu
By Mzee Mwanakijiji | Published  09/18/2007 | Siasa , Mzee Mwanakijiji | Rating:
Tulichofanya Kulisaidia Taifa Letu

TULICHOFANYA
KULISAIDIA TAIFA



Na.
Mjenga Hoja



Kwanza
kabisa kwa niaba yangu binafsi, na kwa niaba ya Watanzania wengi
waliotawanyika pote duniani natuma salamu za pole kwa Mbunge wa
Mchinga Mhe. Mudhihir Mudhihir kwa majeraha na maumivu aliyoyapata
kufuatia ajali ya gari mwishoni mwa juma lilopita. Mimi kama wengine
tulishtushwa na habari ya ajali hiyo na madhara ambayo yamemfika
ndugu yetu na mwakilishi wa watu. Tunamwombea kwa Mnyezi Mungu
majeraha yapone haraka na yeye mwenye apate nafuu na hatimaye arudi
kwenye utumishi wa Chama cha Mapinduzi na uwakilishi wa jimbo lake
kama mchango wake wa kulitumikia Taifa letu.





Zaidi
ya yote napenda kutuma salamu za heri ya Mfungo mtukufu wa Ramadhani
kwa ndugu zetu Waislamu wote wa Tanzania na tunawatakia safari njema
ya kiroho. Tunawaomba kwa namna ya pekee katika kipindi hiki basi
waiombee nchi yetu hasa katika wakati huu ambapo Taifa letu
linajitahidi kutafuta nafasi yake katika mataifa ya ulimwengu.
Wanapojiombea wao, na familia zao basi watuombee na sisi wengine
ambao kila kukicha tunaiwazia nchi yetu na kuitakia mema, licha ya
umbali uliopo na ardhi ya mama zetu. Watuombee tusikate tamaa wala
kurudi nyuma katika mapambano haya ya kifikra.





Katika
makala yangu ya wiki mbili ziliyopita nilijaribu kuanza kujenga hoja
nikijibu sehemu ya Hotuba ya Waziri Mkuu ambapo alihoji kuwa Hawa
wanaobeza kwamba hatujafanya kitu wajiulize wao wamefanya nini
kuisaidia nchi yetu? Katika makala ile nilionesha kuwa kati ya
maswali matatu yanayoendena ambayo Waziri Mkuu angeweza kuuliza
Bungeni wakati akitoa hoja ya kuliahirisha Bunge la Bajeti 2007/2008
yeye alichagua lililo jepesi zaidi. Maswali ambayo angeweza kuuliza
kwa mfuatano ni hawa wamefanya nini kulisaidia Taifa, wao
hawakufanya nini nini, na wao wangefanya nini kulisaidia taifa?





Katika
sehemu ile ya kwanza niliamua kuanza na sehemu ya nini wao (Waziri
Mkuu) na timu yake wamefanya ambacho sisi hatukukifanya. Hata
hivyo leo, nataka nijibu swali moja kati ya yale mengine mawili
yaliyosalia ambayo ni nini tumelifanyia taifa ambacho wao
hawakukifanya?





Kwa
ufupi ni kuwa ingawa Waziri Mkuu na timu yake hawaoni mchango wa
wakosoaji na watanzania wenye mawazo tofauti, mchango wetu ni mkubwa
kuliko ambavyo serikali iko tayari kukiri au kukubali. Serikali iliyo
makini kweli kweli ni serikali inayosikiliza maneno ambayo yanatoka
nje yake, na ambayo iko tayari kumulikwa siyo kwa mwanga wa ndani tu
bali pia kutoka nje. Inaonekana serikali ya Waziri Mkuu wanataka
kumulikwa na mwanga ambao wao ndio wananunuzi wa kurunzi hizo na
endapo mtu mwingine akija na kurunzi ambayo ina mwanga mkali kidogo
basi anapokelewa kwa kejeli, vitisho, na maneno ya kiunyanyasaji.
Najua hawapendi kukosolewa (hata kama wanasema wako tayari
kukosolewa) sina budi angalau kwa dakika chache kupigia panda
mafanikio ya wakosoaji wa serikali na kuonesha kuwa mchango wetu japo
ni kiduchu matokeo yake si ya kupuuzwa au kubezwa!





Tumeonesha
rangi ya kweli ya viongozi wetu. Kwa yeyote ambaye anafuatilia
uongozi wa Tanzania atagundua mara moja kuwa kama kuna kitu
kinawaudhi sana watawala wetu ni watu kuchezea CCM na kuchezea mali
za CCM. Si hivyo tu, ni rahisi kuona kuwa inapotokea jambo linahusu
CCM au maslahi ya Taifa waamuzi wetu mara zote watachagua CCM kwanza;
kwani kwao maslahi ya CCM na ya Taifa hayatengani na yanapoonekana
kutengana maslahi ya CCM hupewa kipaumbele.





Hayo
yameonekana kwenye masuala ya mikataba ya ya wawekezaji, suala la
rushwa, na utawala wa uwazi na ukweli. Walikuwa wa kwanza kupigia
kelele mikataba na wakataka waione mikataba hiyo, wakaapa kabla ya
kikao cha Bunge kuwa Richmond itazungumzwa na kuna wengine
wakasema liwalo na liwe hatutanyamazishwa this time. Wakapewa
nafasi Bungeni ya kuonesha uthabiti huo wa nia; walipopewa nafasi na
Zitto kuchagua maslahi ya Taifa au yale ya CCM wakagwaya kama kuku
aliyeoneshwa kisu! Wakatimka mbio mbio na kujificha kwenye kanuni za
Bunge!





Walipokuwa
kwenye kampeni zao za uNEC wakabwagwa chini kwani walimtaka Zitto
atulie na atumikie adhabu yake. Ni sisi wakosoaji tulionesha hilo
ndani ya CCM. Leo hii wanaposimama majukwani kutamba, wananchi
wanawasikiliza kwa makini na kuwapima kama wanachosema ni kwa ajili
ya CCM au kwa ajili ya nchi.






Tumeonesha
kuwa Rushwa imekithiri ndani ya CCM. Huko nyuma walikuwa wakingaka
na kukana kama wamemuona Malaika wa kifo. Wakadai CCM safi na
ya kuwa madai ya rushwa dhidi ya chama hicho ni kelele za
wapinzani. Mwalimu aliwaambia CCM inanuka rushwa
hawakukubali, wakosoaji tukasema CCM inanuka rushwa wakakataa,
leo hii wanashikana mashati na kubebana mzobemzobe huku watu wazima
na akili zao wanalia rushwa rushwa na wengine wanadiriki kusema
kuwa CCM isipoangalia uongozi ndani ya CCM utapatikana kwa kutoa
tenda! Tulichokisema kumbe ni cha kweli.





Leo
hii wanakamatana na kufikishana mahakamani, tukiwauliza wanatamba
Tunaonesha mfano na Rais amesema atashughulika na rushwa na
huu ndio mwanzo. Wanachoshindwa kutuambia ni walikuwa wapi miaka
yote hii? Walikuwa wapi kwenye uchaguzi wa 2000 na ule wa 2005?
Walikuwa wapi wakati Benki Kuu fedha zinafujwa kama gunia
linalojaribu kujazwa maji!? Sasa wamebakia kupeana maonyo (kama
kawaida yao. Mfano mzuri ni huko Kilimanjaro ambapo kwa mujibu wa
gazeti mojawapo la Kiswahili (siyo Kulikoni) Waziri Mkuu ametaka
kukomeshwa
kwa tabia ya baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Moshi kujenga
mazingira ya kufanya vikao vingi vya dharura ili kujilipa posho
nyingi. Sasa maonyo kama haya yamekuwa yakitolewa kwa muda mrefu
sasa na ni wao wenye uwezo wa kuchukua hatua. Kwa vile fedha
zinazochotwa ni za Umma na si za CCM, viongozi kama kina Lowassa
hawashtuki sana. Lakini ngoja zile za CCM zichotwe angalau kidogo tu,
hadi Kamati Kuu itaingilia kati!





Ni
sisi wakosoaji ambao tumeonesha vile ambavyo serikali haikutaka watu
wajue. Siyo serikali ya CCM iliyowaambia wananchi kuwa ndege ya Rais
inanunuliwa kwa kiasi cha karibu bilioni 50 na siyo wao waliotuambia
kuhusu ununuzi wa rada kwa karibu bilioni nyingine hamsini. Siyo wao
waliotuambia kuhusu mkataba wa Richmond jinsi ulivyoingiwa na jinsi
ulivyosimamiwa na kwa hakika siyo wao ambao waliwaambia wananchi
kuhusu Mkataba wa Buzwagi na ulaghai wa Karamagi. Ni wakosoaji wa
serikali na wale walio nje ya utawala ndio wamekuwa na ujasiri siyo
tu wa kufuatilia kile serikali inafanya bali pia kukiweka wazi kile
serikali inafanya hata kama watawala wetu wangependa tukimezee.





Ni
hao wakosoaji ambao Waziri Mkuu anadhani wanakejeli walioilazimisha
serikali kutetea mafanikio yake, siyo mara moja bali mara mbili.
Makala ya kupaa kwa Tanzania ilipotoka kwa hakika iliwagusa
watawala wetu na hasa yeye Kiongozi shujaa, mahili, na hodari
aliyetamba Bungeni. Ni kwa sababu hiyo basi Ofisi ya Wazir Mkuu
ilijibu hoja zetu na kuonesha jinsi walivyokerwa wakafikia kutuita
wakimbizi. Tulipowajibu tena kwa hoja, hawakuchelewa kujibu
lakini safari hii wakatumia uwanja mpana zaidi. Ndipo pale Waziri
Mkuu akitumia nafasi ya kuliahirisha Bunge la Bajeti aliamua kujibu
hoja na kutetea kwa nguvu mafanikio ya serikali yake.





Alivyokuwa
akipaza sauti kuwaambia wananchi ni mafanikio gani serikali ya CCM
imeweza kuleta na hasa kuonesha ni nchi ngapi tumezipita Waziri
Mkuu alikuwa anajibu hoja za wakosoaji. Kwa upande mmoja alikuwa
anajaribu kuwanyamazisha wakosoaji hao lakini kwa upande mwingine
wakosoaji hao ndio walimpatia nafasi hiyo! Ni kwa sisi kuhoji ndio
maana wao wakatoa majibu, tungekaa kimya wasingejitahidi kushawishi
umma kuwa Tanzania inapaa!





Tatizo
kubwa ambalo ninaliona ni mawazo kuwa wale wote wanaokosoa serikali
au kuihoji basi hao ni wapinzani. Ukweli ni kuwa si wakosoaji wote
wamefungamana na vyama ya kisiasa ingawa bila ya shaka wengi wetu
tuna mitazamao yetu ya kisiasa na itikadi zetu. Hata hiyo
tunapowakosoa, tunapowahoji na tunapowaonesha mapungufu ya utawala
wao si kwa sababu sisi tunapinga tu kwani ndiyo kazi yetu.
La hasha, tunafanya hivyo kwa sababu tumetofautiana na watawala wetu.
Na tofauti hiyo ni tofauti ya msingi.





Tunatofautiana
na kimtazamao na kimaono. Wakati wao wanafikiri kuwa Tanzania bila
CCM haitawaliki sisi wengine tunaamini kabisa kuwa Tanzania bila CCM
inawezekana. Wakati wao wanataka wapatiwe pongezi kwa mema yote na
mazuri yote ambayo yametokea Tanzania chini ya utawala wao, sisi
wengine tunasema na machafu na uozo wote unaotokea nchini ni wao
wanawajibika! Wakati wao wanaona kuwa Katiba iliyopo ni kamilifu na
hahitaji mabadiliko makubwa (kama siyo kuandikwa upya kabisa) sisi
wengine tunaona matatizo mengi na ya msingi ya kikatiba. Wakati wao
wanatawala kana kwamba kwao uongozi ni haki ya kwao na ya kuwa
wameumbwa ili kututawala sisi wengine tunaendelea kuwakumbusha kuwa
uongozi ni dhamana na cheo ni cha muda tu. Hivyo tunapowakosoa na
kuwaonesha mapungufu yao wanadhania tunawachukia au tunawaona wivu!





Ukweli
ni kuwa tunatofautiana nao sana kimsingi kiasi cha kwamba hatuwezi
kuwafumbia macho! Tunatofautiana nao kimtazamo kiasi cha kwamba
Wakati wao wanataka kuangalia kupitia kioo kilicholoweshwa maji sisi
wengine tunataka kuondoa kabisa kioo hicho na kuwafanya waangalia kwa
kitu halisi.





Hivyo
tunavyoendelea kutafakari mustakabali wa Taifa letu, watawala wetu
watambue kuwa hatuaacha kuwakosoa na siyo tu kuwakosoa bali pia
kukusudia kuwatoa kwenye nafasi zao za uongozi na utawala ili watu
wengine ambao wana uwezo wa kuliongoza Taifa letu wapate nafasi.
Walizoea kutoa vitisho na kebehi lakini sasa hivi hawawezi kutupuuzia
tena, kwani wakipuuza ni wao watakaojikuta wanatahayarika na gharama
ya kutupuuza ni mabango waliyokutana nayo huko Buzwagi na Dodoma!
Hawawezi kudhania kuwa kosoa zetu ni kejeli tena, kwani wakifanya
hivyo itakuwa ni kwa hasara yao wenyewe.





Kwa
maneno mengine, tungelikuwa sisi wao tusingewapuuzia wakosoaji wetu,
kwani ni wao ndio wanatuonesha mambo ambayo waliokaribu yetu
hawatuoneshi. Tulichokifanya wanakijua ingawa hawako tayari kukiri,
mchango wetu wanautambua ingawa hawataki kukubali, na mawazo yetu
wanayatambua ingawa huwa wanayatumia kisirisiri. Wakati umefika wao
kuanza kukubali michango ya wakosoaji na siyo kudhania ni kejeli.





Na
katika hili wakati umefika kwa vyombo vyetu vya habari kuanzia kutoa
nafasi kwa msemaji wa upinzani kujibu hotuba ya Rais anayoitoa kila
mwisho wa mwezi. Kutoa nafasi kwa watu wenye mawazo tofauti ni jambo
zuri na lenye maana. Pindi Rais akijua anachotaka kuzungumzia watu wa
Ikulu wawasiliane na uongozi wa kambi ya upinzani ili na wenyewe
angalau kama Rais ametumia dakika 15 kuhutubia basi mara akimaliza
msemaji wa kambi ya upinzani naye apewe angalau dakika 5 kwenye
vyombo vile vile vilivyorusha hotuba ya Rais. Yote hiyo itachangia
katika kutoa mawazo na kubadilishana mawazo na kuwasaidia wananchi
kuelewa masuala mbalimbali kwa mitazamo mbalimbali nwa kwa kufanya
hivyo tutakuwa tunakoleza demokrasia. Wapinzani nao wadai nafasi
hiyo.





Wiki
ijayo, nitamalizia mfululizo wa makala hii kwa kujibu swali la mwisho
nalo, ni tungelikuwa sisi kwenye nafasi yao, tungelifanya nini
ambacho wao hawajathutu kufanya na hawako tayari kufanya?





Niandikie:
mjengahoja@jamboforums.com


Niachie
ujumbe: 1 248 686 2010






How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by Japhari Shabani)
    Rating
    hii yote ni kweli CCM na Serikali wamepitwa na wakati wanaishi katika dunia ya sasa lakini mawazo yao nikatika enzi za Abunwasi
     
Submit Comment


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.